Saturday, May 5, 2012

KING RASHID YEKINI AFARIKI DUNIA

Rashidi Yekini 01
Rashid Yekini 1994 baada ya kufunga dhidi ya Bulgaria


MMOJA wa washambuliaji maarufu wa zamani Nigeria, Rashidi Yekini amefariki dunia. Yekini amefariki jana Ijumaa na mwili wake umepelekwa Offa, mji wa nyumbani kwao Kwara.  
Yekini ni mfungaji bora wa kihistoria wa mabao katika timu ya taifa ya Nigeria, akiwa amefunga mabao 37 katika mechi 58.
Atakumbukwa kwa staili yake ya kushangilia mabao, baada ya kuifungia bao la kwanza kabisa Nigeria katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 dhidi ya Bulgaria. 
Hilo lilikuwa bao lake la mwisho kufunga kwenye fainali za Kombe la Dunia, ingawa alikuwepo pia kwenye Fainali za michuano hiyo mwaka 1998.
Yekini alianzia soka yake katika klabua ya UNTL ya Kaduna kabla hajahamia IICC Shooting Stars, ambako huko ndiko alikoonekana timu ya taifa na kuibuka shujaa wa mabao. 
Amecheza Fainali nyingi za Kombe la Mataifa ya Afrika kaunzia 1984 hadi 1994 nchini Tunisia, ambako Super Eagles ilitwaa taji hilo.
Yekini alikuwa anafahamika kama mtu mstaarabu, muungwana, anayepnda mazoezi, ibada, akiwa anasali katika msikiti wa Ibadan, alikokuwa anaishi. 
Alikuwa hapendi 'misifa' na alijiweka kando kabisa na Waandishi wa Habari na hakuwa kimbelembele kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa zamani.
Yekini atakumbukwa kama mchezaji babu kubwa, ambaye faraja yake kubwa uwanjani ilikuwa ni kuwaokotesha makipa mipira nyavuni. Amefariki akiwa ana umri wa miaka 48.

No comments: