Saturday, April 14, 2012

Simba safari bado ndefu Afrika

Image
Kikosi cha Simba.WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika soka la kimataifa, Simba ya jijini Dar es Salaam, imetinga hatua ya timu 16 bora ya mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), baada ya kuitoa ES Setif ya Algeria.

Simba haikufuzu kirahisi katika hatua hiyo kwani ilifanikiwa kwa faida ya bao la ugenini baada ya timu hiyo kushinda 2-0 katika mchezo wa awali uliofanyika nyumbani na baadae kufungwa 3-1 katika mchezo wa marudiano ugenini.

Baada ya matokeo kuwa 3-3 baada ya mechi hizo mbili, Simba walisonga mbele kufuatia faida ya bao la ugenini. Mchezo unaokuja: Wekundu hao wa Msimbazi baada ya kuwafungisha virago ES Setif ya Algeria, sasa imepata nafasi ya kukwaana na timu nyingine ya Waarabu,
lakini sasa ni kutoka Sudan.

Simba sasa katika hatua hiyo ya 16 bora itacheza na El Ahly Shandy ya Sudan baada ya Wasudani hao kuwafungisha virago vijana wa Msumbiji, Ferroviario.

Kama walivyocheza na Algeria, Simba dhidi ya Sudan wataanza kampeni zao za kusonga mbele katika mashindano hayo kwa kucheza nyumbani kwenye uwanja wa Taifa Jumapili Aprili 29 mwaka huu, kabla ya kurudiana ugeni kati ya Mei 11, 12 na 13.

Kazi Ngumu:
Simba pamoja na kufanya kazi ngumu huko nyuma na kuiwezesha kufuzu kwa hatua hiyo, wawakilishi hao wa Tanzania bado wana kazi ngumu mbele yao ili kuwawezesha wanafanya vizuri kabla hawajafuzu kucheza hatua ya nane bora.

Wengi walifikiria kuwa, baada ya Simba kuwatoa Waalgeria, sasa kazi imebaki kuitoa El Ahly Shandly ya Sudan tu kabla haijafuzu kwa hatua hiyo ya makundi, ambayo hushirikisha
jumla ya timu nane bora.

Hata hivyo, sio hivyo kama walivyofikiria wengi, kwani Simba sasa endapo itawatoa wawakilishi hao wa Sudan itabidi kucheza kwanza na moja ya timu zitakazotolewa katika hatua ya nane bora ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, ili nayo iweze kufuzu kucheza hatua hiyo inayofuata.

Ligi ya Mabingwa:
Timu nane zitakazopigwa chini katika hatua ya 16 ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, zitashuka katika mashindano ya Kombe la Shirikisho na mojawapo itacheza na Simba katika kinyang’anyiro cha kucheza nane bora.

Ndio maana ukitafakari kwa kina na jinsi soka lilivyo, Simba bado wana kibarua kigumu mbele yao ili waweze kufuzu kwa hatua ya nane bora ya mashindano hayo ya Afrika na sio kama
wengi walivyokuwa wakifikiria awali kuwa, ikiitoa timu hiyo ya Sudan, watafuzu kwa makundi.

Endapo Simba itafanikiwa kuwatoa Wasudani na baadae kuitoa timu watakayopangiwa ambayo itatokea katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika, hapo Simba itakuwa imefuzu moja kwa moja kucheza hatua ya makundi na kujipatia donge nono kwa ajili ya maandalizi.

Hivyo si sahihi kwa mashabiki kuanza kuchekelea kwa kuamini wakiifunga Sudan wanaingia hatua ya makundi, badala yake bado wanatakiwa wajifunge kibwebwe.

Uzoefu wa Simba:
Pamoja na uzoefu iliyonayo Simba katika mashindano ya kimataifa na hasa rekodi yake nzuri ya kuzifunga timu za Waarabu, bado timu hiyo inatakiwa ijiandae vizuri ili kuwandoa Waarabu hao wa Sudan.

Simba wamekiri kuwa hawaijui kabisa timu hiyo ya Sudan, lakini wameanza kufanya jitihada kuhakikisha wanapata mikanda yao ya video ili kujaribu kuisoma. Huko nyuma, vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, waliwahi kuzifunga kwa nyakati tofauti timu za Al Ahly, Mehalla Elkubra, Ismailia, Arab Contractors, Al Hadood na Zamalek za Misri.

Pia, kikubwa Simba waliwavua ubingwa wa Afrika Zamalek na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi mwaka 2003. Mbali na kuitoa ES Setif baada ya kuifunga 2-0 katika mchezo wa kwanza na baadae kuchapwa 3-1, Simba miaka ya nyuma iliwahi kuitupa nje ya mashindano ya Afrika timu nyingine ya Algeria ya Al Harrachi.

Hii ni mara ya pili kwa Simba kucheza na klabu kutoka Algeria baada ya mara ya kwanza kuifungisha virago Al Harrach mwaka 1993 walipochuana katika mashindano ya Kombe la CAF.

Mwaka huo wa 1993, Simba ilifanya vizuri katika mashindano ya CAF hadi kucheza fainali lakini walitolewa na Stella Abidjan ya Ivory Coast tena kwa kufungwa nyumbani 2-0 baada ya kutoka suluhu ugenini.

Kushangilia Ushindi:
Simba baada ya kuifungisha virago klabu ya Algeria, waliporejea nchini walipata mapokezi ya kufa mtu kama vile timu hiyo imepata tiketi ya kucheza hatua ya nane bora ya mashindano hayo ya CAF.

Hakukuwa na haja ya kuipatia Simba mapokezi makubwa kama yale wakati timu hiyo bado ina kazi kubwa sana mbele yao. Mwaka 2003 Simba walifanyiwa mapokezi makubwa baada ya kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika tena baada ya kuwafungisha virago Zamalek waliokuwa mabingwa watetezi.

Kwa wakati ule mapokezi yale yalistahili kabisa na hakukuwa na sababu za kutofanya hivyo, kwani tayari walishafuzu kucheza hatua ya nane bora ya mashindano hayo ya Afrika, lakini
kwa hili la sasa wala siliungi mkono.

Salamu za pongezi zilitosha sana kuwapa timu hiyo ili wapate moyo zaidi na kujua kuwa mbele yao bado kuna kazi ngumu kabla ya kufuzu kucheza hatua ya nane bora ya mashindano hayo.

Angalizo:
Simba sasa inatakiwa kufanya haraka kusaka mikanda hiyo ya Wasudani ili kuweza kuisoma mapema timu hiyo. Kingine ni kuachana na pongezi zisizo na msingi ambazo zinaweza hata
kuwavimbisha vichwa wachezaji hao na kuwafanya kubweteka na kusahau kabisa majukumu yaliyomo mbele yao.

Kinachotakiwa ni kuwawekea Simba mazingira mazuri kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ujao kiakili na kimwili, ili waweze kufanya vizuri na kufika mbali katika mashindano hayo, huo ndio utakuwa msaada mkubwa kwa wachezaji wa timu hiyo.

No comments: