Wednesday, July 11, 2012

KAMISHNA WA MADINI KUFUNGA MACHIMBO YA MCHANGA KATIKA MAENEO YASIYO RASMI

 
OFISI ya Kamishna Msaidizi wa Madini wa Kanda ya Mashariki kwa kushirikiana na Mkaguzi wa madini nchini (TMAA), imesema Julai 31 mwaka huu itafunga shuguli za uchimbaji holela wa mchanga katika maeneo yasiyokuwa rasmi na leseni.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam leo, na Kamishna Msaidizi huyo, Alex Magayane, kuwa maeneo ambayo yatahusika ni pamoja na mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Alisema wachimbaji wote wa mchanga katika maeneo mbalimbali wanapaswa kufika kwenye ofisi za mikoa hiyo kuomba leseni ndogo zinazoendana na shughuli zao.


“Tunawashauri watemblee ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Mashariki iliyopo katika Jengo la STAMICO, barabara ya Upanga Dar es salaam kuomba leseni”alisema Magayane.


Magayane alisema leseni hizo ndogo zitahusika pia na uchimbaji wa madini (primary Mining Licenc), kwenye maeneo maalum yaliyotengwa kwa shghuli hiyo.


Akitaja maeneo yaliyotengwa na serikali kwa ajili ya kutolewa leseni za kuchimba mchanga, Magayane alibainisha kuwa ni pamoja na Vianzi, Kisemvule, Mwandilatu na Homboza katika wilaya ya Mkuranga.


Maeneo mengine ni Kidimu, Vikawe, Kwa Mfipa, Viziwaziwa, Misugusugu wilayani Kibaha na Buma katika wilaya ya Bagamoyo.


Magayane alisema katika kutekeleza agizo hilo, kuanzia Agosti 1 mwaka huu ofisi hiyo itafanya ukaguzi kabambe kwenye maeneo yote yanayochimbwa mchanga ili kuwabaini wakiukaji wa sheria.


Alitanabisha kuwa zoezi hilo litasimamiwa kwa pamoja na ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Mashariki, Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini, Jeshi la Polisi na Maofisa kutoka Halmashauri za Wilaya husika.

No comments: