Wednesday, July 18, 2012

BUNGENI HAPAKALIKI

CHADEMA, CCM walumbana bungeni *Chanzo ni vipengele vya hotuba ya upinzani *Lissu, Lukuvi, Jaji Werema, Wenje wakabana *Vurugu zamtisha Cheyo, aomba liahirishwe

HALI ya hewa ndani ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, jana ilichafuka ambapo Mbunge wa Bariadi, mkoani Simiyu, Bw. John Cheyo, alimuomba Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, kutumia kanuni ya 70 inayompa mamlaka ya kuahirisha Bunge kwa muda kama kunatokea vurugu ndani ya ukumbi huo na kumtaka achukue hatua kwa wahusika.

Bw. Cheyo alilazimika kutumia kanuni hiyo baada ya kutokea malumbano na kutoelewa kati ya Serikali na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Hali hiyo ilijitokeza jana mchana wakati Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Bw. Vincent Nyerere, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wakati akiendelea kuwasilisha maoni hayo, Mnadhimu wa Shughuli za Serikali bungeni, Bw. William Lukuvi, alisimama na kutaka utaratibu kwa Bi. Makinda juu ya vipengele vilivyopo katika hotuba hiyo na kuomba visisomwe kwani vinaingilia uhuru wa mahakama.

Bw. Lukuvi alisema ukurasa wa tatu na wanne wa hotuba hiyo, kuna kipengele kinachosema mauji yenye sura ya kisiasa na na kesi nne ambazo zimetajwa zipo mahakamani na zingine katika uchunguzi.

Kwa msingi huo, Bw. Lukuvi alimuomba Bi. Makinda, kuzuia vipengele hivyo visisomwe ambapo Spika kumtaka ataje vipengele hivyo kwani yeye hakuviona.

Awali Bw. Lukuvi alionekana kutokuwa tayari kutaja vipengele hivyo na kutoa maelezo ya jumla ambapo baada ya kubanwa na Bi. Makindaalisema katika hotuba hiyo kuna suala la wabunge wa CHADEMA, Bw. Highnes Kiwia na Bw. Salvatory Machemli, kuvamiwa akisema suala hilo tayari lipo mahakamani.

Alidai kipengele kingine kinazungumzia suala la Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na kutaka kipengele kinachomuhusu Dkt. Steven Ulimboka, kisisomwe kwani mtuhumiwa wake tayari amefikishwa mahakamani.

Baada ya kutoa kauli hiyo, baadhi ya wabunge walisikika wakisema kwa sauti kubwa; “Kichaaa”, wakimaanisha mtuhimiwa huyo ana matatizo ya akili, hali iliyomfanya Bw. Lukuvi, kuwajibu kuwa haijathibitishwa na mahakama (kuwa na matatizo hayo).

Pia Bw. Lukuvi hakutaka kipengele cha mauaji yaliyotokea Iramba Magharibi, kisomwe bungeni kwani tayari wahusika walikuwa wamefikishwa mahakamani jana (juzi).

Muda wote wakati Mnadhimu huyo akijenga hoja zake, baadhi ya wabunge walikuwa wakizomea kama ishara ya kupinga kile alichokusudia kukisema.

Baada ya Bw. Lukuvi kumaliza kuzungumza, alisimama Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Bw. Tundu Lissu, na  kuomba kutoa taarifa ambapo baada ya kuruhusiwa alianza kujenga hoja za kupinga ushauri wa (Bw. Lukuvi), usikubaliwe.

Alisema kiti cha Bi. Makinda hakikuitendea haki kambi ya upinzani kwa kuzuia kukubali msomaji hotuba (Bw. Nyerere) alitishe na kuanza kusikiliza hoja za Bw. Lukuvi kitendo ambacho hakijawahi kutokea tangu aingie bungeni.

Bw. Lissu alisema hajawahi kuona mtu anasoma hotuba iwe Kamati ya Bunge au Waziri na kukatishwa katikati akiongeza kuwa, Bw. Nyerere, ndiyo kwanza alikuwa anaanza kuzungumza na alikuwa hajafikia vipengele vilivyotajwa.

“Angeachwa amalize vinginevyo itafsiriwe kuwa Bunge haliitendei haki kambi hiyo, katika hotuba yetu hakuna sehemu inayotaja mambo yaliyoko mahakamani, imechukuliwa kwa ujumla wake kuwa jambo liko mahakamani,” alisema Bw. Lissu.

Baada ya kumaliza kutoa hoja zake, alisimama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na kumuomba Spika asikubali vipengele hivyo kusomwa kwa madai kesi zake zipo mahakamani.

Jaji Werema alisoma kanuni ya Bunge ambayo inakataza suala ambalo lipo mahakamani kujadiliwa bungeni ambapo kutokana na malumbano hayo, Bi. Makinda alisimama na kumzuia Bw. Nyerere asisome ukurasa wenye vipengele hivyo kwani kuna maelezo yanayozungumzia masuala yaliyopo mahakamani.

Alisema kanuni 64 inazuia masuala yaliyofikishwa mahakamani hayajadili bungeni hivyo yeyote ambaye atakwenda kinyume na kanuni hiyo, atazuiliwa kuendelea kusema jambo analotaka kuzungumza ndani ya Bunge bila kujali ni mbunge au Waziri.

Aliagiza suala hilo likajadiliwe kwenye Kamati ya Madaraka, Haki na Maadili ya Bunge ili kuona kama vipengele vinavyozungumzwa mashauri yake yapo mahakamani.

Spika alipomaliza kutoa kauli hiyo, alisimama Mbunge wa Nyamagana Bw. Ezekia Wenje (CHADEMA), na kusema kilichokuwa kinazungumzwa si kuingilia uhuru wa mahakama kwani katika hotuba ya kambi hiyo, hakuna kipengele kinachogusa mwenendo wa kesi zinazotajwa.

Alisema juzi mbunge mmoja wa CCM aliituhumu moja kwa moja CHADEMA kuwa inahusika na mauji yaliyotokea Singida ambapo baada ya Bw. Wenje kutoa kauli hiyo, Bw. Cheyo aliomba mwongozo wa Spika na kutumia kanuni ya 70 kutaka Bunge liahirishwe kutokana na kutokea vurugu ndani ya bunge ili ijulikane ni mambo gani yako Mahakamani.

Aliongeza kuwa, wananchi wana imani kubwa na kambi ya upinzania hivyo ikiwa itaonekana ni watu wasio na mwelekeo hadi kuvunja meza za ukumbi huo itakuwa jambo la fedheha kubwa kwa kambi hiyo.

Kauli hiyo iliwafanya wabunge kulipuka kwa vicheko baada ya kuonekana wazi kijembe hicho kinamlenga Bw. Lissu ambaye anadaiwa kuharibu sehemu anapokaa kutokana na stahili yake ya kupiga makofi.

Pia Bw. Lissu alipigwa kijembe kama hicho na Jaji Werema aliyetaka wabunge waangalie wanapokaa.

Wiki iliyopita mbunge mmoja aliomba mwongozo wa Spika akisema ukumbwi huo umejengwa kwa fedha nyingi za wananchi, lakini anapokaa Bw. Lissu kumeharibika kutokana na kupiga makofi kama kwamba anatumia miguu.

Mbunge huyo alisema, Bw. Lissu baada ya kuharibi sehemu anayokaa sasa ameihama hivyo aliomba mwongozo kuhusu suala hilo.

No comments: