ILI kukomesha vitendo vya uhamiaji haramu unaofanywa na baadhi ya raia kutoka nchi za Pembe ya Afrika, Serikali imeanzisha Kitengo maalumu ambacho kazi yake itakuwa ni kufanya doria na kusimamia usalama wa mipakani.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salam jana, na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isack Nantanga wakati alipokuwa akizungumzia wimbi kubwa la wahamiaji kuingia nchini wakitokea katika nchi hizo.
Alisema Kitengo hicho maalumu kitafungua ofisi zake karibu nchi nzima katika maeneo ya mipaka kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mara kwa mara huku kikishirikiana na wananchi wanaoishi karibu na mipaka.
Nantanga alibainisha kuwa Kitengo hicho kitakuwa na kiongozi ambaye ngazi yake ya kiungozi atajulikana kwa cheo cha Kamishina.
Aidha, alisema licha ya juhudi za serikali za kupambana na wimbi hilo bado kumekuwa na baadhi ya raia wa pande zote, kule wanakotoka na wanakokwenda kujiingiza katika biashara haramu ya usafirishaji wa wahamiaji hao.
“Kwa kuwa suala hilo linafanyika, serikali italifanyia uchunguzi kama ilivyo kwa dunia nzima inavyopambana na biashara haramu ya binadamu na wote wanaohusika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria”alisema Nantanga.
Alisema katika kuhakikisha kuwa inamaliza tatizo hilo serikali itaongeza wafanyakazi pamoja vitendea kazi ambavyo vitawezesha watendaji kufanyakazi zao kwa ufanisi zaidi.
Vilevile itaogneza nguvu kwa kuwshirikisha wananchi ambao wamepatiwa mafunzo ya kiasikari huku wakitambulika kama polisi jamii.
Akizungumzia kuhusu mazishi ya watu 45 waliokufa na wengine 72 kuwa katika hali mbaya baada ya kukosa hewa katika gari walilokuwa wakisafiria kutoka Ethiopia kwenda nchini Malawi, alisema bado mazungumzo yanafanyika kati ya Tanzania na nchi walikotoka.
Nantanga alisema kwa kuwa wale ni raia wakigeni hivyo haiwezekani Tanzania ikaamua kuwazika bila kuwa na mawasiliano na nchi husika kwa lengo la kusikia wanasema nini juu ya hali ya maiti za watu hao.
No comments:
Post a Comment