Friday, April 6, 2012

Ofisi ya Mbunge Arusha yazingirwa kabla ya hukumu


Peter Saramba na Mussa Juma, Arusha
POLISI mkoani hapa, jana waliizingira ofisi ya mbunge wa Jimbo la Arusha na kuzuia watu kuingia ndani ya ofisi hizo kuanzia Saa 1:00  asubuhi, muda mchache kabla ya kutangazwa kwa hukumu ya kutengua ubunge wa Godbless Lema iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Pamoja na kuzingira ofisi ya mbunge na kuzuia watu kuingia, polisi pia walizingira viwanja vya mahakama kuanzia Saa 1:00 asubuhi huku ikizungusha uzio maalumu wenye kuzuia watu kuvuka eneo la majengo ya mahakama hiyo.
Licha ya kuweka uzio, polisi pia waliimarisha ulinzi kwa kuleta
mahakamani zaidi ya magari 10 yaliyojaa askari wakiwamo askari wa kikosi cha mbwa ambao muda wote walikuwa wakirandaranda ndani na nje ya viwanja vya mahakama.

Ndani na nje ya ukumbi wa mahakama pia walijaa askari kanzu ambao muda wote walikuwa wakijitahidi kusogelea kila kundi la watu zaidi ya moja kujaribu kusikia na kunasa maongezi yao.

Maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wakiongozwa na Naibu Mkuu wa Idara hiyo Mkoa wa Arusha, Selemani Mombo pia ni miongoni mwa watendaji na maofisa wa Serikali waliojazana ndani na nje ya viwanja vya mahakama jana kabla na baada ya hukumu kutolewa.
Akizungumzia polisi kuzingira ofisi yake asubuhi na mapema kabla ya hukumu kutolewa, Lema alionyesha shaka na kitendo hicho kuwa kinadhihirisha uamuzi wa Jaji Gabriel Rwakibarila ulishajulikana kwa wana CCM na vyombo vya dola, jambo alilodai linatia shaka.

 “Walijuaje kwamba mimi nitavuliwa ubunge hadi wavamie ofisi ya mbunge na kuzuia watu kuingia. Walipata hofu gani hadi kuleta polisi wengi mahakamani kuliko hata idadi ya wasikilizaji waliohudhuria? Maana yake ni kwamba walishajua ubunge wangu unatenguliwa na walitarajia wana Chadema wangeleta vurugu au kufanya fujo,” alisema Lema.

Kikosi cha ulinzi cha polisi mahakamani jana kiliongozwa na
Kamanda wa Operesheni maalumu wa polisi Mkoa wa Arusha, Peter Mvulla ambaye alihakikisha askari wake hawaingii kwenye malumbano wala
mapambano na wana Chadema waliojawa jazba na hasira baada ya hukumu kutolewa.

“Hakuna haja ya kukabiliana wala kuwanyamazisha watu wanaoonyesha
hisia zao kwa mbunge wao kuvuliwa ubunge, waacheni wazungumze watakavyo kama hakuna uvunjifu wowote wa amani na utulivu. Wala msiingilie msafara wa mheshimiwa Lema anayetembea kwa miguu kwenda ofisini kwao Ngarenaro,” alisikika akitoa amri Kamanda Mvulla kupitia
radio ya upepo.

Kamanda huyo mwenye uzoefu wa kusimamia ulinzi mara nyingi panapotokea
mvutano kati ya wana Chadema na polisi pia alionekana kupuuza
maelekezo ya Naibu Ofisa Usalama Mkoa wa Arusha, Selemani Mombo aliyemtaka kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wamekusanyika mbele ya geti la kuingilia mahakamani wakifanya mahojiano na kundi
kubwa la waandishi wa habari waliokuwapo eneo hilo.

“Nadhani kuanza kuwahimiza kutawanyika ni kuamsha hisia kwamba wanaingiliwa kwenye haki ya kuonyesha hisia za kumpoteza mbunge wao.
Mie naamini hadi sasa hakuna sababu yoyote ya kuwatawanya watu hasa ukizingatia ukweli kwamba wengi wao wanafanya mahojiano na waandishi wa habari. Labda tuwaombe waandishi ndio wasogee pembeni kidogo kupisha barabara ili magari yapite kirahisi,” alisikika akisema Kamanda Mvulla akimjibu Mombo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Thobia Andengenye alisema jana kuwa uwingi wa polisi kila sehemu muhimu katika mitaa ya Jiji la Arushahaikuhusiana kwa njia yoyote na kujua hukumu ya mahakama, bali
ulilenga kuhakikisha usalama wa watu na mali zao, ambalo ndilo jukumula msingi.

No comments: