Wednesday, May 2, 2012

Collapse all Expand all Print all In new window SERIKALI YATAKIWA KUPUNGUZA UGUMU WA MAISHA KWA WANANCHI

 
Na Gladness Mushi wa Fullshangwe-Arusha


SERIKALI imetakiwa kuunda   mpango wa muda mfupi utakaoweza kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi kutokana na mfumuko wa bei unaoendelea hivi sasa hapa nchini.
 
Hayo yalisemwa na Mchumi, mtafiti na mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Honest Ngowi alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wananchi, yaliyokuwa yameandaliwa na Shirika la Hakikazi Catalyst la jijini hapa, yaliyowashirikisha wananchi wa ngazi mbalimbali kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
 
Dk Ngowi alieleza kuwa  mfumuko wa bei unaongeza ugumu wa  maisha kwa ongezeko la bei la mara kwa mara na hivyo kupunguza uwezo wa watu kununua bidhaa na huduma kutokana na mapato yao kutoongezeka, unaweza kutatuliwa kwa muda mfupi na wa kati, iwapo serikali na wad au watadhamiria kufanya hivyo.
 
 Alisema swala  muhimu ni kupunguza athari za mfumuko wa bei kwa makundi yote likiwemo la wafanyakazi kwa kuongezewa mishahara inayoendana na hali halisi ya ugumu wa maisha.
 
“Hii ni kwa sababu kama mfumuko wa bei unaongezeka bila kuongeza kipato cha mfanyakazi ugumu wa maisha utazidi. Suluhisho lingine ni kwa serikali kupanga na kusimamia bei za bidhaa muhimu kama vile chakula, usafiri na madawa.” Alisema.
 Aliongeza kuwa njia nyingine ya kupunguza mfumuko wa bei  ni  serikali kutoa ruzuku kwa baadhi ya huduma na bidhaa muhimu kwani itapunguza bei anayolipa mnunuzi kwa sababu sehemu ya bei hiyo hulipwa na serikali, kama vile ruzuku inayofanywa kwa pembejeo za kilimo au vyandarua.
 
Akizungumzia jawabu la kudumu la mfumuko wa bei, Ngowi alisema kati ya mkakati mkubwa na endelevu wa kudhibiti mfumuko huo ni kushughulikia masuala ya kimfumo yanayosababisha mfumuko wa bei.
 
“Masuala haya ya kimfumo ni pamoja na kushughulikia na kutatua tatizo la umeme, miundombinu kwa maana ya barabara, madaraja na hata masoko kwa ujumla lakini sana kwa ajili ya kusafirisha pembejeo za kilimo cha mazao ya chakula na mazao yakishazalishwa,”  alisema.

 
Alisema kuna haja pia ya kushughulikia uimarishaji wa thamani ya shilingi ili kupunguza mfumuko wa bei unaotokana na kushuka kwa thamani ya shilingi.
 
Mhadhiri huyo alisema suala hilo linawezekana kwa kuweka mazingira yatakayowezesha kuongeza uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi na kupunguza manunuzi yasiyo ya lazima toka nje ambayo hupunguza fedha za kigeni na kufanya shilingi kuwa dhaifu.
 
Kuhusu mambo ambayo serikali imefanya na kama ni sahihi, Ngowi alisema serikali kupitia Benki Kuu (BoT), imekuwa ikijaribu kupunguza mfumuko wa bei kwa kutumia sera za kifedha.
 
Alisema hili limefanyika kwa kupunguza fedha katika mzunguko ambayo ni njia mojawapo ya kupunguza mfumuko wa bei unaotokana na kuwa na fedha nyingi kupita kiasi katika mzunguko.
 
Alieleza kuwa  kwa Tanzania, tatizo kubwa linalopelekea mfumuko wa bei kuongezeka sio kuwa na fedha nyingi katika mzunguko bali ni masuala ya uzalishaji na usafirishaji.

No comments: