WAZIRI wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Haroun Ali Suleiman ambaye hivi karibuni alizushiwa kupitia mitandao ya kijamii kwamba amekuwa anatoa maelekezo kwa wananchi namna ya kutoa maoni yao kwenye Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba mpya, amesema kundi lililozusha taarifa hizo litafahamika hivi karibuni.
Akizungumza mjini Zanzibar jana, Waziri Haroun ambaye awali alikuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali katika Serikali ya Rais Mtaafu, Amani Abeid Karume na kujipatia umaarufu mkubwa alisema uchunguzi unaoendelea kufanyika utasaidia kuwabaini wabaya wake hao.
Kupitia mitandao ya kijamii, Waziri Haroun alizushiwa kwamba aliwaandalia maelezo ya namna ya kutoa maoni yao kwenye Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba kuhusu masuala yanayohusu Muungano lakini alikanusha madai hayo hivi karibuni akizungumza ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Hata hivyo uzushi huo ulipingwa vikali na wadadisi wengi wa masuala ya siasa kutokana na wengi kumtaja Waziri Haroun kuwa kiongozi makini, mpole na msomi anayeheshimu uhurui wa wananchi katika kutoa maoni yao hatua iliyomfanya kujitokeza kugombea nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu uliopita kupitia Chama Cha Mapinduzi.
“Nadhani nitawafahamu tu maana nimeshaanza kupata tetesi tena wengine wanaonichafua ni watu wangu wa jirani wenye ajenda za siri dhidi yangu,” alisema Waziri Haroun.
Hivi karibuni, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alimmwagia sifa Waziri Haroun akisema ni miongoni mwa mawaziri wachache ambao wamefanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo tangu aunde baraza lake la Mawaziri.
Mbali ya kusifiwa na Dk. Shein, Waziri Haroun pia alipewa sifa nyingi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kazi nzuri ya kuwajengea uwezo wa kiuchumi wananchi wa Zanzibar akiwa Waziri wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika.
Akizungumza ndani ya Baraza la Wawakilishi, Waziri Haroun alisema anawaheshimu wananchi wa Zanzibar na anajua wanaifahamu vilivyo historia ya nchi yao na pia wanafahamu fika masuala muhimu yanayohusu Muungano na hivyo wanao upeo mkubwa wa kuwasilisha maoni yao kwa Tume.
No comments:
Post a Comment