Na Khatimu Naheka
KOCHA Mkuu wa Coastal Union ya Tanga, Juma Mgunda, amekubali kipigo kutoka kwa Yanga lakini amemtaja kiungo Jerry Santo (pichani) kuwa ndiye aliyesababisha wafungwe.
Coastal ilipigwa 2-1 na Yanga kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa juzi, Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumza na Championi Jumatatu baada ya mchezo huo, Mgunda alisema kikosi chake kilicheza vizuri na kufanikiwa kuongoza kwa bao 1-0 kwa muda mrefu, lakini kitendo cha Santo kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 60 kufuatia kuzozana na mwamuzi Hashim Abdallah, kilichangia kikosi chake kupoteza mwelekeo na kutoa mwanya kwa Yanga kushambulia na hatimaye kuibuka na ushindi.
“Timu yangu ilicheza vizuri leo (juzi) na mimi kama kocha nimeridhika na hilo, tumepoteza leo siyo kwamba Coastal mbovu, isipokuwa wenzetu walikuwa vizuri kwa kuwa wameshacheza michezo mingi ya kirafiki, lakini pia wametoka katika mashindano,” alisema Mgunda.
“Lakini pia bila Santo kupewa kadi nyekundu nadhani timu yangu ingeibuka na ushindi, tulifanikiwa kuwabana vizuri wapinzani wetu na muda mrefu wa mchezo tulikuwa tunaongoza lakini tulipopungua ndiyo wakapata nafasi ya kututawala na kupata mabao mawili ya harakaharaka.”
Misimu miwili iliyopita, Santo alikuwa mchezaji wa Simba.
No comments:
Post a Comment