Wednesday, August 1, 2012

MAHAKAMA YA RUFAA YA ICTR KUTOA HUKUMU OKTOBA


 
Arusha, Julai 31, 2012 (FH) – Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) inatarajia kuwa na vikao viwili kabla ya mwisho wa mwaka huu kikiwemo kimoja cha kutoa hukumu, chanzo cha habari cha uhakika kililiambia Shirika la Habari la Hirondelle Jumatatu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kutakuwaapo na hukumu moja katika kesi ya rufaa ya afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Jean Baptiste Gatete, ambaye anapinga adhabu ya kifungo cha maisha aliyopewa na mahakama ya awali Machi 29, 2011 baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na kutekeketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu.
Kutakuwapo pia usikilizaji wa kesi ya rufaa ya mawaziri wawili wa zamani wa Rwanda, Prosper Mugereneza na Justin Mugenzi katika mwezi huohuo. Mawaziri hao wanapinga hukumu na adhabu ya  miaka 30 waliyopewa Septemba 30, 2011 baada ya kutiwa hatiani kwa kula njama za kufanya mauaji ya kimbari na uchochezi.
Mbele ya Mahakama ya Rufaa zipo kesi nane zenye jumla ya watuhumiwa 18 zikisubiri kushughulikiwa na mahakama hiyo. Kesi hizo ni pamoja ile inayojumuisha washitakiwa sita maarufu kwa jina la ‘’Butare’’ akiwemo mwanamke pekee kuwahi kushitakiwa na ICTR ambaye pia alikuwa Waziri, Pauline Nyiramasuhuko.
Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka mpaka sasa upande wa utetezi haujawasilisha rufaa yake kutokana na matatizo ya lugha. Hukumu hiyo yenye jumla ya kurasa 1,548 ilitolewa na mahakama ya awali Juni 24, 2012 kwa lugha ya Kiingereza wakati warufani wote wanajua lugha ya Kifaransa.

 
Kesi nyingine inawahusisha viongozi wawili wa kilichokuwa chama tawala nchini Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari cha MRND, ikiwa ni pamoja na Matthieu Ngirumpatse na Edouard Karemera ambao walihukumiwa vifungo vya maisha jela. Upande wa mashitaka umesema ni Ngirumpatse pekee mpaka sasa ndiye aliyewakwishawasilisha rufaa yake wakati Karemera atafanya hivyo pia kwa siku za usoni.
Kesi nyingine iliyoko mbele ya Mahakama ya Rufaa pia inajulikana kwa jina la Military II, yenye jumla ya maafisa wanne wa zamani wa jeshi la Rwanda. Hao ni pamoja na majenerali wawili, Augustin Bizimungu na Augustin Ndindiliyimana, Meja Francois-Xavier Nzowonemeye na Kapteni Innocent Sagahutu.Wanapinga hukumu iliyotolewa Mei 17, 2011.
Bizimungu alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela wakati Ndindiliyimana alihukumiwa adhabu ya muda aliokwishatumikia tangu atiwe mbaroni Januari 29, 2000. Nao Nzuwonemeye na Sagahatu walihukumiwa vifungo vya miaka 20 jela kila mmoja.Pande zote mbili za mwendesha mashitaka na utetezi zimekata rufaa.
Kesi ambazo zina warufani mmoja mmoja ni pamoja na za Meya wa zamani Gregoire Ndahimana aliyefungwa miaka 15 jela, waziri wa zamani Calixte Nzabonimana, aliyepewa kifungo cha maisha na afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Kapteni Idelphonse Nizeyimana ayelihukumiwa kifungo cha maisha jela.

No comments: