Tuesday, April 17, 2012

Ole Millya ahamia Chadema


 MBOWE ASEMA AMEFANYA UAMUZI WA KIJASIRI, MUKAMA, NAPE WAMKEJELI
waandishi wetu
KITENDO cha Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mkoa wa Arusha, James Millya kukihama ghafla chama hicho na kujiunga na Chadema kimekitikisa chama hicho tawala na jana kwa nyakati tofauti, viongozi wake walitoa matamko mbalimbali kumkejeli.

Mara tu baada ya Millya kutangaza kung'atuka CCM kwenye mkutano wake na waandishi wa habari mkoani Arusha, viongozi wa chama hicho, akiwamo Katibu Mkuu, Wilson Mukama, Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigella, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare, walitoa matamko mbalimbali.

Kwa upande wake, Chadema kimefurahia hatua hiyo na jana Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kwamba kinampokea Millya kwa mikono miwili na kinaamini kuwa atakuwa na mchango mkubwa.

Jana, Ole Millya alitangaza kujivua nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho tawala kuanzia ngazi ya taifa na kujiunga na Chadema akidai kuwa CCM kimefilisika kimawazo na hakitoi matumaini kwa Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Arusha jana, Ole Millya alisema amefikia uamuzi huo baada ya kugundua kuwa ‘gari’ alilopanda limepata pancha na haliwezi kumfikisha safari ya ukombozi wa taifa.

“Ukipanda gari halafu likapata pancha ambayo hakuna namna yoyote ya kuiziba na wala hakuna juhudi za kutafutia ufumbuzi tatizo hilo, busara ni kuhamia usafiri mwingine wenye uhakika wa kukufikisha safari yako,” alisema Millya.

Akirejea kauli ya Baba wa Taifa, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Millya alisema CCM siyo mama yake wala baba yake na kwa sababu kimeshindwa kujibu mahitaji na matatizo ya umma, ameamua kukihama.

“Natangaza rasmi kujitoa CCM na kujiunga Chadema kuendeleza harakati za kulikomboa taifa hili kutoka mikononi mwa watu wachache wenye fikra kwamba ndiyo wenye hatimiliki ya nchi hii,” alisema Ole Millya

Alisema amegundua kuwa alikuwa akichezea timu isiyo na uwezo wala nia ya ushindi katika ulingo wa siasa na uongozi wa umma na kujipa moyo kwamba licha ya kuchelewa kugundua kosa hilo, sasa amegundua na anakihama chama hicho kikongwe nchini.

Akiwa na wapambe wake wawili ambao hakuwa tayari kutaja majina yao kwa maelezo kuwa ni watu waliomsindikiza, alitaja mambo kadhaa yaliyomfanya akihame CCM ikiwemo kauli ya UVCCM mkoa wa Pwani waliodai Rais ajaye hawezi kutoka Mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

“Baada ya kauli ile mimi nilitoa tamko kupinga na kulaani kauli hiyo kwa sababu ni kinyume cha katiba. Kanuni na taratibu za CCM lakini tangu kipindi hicho hakuna kiongozi yeyote ndani ya chama aliyejitokeza kukemea jambo hilo,” alisema Ole Millya.

Alisema licha ya kutangaza Rais ajaye kutotoka Kanda ya Kaskazini, vijana hao wa Pwani pia walidai anayemjua Rais wa Awamu ya Tano ni Rais Jakaya Kikwete akisema kitendo cha kiongozi huyo kukaa kimya ni kielelezo kuwa vijana hao walikuwa na baraka zake au za uongozi wa juu wa
CCM.

Ole Millya aliahidi kuwa kundi kubwa la vijana wa CCM wako nyuma yake na wanasubiri muda muafaka kuhamia Chadema.

Mwaka jana, Ole Millya aliingia kwenye mgogoro mkubwa na viongozi wa CCM Mkoa wa Arusha hadi kupewa karipio kali kwa tuhuma za kumtolea maneno machafu Katibu wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda.

Oktoba mwaka jana, Ole Millya pamoja na viongozi kadhaa wa UVCCM akiwemo Makamu Mwenyekiti, Beno Malisa waliingia kwenye mgogoro baada ya kuandaa na kuongoza maandamano makubwa ya vijana kufungua matawi kabla ya kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara eneo la
Karibu na Hospitali ya St Thomas, Arusha.

Baada maandamano na mkutano huo, Ole Millya alihojiwa polisi na jeshi hilo lilisema kwamba licha ya kuvunja sheria, walioshiriki walipewa onyo na kutakiwa kutorudia makosa kama hayo.

Kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita, Ole Millya anayeaminika kuwa mfuasi mtiifu wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa aliingia kwenye mgogoro mkubwa na Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka alipodai kupigwa na kutishiwa kwa bastola.

Alimshtaki Ole Sendeka mahakamani ambaye aliachiwa huru baadaye baada ya kukosekana kwa ushahidi.

Viongozi wa CCM
Viongozi wa CCM walijitokeza kwa nyakati tafauti jana na kumponda huku baadhi wakieleza kuwa hatua yake hiyo, siyo tishio kwa chama chao.
Mukama alisema Millya alikuwa chini ya karipio kali na alikuwa amebakiza hatua moja kufukuzwa akidai kuwa
alikuwa mtovu wa nidhamu na msumbufu.

Alisema anamhurumia kwa kuwa walimpa nafasi ya kujirudi lakini hakufanya hivyo akisema huko aendako haionyeshi kama atafanikiwa.

Kwa upande wake, Shigella alisema Ole-Millya alikuwa ni mzigo ndani ya chama hicho huku akitamba kwamba kuondoka kwake kunakijenga UVCCM badala ya kukibomoa kama wengine wanavyoamini akiwataka wengine ambao ni mzigo kujiondoa kama alivyofanya.

Alisema kuondoka kwake ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Halmashauri Kuu ya CCM la mwaka jana kuwa kila mwanachana anatakiwa kujipima mwenyewe na akibaini kuwa ni mzigo, basi ni vyema akaachia ngazi kwa hiari yake. Alimshukuru Ole Millya kwa kujipima na kubaini kuwa alikuwa ni mzigo na akaamua kuondoka.
Nnauye alituma ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook uliosomeka: “Nampongeza Millya kwa kuamua kukisaidia chama changu, kwani alishakuwa mzigo mkubwa kwa CCM. Itakumbukwa alikuwa afukuzwe kwenye chama kutokana na mambo alokuwa akifanya. Akapewa karipio ili apate muda wa kurekebisha tabia yake! Kaondoka akiwa chini ya karipio. Kajivua gamba, tunampongeza kwa kuitikia wito wa kujivua gamba. Kila la kheri aendako ni kijana bado anayo mengi ya kujifunza!”

Sanare kwa upande wake, alisema kuondoka kwa kada huyo kamwe hakuwezi kuathiri utendaji wa kazi za CCM Arusha na kwamba hakijatikiswa na uamuzi huo wa Ole Millya akisema kina zaidi ya wanachama milioni nne.

Hata hivyo, alisema endapo kiongozi huyo angekuwa na sababu zake zinazomkereketa angeweza kuzifikisha mbele ya chama ili zijadiliwe badala ya kuchukua uamuzi wa kuhama.

Alisema kwamba chama chao kimejipanga kwa mapambano yoyote ukiwemo uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini endapo Mahakama itatupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na Chadema.

Lakini Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole alisema ameshtushwa na taarifa hiyo na kuahidi kutoa tamko leo… “Nimezipata hizi taarifa. Kweli ni mbaya kwetu lakini kesho tutakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumza.”
Chadema wamkaribisha

Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kwamba ya Ole Millya atakuwa na mchango mkubwa na kubeza kauli kwamba alikuwa mzigo akisema ni kauli zinazotolewa sasa baada ya kuamua kujitoa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alisema chama hicho kimefurahi kumpata Ole Millya na kimempokea kwa mikono miwili akiamini kuwa atakisaidia kukiondoa CCM madarakani.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Aman Golugwa alisema wamempokea Ole Millya na tayari, wamemkabidhi kadi ya Chadema… “Ninachoweza kusema ni kwamba amevua magwanda ya CCM na tumemvika kombati za Chadema na kuna wenzake wengi tutawapokea ila bado tunaandaa utaratibu maalumu.”
Alisema Ole Millya ametambua kuwa kamwe hawezi kuwa mtetezi wa haki za vijana akiwa CCM na ndiyo sababu ya kujiunga na chama cha ukombozi na utetezi wa watu wote.
Habari hii imendaliwa na Moses Mashalla, Juma Juma na Peter Saramba, Arusha, Habel Chidawali,Dodoma, Boniface Meena,

No comments: