Monday, September 3, 2012

Twite awaelekezea mtutu mashabiki Simba

Beki mpya wa Yanga, Mbuyu Twite.
Na Khatimu Naheka
BEKI mpya wa Yanga, Mbuyu Twite, amewafanyia kitu kibaya mashabiki wa Simba, kufuatia kumzomea alipokuwa akiitumikia timu yake kwa mara ya kwanza nchini, juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Beki huyo raia wa Rwanda, mwenye asili ya DR Congo, alitua nchini mwishoni mwa wiki iliyopita na juzi alicheza mchezo wake huo wa kwanza nchini dhidi ya Coastal Union na kuonyesha kiwango kizuri ambacho kiliisaidia Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Katika mchezo huo, beki huyo alijikuta akizomewa na mashabiki wa Simba kila alipokuwa akigusa mpira. Katika kipindi cha pili, Twite aliwageukia na kuwataka kushangilia zaidi huku akibusu jezi ya Yanga.
Licha ya Twite kuwadhihaki hivyo, mashabiki hao waliendelea kumzomea kwa kumuita mwizi, lakini beki huyo aliwamaliza zaidi mara baada ya Yanga kupata bao la pili la ushindi ambapo aliwaelekeza wenzake kushangilia kwa kuonyesha ishara ya kuwalipua kwa risasi mashabiki hao.
Kitendo hicho kilimfanya ashangiliwe kwa nguvu na mashabiki wa timu yake ya Yanga.
Mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Twite aliliambia Championi Jumatatu kuwa, alilazimika kufanya vitendo hivyo, ili kujibu mashambulizi ya kuzomewa na mashabiki hao huku akiwataka kutulia na kusema hawezi kuchukiwa kwa uamuzi alioufanya.
“Sikufurahishwa na walivyokuwa wakinifanyia pale uwanjani, kipindi cha kwanza niliweza kuvumilia na nilipoona wanazidi kuendelea na mimi, nikaona ngoja niwajibu, waambie watulie nicheze mpira, wakichukia haitasaidia kwa kuwa wao ndiyo waliofanya makosa,” alisema Twite.

No comments: