Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Imeelezwa kuwa Tanzania kwa sasa haina  raia yeyote  aliyeingia nchini kutoka mataifa mengine aliyebainika kuwa na maabukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Ebola kufuatia zoezi linaloendelea la uchunguzi wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege na maeneo mengine.
Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti na wataalam wa ufuatiliaji wa magonjwa ya binadamu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wanaoshughulikia magonjwa ya milipuko wakati wa mafunzo kuhusu ugonjwa  wa Ebola kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Wamesema kuwa ugonjwa huo licha ya kuleta madhara na maafa makubwa katika maeneo ya nchi za Afrika Magharibi kama zinavyoonyesha taarifa za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) bado haujaingia nchini Tanzania na kuongeza kuwa tayari Serikali kupitia wizara ya Afya imechukua  hatua za udhibiti  kupitia timu ya wataalam wa afya walio katika maeneo mbalimbali nchini.
SONY DSC
Dkt. Chacha Mung’aho ambaye ni Afisa Afya Mkuu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anayeshughulikia maeneo ya Bandari, Viwanja vya ndege na mipakani akizungumzia namna walivyojipanga kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola  kupitia wasafiri wanaoingia nchini Tanzania amesema kuwa  tayari Serikali imetenga maeneo maalum, vifaa vya uchunguzi na huduma kwa wasafiri watakaobainika kuwa na dalili za maambukizi ya ugonjwa huo.
Amesema kuwa wataalam waliopo kutoka Wizara ya Afya wanaendelea  kushirikiana na wenzao wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege, Uhamiaji na Wizara ya Kilimo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuendesha zoezi la uchunguzi wa afya ili kupata taarifa za wasafiri kulingana na mataifa wanayotoka.
“Kwa sasa tunafanya kazi kwa kushirikiana na tunapata taarifa sahihi za abiria kutoka kwa mashirika ya ndege wanayotumia kusafiria jambo linalotusaidia kuwabaini wasafiri waliotoka katika nchi za Liberia, Ivory Coast na Guinea zilizoathiriwa na ugonjwa huo” Amebainisha Dkt. Chacha.
Amesema tangu kugunduliwa kwa ugonjwa huo mwezi Machi mwaka huu huko Afrika Magharibi mataifa  mbalimbali duniani kote yamekuwa katika mapambano kudhibiti ugonjwa huo kuendelea kusambaa na kuleta maafa katika maeneo mengine duniani ambako haujafika.
SONY DSC
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Binadamu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Janeth Mghamba akifungua  wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa ugonjwa wa Ebola jijini Dar es salaam.
Naye Dkt. Vida Mmbaga akitoa ufafanuzi kuhusu historia ya ugonjwa wa Ebola, Virusi vyake , dalili na kuenea kwake amesema kuwa kwa mara ya kwanza uligunduliwa mwaka 1976 nchini Zaire maeneo ya mto Ebola ukihusishwa binadamu kula nyama ya wanyama jamii ya Sokwe, Nyani na Popo.
Amesema kuwa katika nchi za Afrika ya Magharibi ambako sasa ugonjwa huo umeshika kasi chanzo kimetajwa kuwa ni binadamu kula nyama ya wanyama jamii ya Sokwe na Popo huku wengine wakiambukizana kupitia kugusana na mgonjwa, majimaji, kushika damu ya mgonjwa, mate, mavazi au mwili wa mtu aliyekufa kwa Ebola.
Kuhusu kipindi cha mgonjwa kuanza kuonyesha dalili za kuambukizwa ugonjwa huo kinaazia siku ya 2 hadi ya 21 na kufafanua kuwa dalili hizo huambatana na kutokwa na damu zehemu za wazi, maumivu makali ya mwili na kichwa na kuongeza kuwa mgonjwa asipopatiwa tiba ya dalili hizo mapema hupoteza maisha.
SONY DSC
Afisa Afya Mkuu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anayeshughulikia maeneo ya Bandari, Viwanja vya ndege na mipakani Dkt. Chacha Mung’aho  akizungumza namna walivyojipanga kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola  kupitia wasafiri wanaoingia nchini Tanzania.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari juu ya namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari na  endapo watabaini uwepo wa mtu mwenye dalili za Ebola pia kuratibu mipango yote ya vifaa tiba,matibabu na mazishi endapo ugonjwa huo utaingia nchini kupitia kamati ya maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu .
Aidha, amesema licha ya ugonjwa huo kuibuka na kupotea katika vipindi tofauti katika mataifa mengine ya bara la Afrika na nchi jirani  za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda , wataalam hapa nchini wanaendelea kufanya utafiti juu ya chanzo kinachohifadhi Virusi hao kutokana na tabia yao ya kupotea katika kipindi fulani na kuibuka tena.
SONY DSC
Sehemu ya waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo hayo.