Wednesday, June 13, 2012

MUNGU TUSAIDIE VENGU WETU APONE



Na Mwandishi Wetu
WAKATI afya ya staa wa filamu Bongo, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ikiendelea vizuri baada ya kupata matibabu nchini India, kuna utata juu ya maendeleo ya afya ya mchekeshaji maarufu nchini, Joseph Shamba ‘Vengu’ ambaye naye yuko nchini humo kwa matibabu, Risasi Mchanganyiko lina kitu cha kueleza.
Habari ambazo hazina ganzi hata chembe zinadai kuwa hali ya msanii huyo wa Kundi la Orijino Komedi imekuwa ya giza mbele ambapo nduguze waishio Dar hawajui nini kinaendelea.
Katikati ya mwezi Mei, ilidaiwa Vengu angerejea nchini wakati wowote baada ya afya yake kutengemaa, lakini ndugu mmoja wa karibu (jina lipo) akasema imeshindikana kuruhusiwa baada ya hali ya msanii huyo kubadilika ghafla.
“Ilikuwa arudi nyumbani kweli, maana kidogo alikuwa anaridhisha, lakini ghafla hali ikabadilika tena, kwa hiyo hatarudi kwa sasa,” alisema ndugu huyo.
Kwa mujibu wa habari za ndani, hali ya Vengu ni kama bahari kupwa na kujaa, kwani kuna wakati analeta matumaini lakini ‘vikicharuka’ anakuwa kama alivyoondoka Tanzania.
Awali Vengu alilazwa kwa muda mrefu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) akikabiliwa na ugonjwa uitwayo Brain au Cerebral Atrophy. Ugonjwa huu husababisha seli za kichwani kukosa mawasiliano na sehemu nyingine na mgonjwa huzimia mara kwa mara.
Akiwa hospitalini hapo, hali ilizidi kuwa mbaya hivyo ‘komediani’ huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Apolo iliyopo nchini India kwa matibabu zaidi.
Kwa upande wake, Sajuki alikwenda Mumbai, India katikati ya Mei mwaka huu kutibiwa matatizo ya uvimbe tumboni. Alirejea Bongo, Juni 6 mwaka huu akiwa anaendelea vizuri.

No comments: