MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita amesema kama siyo busara za Rais Jakaya Kikwete kukiongoza chama hicho, tayari kingekuwa kimesambaratika.
Pia, Guninita ameonya kuwapo watu wanaotumia vibaya jina Rais Kikwete katika uchaguzi wa CCM unaoendelea nchini. Akizungumza Dar es Salaam na viongozi wa CCM Kata ya Mbezi Juu mwishoni mwa wiki iliyopita,Guninita alisema kuwapo kwa chama hicho licha ya wengine kudai kuwa kimepoteza mvuto na haiba mbele ya umma, kumetokana na busara za Rais Kikwete.
Guninita alisema tangu Rais Kikwete ashike usukani wa chama hicho, kimepita kwenye mawimbi makali ambayo kama siyo busara zake yalikuwa yanakizamisha.
“Amekuwa (Rais Kikwete) akitumia vikao kumaliza misuguano inayotokea kwa baadhi ya wanachama… tangu ashike usukani wa chama mwaka 2006, CCM imekumbwa na mawimbi mazito lakini busara zake zimeokoa jahazi kuzama,” alisema Guninita.
Kuhusu baadhi ya wanachama wanaopita pita wakitumia vibaya jina la Rais Kikwete, Guninita aliwaonya kuacha mara moja kwa sababu ana uhakika hakuna aliyetumwa zaidi ni kuchafua jina linalo heshimika kwa wananchi.
Alisema hali hiyo imesababisha watu wengine wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kuogopa kujitokeza kuchukua fomu na kuzua malalamiko.
“Ni haki ya kila mwanachama na kila kiongozi kugombea,huyo anayesema ametumwa na JKni mnafiki mpuuzeni,hata kwenye nafasi yangu jitokezeni hiyo ndiyo demokrasia,”alisema Guninita.
Alisema mtu anayetumia jina la viongozi wakubwa licha ya kuwatisha wanachama wenzake, anakiharibu chama na kudhalilisha demokrasia. Pia,aliwataka wanachama wa chama hicho kuchagua viongozi bora wanaopenda kushirikiana na wenzao,ambao watakisaidia chama kushinde chaguzi mbalimbali.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment