Sunday, October 7, 2012

SIR ALEX FERGUSON AMSIFIA DE GEA NA KUENDELEZA FOMULA YAKE YA KUBADIRISHA MAKIPA KILA MECHI!

Ingawa Sir Alex Ferguson amemsifia Kipa wake David De Gea kwa kudaka vizuri kwenye Mechi ya UEFA CHAMPIONS LIGI hivi juzi katikati ya Wiki walipocheza huko Romania na CFR Cluj na kushinda bao 2-1, Meneja huyo wa Manchester United amesema ataendelea kuwabadili Makipa katika Mechi zijazo.
De Gea, Miaka 21, aliejiunga na Man United Msimu uliopita, aliachwa baada ya kucheza Mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu England Msimu huu na namba yake kupewa Anders Lindegaard, Miaka 28, kwenye Mechi 4 za Ligi ingawa De Gea alirudi tena na kucheza Mechi ya UEFA CHAMPIONZ LIGI na CAPITAL ONE CUP dhidi ya Newcastle.
Mechi ijayo ya Man United ni ile ya Ligi Jumapili huko Sport Direct Arena ambapo wataivaa Newcastle na ni juu ya Ferguson kuamua amchezeshe Kipa toka Spain De Gea au Lindegaard kutoka Denmark.
Kuhusu hilo, Ferguson ametamka: “Yeye De Gea alicheza vyema na Cluj, ni Kipa mzuri sana, bado Kijana na anazidi kuimarika. Sijajua kama nitamchezesha yeye au la lakini tulichokuwa tukifanya katika Wiki chache zilizopita kimeenda vyema.”
Aliongeza: “Kila Mtu anataka kucheza na Makipa sio tofauti. Lakini ninachotizama sasa ni kuwapa uzoefu wote kitu ambacho kitatusaidia katika malengo ya muda mrefu. Ni wazi utafika wakati mmoja wao ndio atakuwa Namba wani akionyesha uimara mfululizo na akikomaa. Kwa sasa wote bado hawana uzoefu wa Mechi kubwa kabisa. Na hilo watalipata baada ya muda!”
Akizungumzia Makipa kucheza wakiwa na umri mkubwa, Ferguson alimtaja Kipa wake Edwin van der Sar aliestaafu Mwaka 2011 akiwa na Miaka 40 na akaongeza: “Peter Schmeichel alikuwa na Miaka 27 alipojiunga nasi na kila Mtu alimzungumzia kuwa ni Kijana wakati alikuwa na Miaka 27 lakini alitupa Miaka 8 ya uchezaji bora. Makipa wanaweza kucheza hata wakiwa na umri mkubwa sana wa kukaribia Miaka 40. Mtazame Brad Friedel, na Peter Shilton kwenye Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 1990, alikuwa na Miaka 40!”

No comments: