Tuesday, October 9, 2012

WFP NA VODACOM ZATUMIA TEKNOLOJIA YA SIMU ZA MKONONI KUBADILI DESTURI ZA LISHE TANZANIA

Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Bw.Richard Ragan akiongea na waandishi wa habari (Hawapo pichani) wakati wa utambulisho wa mradi wa majaribio wa uwezeshaji wanawake wajawazito na watoto mkoani Mtwara kupata fedha za kununua chakula chenye lishe. Walengwa watakuwa wakipokea fedha kila mwezi kupitia mtandao wa M-PESA. Kushoto ni Mkuu wa kitengo cha Vodacom Foundation Bw.Yessaya Mwakifulefule.
  Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Bw.Richard Ragan (katikakati)akisisitiza jambo kwa  waandishi wa habari wakati wa utambulisho wa mradi wa majaribio wa uwezeshaji wanawake wajawazito na watoto mkoani Mtwara kupata fedha za kununua chakula chenye lishe. Walengwa watapokea fedha hizo kupitia huduma ya M-pesa. Wengine pichani ni Mkuu wa kitengo cha Vodacom Foundation Bw.Yessaya Mwakifulefule na Ofisa lishe wa WFP Rosemary Mwaisaka.
 Mkuu wa kitengo cha Vodacom Foundation Bw.Yessaya Mwakifulefule (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa WFP nchini Bw.Richard Ragan,wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu ushirikiano wa Vodacom Tanzania na WFP katika mradi wa uwezeshaji wanawake wajawazito  fedha za kununulia chakula chenye lihse mkoni Mtwara.  Feha hizo hutumwa kupitia huduma ya M-pesa.

*****
DAR ES SALAAM - Vodacom Tanzania na Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) leo wametangaza  ushirikiano ambao utahamasisha jamii zisizokuwa na uhakika wa chakula katika Mkoa wa Mtwara kupata elimu  ya afya na  lishe na kwa njia ya kupatiwa msaada wa fedha  kupitia mtandao wa simu za mkononi.

Mradi huu wa majaribio, ambao utazinduliwa Jumanne 9 Oktoba 2012 katika Kata ya Nanguruwe, Mtwara, utakuza desturi chanya za lishe kwa njia ya kutuma fedha kwa  kutumia Vodacom M-Pesa. Mtwara ni miongoni mwa mikoa yenye tatizo sugu la utapiamlo na ukosekanaji wa virutubishi muhimu  kwa muda mrefu.

Mkurugenzi wa WFP Nchini,  bwana Richard Ragan, alisema ushirikiano huo na Vodacom utasaidia kufikisha elimu ya lishe kwa kaaya zilizolengwa zipatazo 2,200 katika sehemu zote za mkoa wa Mtwara  kwa kutoa motisha kwa kina mama kushiriki kwenye mafunzo.

"Teknolojia ya simu za mkononi ya M-Pesa inatoa njia mbadala ya usambazaji wa chakula," alisema Ragan." Kwa kusaidiana na Vodacom Tanzania, WFP inachangia juhudi za kitaifa za kupambana na lishe duni hapa Tanzania."

Akina mama watakaoshiriki watatumiwa kwa M-Pesa  kiasi cha TShs 16,000 (takriban dola za kimarekani 10) kila mwezi , ambazo zitawawezesha kununua chakula kinachojenga afya zaidi na chenye virutubisho zaidi. Fedha  hizi zitatumwa kutegemeana na mahudhurio kwenye kliniki za kuelimisha kuhusu umuhimu wa lishe kwa mtoto "Katika Siku Zake Elfu Moja za Kwanza " za maisha ya mtoto, ikiwa ni pamoja na kumnyonyesha.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkuu wa Vodacom Foundation Bwana Yessaya Mwakifulefule alisema Vodacom Tanzania itaendelea kuisaidia miradi ya Vodacom Mobile for Good, inayoboresha maisha ya vikundi vilivyo hatarini  hapa nchini  kwa kulenga maeneo muhimu ya afya na ustawi wa  jamii.

"Kupitia Vodacom M-Pesa, tutaisaidia WFP kutuma pesa kila mwezi moja kwa moja kwa walengwa stahili.  Hii, pamoja na elimu ya lishe, itawahamasisha akina mama walio wajawazito na wanaolea watoto wachanga na akina mama wenye watoto walio chini ya miaka 2 kununua chakula kinachojenga afya  na
kuifanya milo yao iwe anuwai," alisema Mwakifulefule.

"Vodacom Tanzania ina furaha kuwa sehemu ya mradi huu kabambe; ni lengo la kampuni kuhakikisha teknolojia yake ya simu za mkononi inabadili maisha ya watu katika kila sekta nchini," aliongezea. Mradi utafanyiwa majaribio katika vijiji 27 katika kata za Nanguruwe, Naumbu, Madimba na Nitekela,
zilizoteuliwa kwa kushauriana na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara. Huu ni mradi wa kwanza wa kulipa fedha taslimu ambao WFP iaufanyia majaribio Tanzania,  na utapima jinsi malipo ya pesa taslimu yanavyoweza kufanyika katika miradi ya jamii inayowalenga mama na mwana katika masuala ya, na shughuli za, lishe.

No comments: