Apolo Milton Obote
Na Walusanga NdakiRais wa Uganda aliyepinduliwa, Nyerere akampa hifadhi Tanzania
JINA lake kamili ni Apolo Milton Obote, alikuwa Rais wa Uganda tangu uhuru mwaka 1962. Mwaka 1971 alipinduliwa na mwanajeshi wa nchi hiyo, Jenerali Idi Amin wakati Obote akiwa nchini Singapore kwenye mkutano wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Madola).
Baada ya mapinduzi hayo, Obote alikimbilia hapa Tanzania. Wakati huo rais akiwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa rafiki yake kipenzi.
Mwaka 1980, Obote alirudishwa madarakani baada ya majeshi ya Tanzania kuuangusha utawala wa Idi Amini kufuatia vita vilivyopiganwa mwaka 1979. Alirudi madarakani baada ya upigaji kura ambao baadhi ya mataifa duniani yaliuelezea kuwa ni wa ‘kihuni’.
Hata hivyo, la kuvunda halina ubani, baada ya kurudi madarakani mwaka 1980, Obote alipinduliwa tena Julai 27, 1985 na jeshi baada ya utawala wake kuandamwa na mauaji makubwa ya wananchi kama ilivyokuwa wakati wa Idi Amin.
Wanajeshi waliomwangusha, nao waliangushwa miezi michache na Yoweri Museveni ambaye ni rais wa sasa wa Uganda.
Katika kujiweka sawa, akiwa amerudi madarakani, mbali ya kuwa rais pia alijipa nafasi ya uwaziri wa fedha, hivyo, alipong’olewa aliondoka na ‘mshiko wa uhakika’ kukwepa maisha ya ‘ulofa’ aliyoishi wakati alipokimbilia Tanzania mara ya kwanza.
Katika mapinduzi ya pili, Obote alikimbilia nchini Zambia wakati huo rais akiwa Kenneth Kaunda na akajitoa katika siasa hadi alipofariki dunia Oktoba 10, 2005 akitibiwa Afrika Kusini baada ya kuugua figo kutokana na kile kilichosemwa ni ‘pombe na sigara za kutosha’.
Ni Milton Obote, mtu wa kabila la Lango, aliyezaliwa mwaka 1925, mume wa Miria Obote ambaye alimwachia watoto watano.
No comments:
Post a Comment