Friday, April 13, 2012

MWENYEKITI CHAMA CHA CHADEMA MONDULI ALIA NA HUKUMU YA LEMA


NA GLADNESS MUSHI WA FULLSHANGWE- ARUSHA


MWENYEKITI  wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA,wilaya ya Monduli  ,Amani Silanga  amesema kuwa hukumu iliyotolewa ya kutengua  nafasi ya ubunge wa Arusha mjini ni kipimo tosha kinachowapa nguvu wabunge wa chadema waliotukanwa  na kudhalilishwa katika chaguzi mbalimbali zilizopita ,kufungua kesi mahakamani.

Silanga aliyesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa,kuhusiana na hukumu iliyomuengua aliyekuwa mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema baada ya mahakama kuu kumtia hatiani kutokana na maneno ya udhalilishaji na kashfa dhidi ya mgombea mwenzake.,Dkt Batilda Burian.

Alisema kuwa katika uchaguzi mkuu  wa mwaka 2010 ,wabunge wegombea wengi wa chadema walitukanwa natusi makubwa na kudhalilishwa na wenzao waCCM lakini hawakufikia hatua ya kufungua kesi mahakamani ya kulalamikia hatua hiyo ,na waliona ni sehemu ya kampeni za kisiasa.

‘’unajua siasa za kukashifiana zilianzishwa na wana CCM wenyewe  miaka ya nyuma,hata sisi wapinzani tumerithi kutoka kwao ,kwani wakati upinzani unaanza walitutukana sana na kuonekana kama  adui katika jamii na wengine walithubutu hata kututukania wazazi wetu lakini tulidharau ‘’alisema

Aliwashauri  wagombea wengine wa kutoka vyama mbalimbali vya siasa walioangushwa kwa sababu ya kutukanwa na kufedheheshwa ,kutovumilia hali hiyo na wafungue kesi mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake na  wajue iwapo hii sheria ilikuwa ni kwa ajili ya Lema pekee ama ipo kwa kila mgombea yoyote.

Hata hivyo aliwasihi majaji na mahakimu kuwa makini katika kufuata sheria pindi wanapotoa hukumu hususani  kesi za uchaguzi kwa kuzingatia sheria zaidi ili kuepusha migogoro isiyorasimi ndani ya jamii.
Silanga aliwataka majaji wanaosikiliza kesi hizo kumweka mungu mbele  na kuogopa kutenda dhambi ya wazi pale baadhi yao wanapoamua kupindisha sheria kwa maslahi ya kuufurahisha upande mmoja,jambo ambalo linahatarisha amani ya nchi na kufanya wananchi wazichukie mahakama zao.

Aidha alizisihi mahakama hapa nchini kuacha kurubuniwa ama kuingiliwa na chombo chochote ama mtu binafsi katika kutoa maamuzi na badala yake zifuate kanuni na sheria zilizopo bila kufanya upendeleo wa  upande wowote.

Hata hivyo wananchi mbalimbali katika jimbo la Arusha mjini wamekuwa na maoni kuwa hukumu hiyo haikuwashtua kwani wanakumbukumbu ya miaka ya nyuma ambapo kila mpinzani anapochaguliwa kuongoza jimbo hilo amekuwa akienguliwa na mahakama na baadae uchaguzi kurudia kwa mara nyingine tena.

Wakitolea mfano ,Makongolo Nyerere aliyechaguliwa kuwa mbunge wa Arusha mjini kupitia chama cha NCCR mageuzi mwaka 1995,ambapo ubunge wake ulidumu kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya mahakama kumwengua kwenye wadhifa huo.

No comments: