Saed  Kubenea - Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi  inayochapisha  gazeti la Mwana Halisi akionesha baadhi ya Magazeti  yaliyolalamikiwa na  Serikali 
WAKATI  Mkurugenzi Mtendaji wa Gazeti la MwanaHalisi, Saed Kubenea akiitaka  Serikali kuondoa amri ya kulifungia gazeti lake, Jukwaa la Wahariri  Tanzania (TEF) limetoa tamko juu ya suala hilo.
Kubenea  aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba  Sheria  ya Magazeti ya  mwaka 1976 ni katili kwa sababu  haishauri Serikali kutoa maelezo ama  kukumweleza mwenye gazeti juu ya nia ya kulifunga. 
Kubenea  alilazimika kuwaeleza waandishi juu ya suala hilo kufuatia kitendo cha  Serikali  kulifungia Gazeti la MwanaHalisi kwa kile ilichodai  kuwa   mwenendo wake wa kuandika habari na makala ni wa kichochezi, uhasama na  uzushi.
Alisema  yeye hakuitwa kujitetea , bali alipata barua kutoka Maelezo iliyokuwa  na  maelekezo ya  kwamba amezuiwa  kutoa gazeti  na kwamba asome kwenye  gazeti la Serikali namba 258 la Julai 27, mwaka huu.  “Sheria hii katili  ya magazeti ingali hai. Haijafutwa. Watawala wanaihitaji. Wanaitumia  kutunyang’anya uhuru wa kufikiri, uhuru wa kutoa maoni na kuwasiliana,  wamefanya hivyo kwa Mwanahalisi. Wametishia kufanya hivyo kwa vyombo  vingine vya habari. Hii ni hatari,”alisema Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Licha  ya kuitaka Serikali kuondoa amri ya kulifungia gazeti lake, Kubenea   pia aliwaomba wasomaji wao na wadau wengine  wa habari kusimama  nao  katika kudai huru na haki ya kutafuta na kusambaza habari kwa sababu  nchi hii ni yetu sote.
Katika  hatua nyingine, Jukwaa  la Wahariri Tanzania (TEF), limelaani kitendo  cha kufungiwa kwa Gazeti la Mwanahalisi, likitoa maelezo kuwa lengo la  Serikali ni kuviziba midomo vyombo vya habari ili visifichue uovu  unaofanywa katika mfumo wa utawala.
Taarifa  ya jukwaa hilo ilisema kuwa,  sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo  Serikali imeitumia kulifungia gazeti hilo,  ni moja ya sheria ambazo  zimekuwa zikilalamikiwa na kuwa mara kadhaa yamekuwapo mapendekezo  kwamba sheria hizo zifutwe.
“Uamuzi  wa kulifungia MwanaHalisi haukubaliki na tunauona kama mwendelezo wa  jitihada za Serikali kukandamiza uhuru wa habari na wanahabari nchini,  lengo likiwa ni kuwaziba midomo wasiseme ukweli kuhusu uovu unaofanyika  katika mfumo wetu wa utawala na jamii kwa ujumla,” ilisema sehemu ya  taaifa ya TEF iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake, Neville Meena.
Ilisema  pia kuwa,  uamuzi huu wa Serikali unaonekana una nia mbaya ndani yake,  kwani adhabu ya kulifungia kwa muda usiojulikana ina tafsiri pana kwani  inawezekana lengo la Serikali ni kulifuta gazeti la MwanaHalisi kijanja.
Naye  wakili wa gazeti hilo, Legemeleza Nshala  alisema  Serikali  ilikiuka  ibara ya 18 kifungu cha 26 (1) na cha (2) na kifungu cha 30 (1) na cha 8  (2) (a)-(e) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.  Alisema  pia kuwa imekiuka Ibara ya 19 ya Agano la Kimataifa  la Haki  za  Binadamu la mwaka 1966 na Ibara ya 6 ya Agano la Fungamano la Afrika  Mashariki pamoja na Ibara ya 8 ya Agano la Haki za Binadamu  na watu la  Afrika la mwaka 1981.
No comments:
Post a Comment