Monday, August 20, 2012

Kikwete: Tanzania haitapigana na Malawi .





Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Rais wa Malawi, Joyce Banda mjini Maputo nchini Msumbiji jana, Marais hao walizungumzia namna ya kutafuta suluhu katika mgogoro wa mpaka kati nchi hizo katika ziwa Nyasa kwa njia za kidiplomasia kupititia kamati maalumu iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo. Picha na Ikulu

"Namhakikishia dada yangu (Joyce Banda) na watu wote Malawi kwamba, hatuna nia wala mpango wa kuingia vitani. Hatuna matayarisho ya jeshi wala jeshi alijasogea popote kwa vile hakuna sababu ya kufanya hivyo,” alisema Kikwete na kusisitiza:

"Mimi ndiye amiri Mkuu wa Majeshi ya Tanzania na sijapanga wala kutoa maelekezo ya vita."Kauli hiyo inapingana na iliyowahi kutolewa hivi karibuni na Edward Lowassa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, aliyesema kuwa Tanzania iko tayari kwa vita iwapo Malawi itaendelea kushikilia msimamo wake kuwa eneo hilo ni la Malawi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma hivi karibuni, Lowassa alisema kuwa Tanzania imejiandaa kiakili na kivifaa kuingia vitani na Malawi kama italazimika kufanya hivyo na kwamba kamati yake imeridhishwa na maandalizi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Rais Kikwete, alisema kwa muda mrefu kumekuwa na utata kuhusu suala la mpaka na tayari maofisa wa pande zote mbili wameanza kulizungumzia kwa nia ya kulitatua kwa amani.

Rais Kikwete aliwalaumu wanasiasa kwa kulikuza suala hilo na kuwataka waandishi wa habari kujiepusha na maneno yanayoleta taharuki na chokochoko baina ya nchi hizo mbili.

"Tuviachie vyombo vyetu vya umma vifanye kazi. Hebu tuvipe nafasi na wanasiasa na waandishi wa habari wajiepushe na maneno haya yanayosababisha taharuki na chokochoko, kwani hayana maana yoyote katika kujenga uhusiano wetu,” Kikwete alisisitiza na kuongeza:
“Naomba wanasiasa na waandishi wa habari waiache diplomasia ifanye kazi yake."

Rais Kikwete yuko mjini Maputo, Msumbiji kuhudhuria mkutano wa viongozi wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofunguliwa juzi na ulitarajiwa kumalizika jana jioni.

Kutokana na kauli hiyo, Rais Banda alisema kuwa, amefurahishwa na kufarijika kwa  Rais Kikwete kumhakikishia kuwa hakuna vita.

"Nimefarijika sana, suala hili limetusumbua sana," alisema Rais Banda na kuvishukuru vyombo vya habari vya Malawi kwa kuonyesha uzalendo na ukomavu katika suala hilo.

Kauli ya Lowassa
Katika mkutano wake na wanahabari mjini Dodoma, Lowassa alisema kuwa kamati yake imepewa maelezo na jeshi kwamba wameridhika na kuwa ikibidi kuingia vitani jeshi liko vizuri na limejipanga vizuri kwa uhakika, kiakili na kivifaa.
Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, Lowassa alifanya kikao cha dharura cha faragha kilichohusisha wajumbe wa kamati hiyo na makamanda wa JWTZ waliofika bungeni kutoa taarifa kwa kamati hiyo.
Hata hivyo, katika tamko hilo Lowassa alisema Tanzania inatarajia mgogoro huo utamalizika kwa njia za kidiplomasia kwa sababu Watanzania na Wamalawi ni ndugu wa muda mrefu.
Mwenyekiti huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu kabla ya kujiuzulu, alisema kuwa kama Tanzania itafikishwa mahali itabidi damu ya Watanzania imwagike, nchi iko tayari kulinda mipaka yake kwa nguvu.
Alisema kama itabidi kuingia vitani, itatumia umoja na mshikamano wa Watanzania wa mwaka 1978 wakati wa Vita na Uganda kulinda mipaka ili kulinda heshima ya nchi.
Lowassa alisema kuwa kamati yake inajua madhara ya kiuchumi yaliyotokana na Vita ya Idd Amin na kwamba vita yoyote ikipiganwa, lazima kunakuwa na madhara ya kiuchumi.
Hata hivyo, alisema anaamini mgogoro huo hautafika huko na kusisitiza kuwa, lakini ikibidi JWTZ ni moja kati ya majeshi bora duniani na ni jeshi lililojiandaa vizuri kwa lolote.

Kauli ya Lowassa ilikuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kutoa msimamo bungeni kuhusu mgogoro huo na kwamba ndiyo kauli rasmi ya Serikali.
Kauli ya Membe
Katika msimamo huo, Waziri Membe alizionya kampuni za kigeni za Malawi zilizoingia katika ardhi ya Tanzania eneo la Ziwa Nyasa kutafiti mafuta na gesi akizitaka kusitisha mara moja.
Akiwasilisha makadirio ya wizara yake, Membe alisema upo ushahidi kuwa ndege tano za utafiti za Malawi ziliruka anga la Tanzania na kutua katika Ziwa Nyasa upande wa Tanzania.
Membe alisema pamoja JWTZ kutoruhusu ndege hizo za Malawi kuingia na kutua eneo hilo la Ziwa Nyasa, bado ziliingia na kutua kinyume kabisa cha sheria za kimataifa.
Chimbuko la mgogoro
Mapema mwezi Julai, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Patrick Kabambe alikaririwa na Redio Sauti ya Ujerumani akisema wataendelea na utafutaji mafuta licha ya onyo hilo la Tanzania.
Waziri huyo alisema ziwa hilo linaitwa Malawi na siyo Ziwa Nyasa na kwamba utafutaji wa mafuta na gesi utaendelea na hakuna wa kuwasimamisha. Alihoji, iweje Tanzania ishtuke sasa?

No comments: