Saturday, May 5, 2012

SIMBA WATWAA UBINGWA NJE YA UWANJA, AZAM FC WAONYESHWA HAWAJUI

Kikosi cha Simba kilichotwaa ubingwa leo kikiwa kambini Zanzibar, baada ya Mtibwa Sugar kuituliza Azam kwa kichapo cha mabao 2-1.

SIMBA leo wanaanza kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya Azam FC kufungwa mabao 2-1 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ina pointi 59, ambazo sasa haziwezi kufikiwa na timu yoyote msimu huu na imebakiza mechi moja dhidi ya watani wa jadi, Yanga Jumapili ambayo kwao itakuwa ya kulinda heshima tu.
Lakini Azam tayari imejihakikishia nafasi ya pili kwenye ligi hiyo na hivyo kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwakani.
Waliokuwa mabingwa watetezi Yanga, hawana tena chao- kwani hata wakiifunga Simba keshokutwa watabaki nafasi ya tatu tu, hivyo mwakani hawavuki mipaka ya nchi.
Tumaini pekee la Yanga kucheza michuano ya Afrika mwakani ni iwapo Simba SC itaingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu- ikiwa imebakiza mitihani miwili kufikia mafanikio hayo.
Inatakiwa kuitoa Al Ahly Shandy ya Sudan- na baadaye iitoe timu itakayokutana nayo kwenye mchujo wa kuwania kucheza hatua hiuyo, ambayo itakuwa imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa.
Hapo, Tanzania itakuwa na nafasi mbili kwenye Kombe la Shirikisho mwakani, kwa mujibu wa kanuni mpya za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Tayari Simba imeifunga Shandy mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza na inahitaji sare katika mchezo wa marudiano wiki ijayo ili kusonga mbele.
Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko, tayari Mtibwa walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Awadh Issa dakika ya 25, wakati kipindi cha pili, Wakata Miwa hao wa Manungu waliokuwa wanashangiliwa kwa nguvu na mashabiki wa Simba, walipata bao la pili dakika ya 59, mfungaji akiwa ni Juma Abdul.
Awadh alifunga bao lake akiunganisha kona iliyochongwa na nyota wa mchezo wa leo, Juma Abdul ambaye naye alifunga bao la pili kwa mpira wa adhabu, baada ya Luckson Kakolaki kumchezea rafu Vencent Barnabas Saramba. John Raphael Bocco 'Adenauor' aliifungia Azam bao la kufutia machozi.

MABINGWA WA JUMLA LIGI KUU:
1965 : Sunderland (Dar es Salaam)
1966 : Sunderland (Dar es Salaam)
1967 : Cosmopolitans (Dar es Salaam)
1968 : Yanga
1969 : Yanga
1970 : Yanga
1971 :  Yanga
1972 : Yanga
1973 : Simba
1974 : Yanga
1975 : Mseto SC (Morogoro)
1976 : Simba
1977 : Simba
1978 : Simba
1979 : Simba
1980 : Simba
1981 : Yanga
1982 : Pan African
1983 : Yanga
1984 : Simba
1985 : Yanga
1986 : Tukuyu Stars (Mbeya)
1987 : Yanga
1988 : Coastal Union (Dar es Salaam)
1989 : Yanga
1990 : Simba 
1991 : Yanga
1992 : Yanga
1993 : Yanga
1994 : Simba
1995 : Simba
1996 : Yanga
1997 : Yanga
1998 : Yanga
1999 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
2000 : Mtibwa Sugar (Morogoro) 
2001 : Simba
2002 : Yanga
2003 : Simba
2004 : Simba
2005 : Yanga
2006 : Yanga
2007 : Simba (Ligi Ndogo)
2008 : Yanga
2009:  Yanga
2010: Simba SC
2011: Yanga SC
2012: Simba SC

No comments: