Saturday, April 7, 2012

Simba raha tu, yawanyoosha Waarabu



MABAO mawili ya kipindi cha pili ya Emmanuel Okwi na Haruna Moshi yaliiwezesha Simba jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya ES Setif ya Algeria kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Hudu Munyema kutoka Rwanda ulishuhudiwa timu hiyo kutoka Algeria ikijihami muda mwingi wa mchezo huo hasa kipindi cha kwanza, huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza yaliyodhibitiwa vyema na mabeki wa Simba na kipa Juma Kaseja.

Simba iliyokuwa inacheza mchezo wa kushambulia kwa nguvu ilikosa nafasi nyingi za kufunga hasa kipindi cha kwanza kwa washambuliaji wake Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Patrick Mafisango kushindwa kuzitumia nafasi hizo.

Dakika ya kwanza ya mchezo, Yousef Ghezari alimtoka beki Amir Maftah na kupiga krosi iliyookolewa Simba na Juma Kaseja. Simba ilijibu dakika ya nne kwa shambulizi lililofanywa kwa ushirikiano wa Shomari Kapombe na Mafisango, lakini Sunzu alishindwa kumalizia kwa kupiga shuti lililotoka nje ya lango.

Dakika moja baadaye Salumu Machaku aliwatoka walinzi wa Setif na kupiga krosi, lakini Okwi na Mafisango walichelewa na mpira kutoka nje ya lango.

Machaku tena dakika ya 9 alipiga krosi, lakini Sunzu alipiga kichwa kilichopaa juu ya lango la Setif. Setif walifanya shambulizi la kushtukiza dakika ya 12, lakini mabeki wa Simba Kelvin Yondani na Juma Nyosso walimdhibiti Yousef Sfiane aliyekuwa anaenda kumuona Kaseja.

Kipindi cha pili Setif kama kawaida yao walionekana kucheza kwa kutaka sare, huku Simba wenyewe wakiongoza kasi yao ya mashambulizi zaidi ya walivyocheza kipindi cha kwanza.

Dakika ya 73 Okwi aliifungia Simba bao la kuongoza baada ya shuti kali alilopiga nje ya eneo la penalti kuwagonga mabeki wa Setif na kutinga wavuni.

Baaada ya bao hilo Setif waliokuwa wamejazana nyuma na katikati ya uwanja kama mbinu yao ya kujihami walifunguka na kufanya mashambulizi kadhaa yaliyoipa Simba nafasi ya kufunga bao la pili kwani dakika ya 81 mfungaji akiwa Moshi.

Alifunga bao hilo baada ya mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Machaku kuwagonga mabeki wa Setif na kumkuta Moshi aliyepiga shuti kali lililotinga wavuni.

Kutokana na matokeo hayo, Simba imejiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele, ambapo mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo nchini Algeria itakuwa inahitaji sare au isifungwe zaidi ya bao 1-0.

No comments: