Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa jumla ya wagonjwa wapya wa saratani 3,411 wamehudumiwa na Taasisi ya Saratani Ocean Road.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma wakati Waziri huyo akiwasilisha hotuba yake kuhusu Makadrio ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa mwaka 2013/2014 ya sh. 753,856,475,000 ambapo aliomba Bunge lijadili kuidhinisha.
Alisema wagonjwa hao walihudumiwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo wanaume ni 1,159 na wanawake ni 2,252. Hivyo wagonjwa 1,193 walitibiwa kama wagonjwa wa nje na wengine 2,218 walilazwa.
Aliongeza kuwa hospitali hiyo ilihudumia wagonjwa 12,423 wa marudio katika kliniki, mbapo wanaume walikuwa ni 4,352 na wanawake ni 8,080.
Aidha alifafanua kuwa jumla ya wanawake 8,765 walifanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti.
Kati yao, 788 waligundulika na dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi na 23 walikutwa na saratani ya matiti na walianza kupatiwa matibabu. Chanzo: Magreth Kinabo, Maelezo Dodoma
No comments:
Post a Comment