Machangu wamekiona cha mtemakuni! Wakati Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ukiwa katika chungu cha nane, akina dada wanaofanya biashara haramu ya kuuza miili maarufu kama Machangudoa au Chipsi Funga au Wauza Sukari Tamu, wamekula viboko laivu baada ya kutuhumiwa kuwatega Waislamu.
Tukio hilo lilijiri katikati ya wiki hii ambapo vijana wa Kiislamu waliodai ni wa kikundi cha Jumuiya ya Uamsho Tanzania Bara walizunguka mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuwashushia fimbo machangu ambao kwa sasa wametapakaa kila kona jijini.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, waumini hao, wakiwa wamevaa kanzu huku wakitembea na bakora mkononi walichukua jukumu la kukodi Bajaj na kuzunguka maeneo mbalimbali jijini inapofanyika biashara hiyo haramu ya ukahaba.
Vijana hao waliolenga kukomesha biashara hiyo hasa kipindi hiki cha mfungo walianzia kwenye Barabara ya Shekilango inayokatiza kwenye viunga vya Sinza, Dar ambapo kila kituo cha daladala kuanzia Afrika Sana hadi kwenye mataa ya Shekilango waliwakuta machangu na kuwatandika viboko kabla ya kutua mitaa ya Mwenge.
KINONDONI
Baada ya kufagiafagia Sinza kwa kuwaadabisha wanawake hao ndipo zoezi likahamia mitaa ya Kinondoni ambapo nao walipokea bakora za kutosha huku wengine wakitoka nduki.
Kwa mujibu wa vijana hao, walifikia hatua ya kufanya zoezi hilo baada ya muumini mmoja wa kiume kukatiza maeneo ya Corner Bar, Afrika Sana na kuvutwa kisha kuchezewa nyeti na makahaba na kusabisha kuharibika kwa swaumu yake.
Ilielezwa kuwa baada ya kukutwa na kimbembe hicho, ilibidi muumini huyo kukatiza safari yake ya kwenda kuswali msikikini mishale ya saa 2:00 usiku.
Waandishi wetu, wakiwa kwenye mishemishe zao za kutafuta habari mishale ya saa 5 usiku waliwashuhudia waumini hao wapatao saba wakishuka kwenye Bajaj nyeusi maeneo ya Sinza wakiwa na bakora mikononi kisha kuwavaa machangu hao na kuwatandika.
Wakati wakitekeleza zoezi hilo, jamaa hao walisikia wakiwaambia: “Sisi tupo kwenye swaumu nyiye mnatutega, ala!”
Waumini hao waliongeza kuwa makahaba hao wamekuwa hawaheshimu mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan ndiyo maana wanaendeleza biashara yao hiyo ya aibu.
No comments:
Post a Comment