TAMKO LA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
KUHUSU KUFUNGIWA KWA MWANAHALISI 
Chama  Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinalaani uamuzi wa Serikali  inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulifungia kwa muda  usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kwa kutumia mwanya wa sheria mbovu ya  magazeti inayokwenda kinyume na haki za binadamu na utawala bora.
CHADEMA  kinaitaka Serikali kulifungulia gazeti hilo haraka iwekanavyo na  kimewasiliana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA  kuchukua hatua za kibunge kuisimamia Serikali  kurekebisha udhaifu huo  ikiwa inaheshimu uhuru wa habari na inazingatia maslahi ya taifa.
CHADEMA  kinatafsiri hatua hiyo ya Serikali ya kufungia gazeti la MwanaHalisi  kuwa ni sawa na kufungia uhuru wa kusambaza habari, uhuru wa kupokea  habari na uhuru wa kutoa maoni, hivyo tunatoa mwito kwa wananchi na  wadau wote wa habari kuungana pamoja kupinga hatua hiyo, na CHADEMA  kitaeleza hatua za ziada za kuchukuliwa iwapo Serikali haitasikiliza  kauli za wadau wa habari juu ya suala hili.
CHADEMA  kinatambua kuwa uamuzi wa Serikali kufungia gazeti hilo kwa mara  nyingine tena ni kwenda kinyume na haki za binadamu, kinyume na utawala  bora na ni kikwazo kwa demokrasia na maendeleo nchini.
CHADEMA  kinapinga hatua ya Serikali ambayo viongozi na watendaji wake wakiwa  wametajwa kama watuhumiwa katika habari zilizoandikwa na gazeti hilo  imetumia mamlaka haramu ya Waziri mwenye dhamana ya sekta ya habari  kugeuka mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mfungaji huku ikipuuza  taasisi za kusimamia uwajibikaji na haki.
CHADEMA  ilitarajia badala ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi ingewezesha  kufanyika kwa uchunguzi huru kufuatia habari za kiuchunguzi  zilizoandikwa na gazeti hilo juu ya watendaji na watumishi wa Serikali  kuhusishwa na jaribio la mauji ya Dr Ulimboka Steven, kupanga njama za  mauji ya viongozi wa CHADEMA na matukio mengine ambayo yenyewe ndiyo  yenye mwelekeo wa kufanya wananchi wapoteze imani na vyombo vya dola  hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.
CHADEMA  kinalinganisha uamuzi huo wa Serikali uliotangazwa tarehe 30 Julai 2012  na Msajili wa Magazeti chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na  Michezo  kuwa ni sawa  kujichukulia sheria mikononi kwa kuwa Serikali  yenye kuheshimu misingi ya asili ya haki ingezingatia kwamba ikiwa  chombo chochote cha habari kimedaiwa kuvunja sheria ama kukiuka maadili  dhidi ya Serikali, viongozi wake ama watu binafsi mashtaka au malalamiko  yangepelekwa kwa taasisi zinazohusika mathalani Baraza la Habari (MCT)  au mahakama.
CHADEMA  kinafahamu kuwa Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda  usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya  mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i); hata hivyo uamuzi huo ni kinyume cha  misingi ya asili ya utawala wa sheria.
CHADEMA  kinaelewa kwamba zipo sheria nyingine katika nchi yetu ambazo Serikali  ingeweza kuzitumia kushughulikia madai iliyoyatoa kuwa Gazeti la  Mwanahalisi limeandika habari na makala za uchochezi, uhasama na uzushi  kupitia mahakama lakini imeamua kwa makusudi kuendelea kutumia sheria  mbaya isiyokuwa na uhalali wa kihaki (illegitimate).
CHADEMA  kinakumbusha kuwa kwamba Sheria hiyo ni kati ya Sheria zilizotajwa na  Tume ya kukusanya maoni juu ya mfumo wa vyama vingi (Tume ya Nyalali)  kuwa ni sheria mbaya miaka 20 iliyopita kuwa na Sheria mbaya na Serikali  imekuwa ikikwepa kutunga sheria mpya pamoja na wadau wa habari kuandaa  miswada ya sheria ya huduma za vyombo vya habari na uhuru wa taarifa kwa  nyakati mbalimbali.
CHADEMA  kinatoa mwito kwa wananchi na taasisi zote za kitaifa na kimataifa  kufuatilia kwa karibu tukio hili la kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi  na matukio mengine ya hivi karibuni kuhusu asasi za kiraia, makundi  mbalimbali katika jamii ikiwemo madaktari na vyama vya siasa hususan  CHADEMA yenye kuashiria kwamba Serikali inayoongozwa na CCM imeanza  mkakati wa kuficha ukweli na kudhibiti mabadiliko kwa kutumia sheria  kandamizi, vyombo vya dola na njia nyingine haramu.
Hivyo,  ieleweke kwamba hatua hii dhidi ya Gazeti la MwanaHalisi ni mwanzo tu  wa hatua zingine zaidi dhidi ya magazeti mengine na taasisi nyingine  hali ambayo inahitaji wananchi na wadau wote kuunganisha nguvu za pamoja  katika kuchukua hatua za haraka kuinusuru nchi na mwelekeo huo.
Imetolewa tarehe 30 Julai 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

No comments:
Post a Comment