Ndugu zangu,
HAYA ni moja ya maandiko yangu muhimu katika kazi yangu ya uandishi na uelimishaji jamii.
Ni kwa
kutambua ukweli, kuwa nchi yetu imepatwa na shambulizi la kigaidi.
Imetokea Arusha, ingeweza kutokea popote pale katika ardhi ya nchi yetu.
Tunawapa pole wahanga wa tukio hili. Ni msiba wetu sote. Tuwe sasa na
mioyo ya ustahamilivu. Tusikimbile kunyosheana vidole. Tuwaache
tuliowapa dhamana ya kuchunguza waifanye kazi yao. Wajibu wetu wa
kizalendo ni kutoa ushirikiano.
Naam,
kama nchi, tunapitia sasa kwenye kipindi cha majaribu makubwa. Huu ni
wakati wa kuizunguka bendera yetu ya taifa. Ni wakati wa kuonyesha
umoja, uzalendo na mshikamano wetu kama taifa. Umoja, uzalendo na
mshikamano wetu ni silaha muhimu na kubwa kabisa Watanzania tumeendelea
kuimiliki tangu enzi na enzi. Ndio silaha tunayoendelea kuimiliki hadi
sasa. Tuna lazima ya kupambana hadi risasi ya mwisho kuhakikisha adui
hatupokonyi silaha hii.
Ndugu zangu,
Hii ni
Nchi Yetu. Ni nchi yetu sote, Watanzania wa imani zote. Tutambue sasa,
kuwa kwenye safari tunayokwenda kama taifa, mbele yetu kuna mawimbi
makubwa. Kwa pamoja tutavuka, kwa kugawanyika tutazama.
Wahenga
wetu walisema; kamba hukatikia pabovu. Watanzania wa imani tofauti tuna
historia ya kuchanganyika na kuishi kwa amani na upendo. Hatuna hulka ya
kubaguana. Tukianza sasa dhambi ya kubaguana, basi, itaendelea
kututafuna.
Na siku
zote, uzoefu ni mwalimu mzuri . Mathalan, uzoefu unatufundisha, kuwa
kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini, kuuzima moto, ni kazi ngumu
sana.
Ona, moto
ulioanza kwenye nyumba moja ya nyasi kijijini, waweza kusambaa haraka
na hata kuteketeza kijiji kizima. Na tangu utotoni tumetahadharishwa
hatari ya kucheza na moto.
Naam, binadamu usicheze na moto, labda iwe kwenye mazingaombwe.
Na
ningependa hapa tuyakumbuke maneno ya busara na hekima nyingi kutoka kwa
Bi. Joy Mukanyange ( Pichani). Huyu alikuwa Balozi wa zamani wa Rwanda
nchini Tanzania. Mama huyu aliyatamka maneno haya miaka 13 iliyopita,
takribani miezi sita kabla ya kifo cha Baba wa Taifa. Bi. Joy Mukanyange
alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona. Ni kama vile alikuwa
mtabiri, maana, alichokisema mama yule leo ndio tunaanza kukiona. Siku
ile ya Aprili 6, 1999, katika iliyokuwa Kilimanjaro Hotel, Bi Joy
Mukanyanga aliyatamka haya;
"
Naogopa, kwani nimeanza kuona dalili zinazojengeka za mgawanyiko wa
kidini nchini Tanzania na eneo lote la Maziwa Makuu, hali ambayo inaweza
kusababisha maauji ya halaiki kama yale yaliyotokea nchini mwetu mwaka
1994." Alisema Balozi yule wa Rwanda kabla ya kuendelea kutoa ufafanuzi
wa historia ya Rwanda na matukio yaliyosababisha mauaji yale ya
Wanyarwanda ya wao kwa wao. Ndio, Bi Joy Mukanyange alikiona kile
ambacho Watanzania hatukukiona.
Na
tutafanya makosa makubwa, kama hata sasa, tutajifanya kuwa hatukioni
kile ambacho Balozi Joy Mukanyange alikiona . Watanzania tukubali sasa
kuwa tumepatwa na bahati mbaya sana ya baadhi ya Watanzania wenzetu
kuanza kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu. Kuna wanaotaka tuanze
kubaguana kwa misingi ya kidini.
Hili ni
jambo la hatari sana. Ni hulka ya mwanadamu, anapokuwa matatizoni
kumtafuta kondoo wa kafara. Mtu mwingine wa kummyooshea kidole kwa
matatizo yake. Hali duni ya uchumi wa nchi, hali duni za maisha na
umasikini wa watu wetu isiwe chachu ya kuanzisha vurugu za kijamii.
Maana,
taratibu tumeanza kuizoea misamiati ya sisi na wao. Mathalan, sisi
Wakristo na wao Waislamu. Sisi Wachagga na wao Wazaramo. Tunasahau, kuwa
katika nchi yetu hii hakuna Sisi na Wao, kuna SISI tu.Tutakapokumbwa na
maafa ya kitaifa watakaoathirika ni SISI, hakutakuwapo na WAO.
Hatari
kubwa ninayoiona ni tatizo la wengi wetu kuwa na ufahamu mdogo juu ya
dunia tunayoishi sasa, kibaya zaidi, ufahamu mdogo wa historia yetu.
Hivyo basi, kupelekea hali ya kutojitambua kama taifa.
Ndio,
uelewa wa historia ya jamii husika ni jambo muhimu sana. Kiumbe huwezi
kuelewa ya leo, kesho na kesho kutwa kama huelewi ya jana. Kuielewa
historia yako ni kuelewa ulipo na unakokwenda. Historia ni kama maji ya
mto, yakipita hayarudi. Historia ni wakati, ni muda. Kihistoria jana ni
sawa na zamani.
Karne
nyingi zilizopita wahenga wetu walitafsiri muda kama mkusanyiko wa
matukio ya zamani na sasa. Waliamini kuwa yaliyotokea zamani na
yanayotokea sasa ndiyo yenye kusaidia kubashiri yatakayotea kesho,
yataamua mustakabali wetu.
Dalili
tunazoziona sasa za kupandikiza mbegu za chuki kwa misingi ya udini si
dalili njema. Haya yatatupelekea kwenye maafa. Tuliopata bahati ya
kutumia kalamu zetu hatuna budi kuliweka hili hadharani. Ni wajibu wetu
wa kizalendo.
Narudia,
Hii ni Nchi Yetu. Katika ulimwengu tunamoishi kuna mamilioni ya watu
ambao hawana nchi. Wahenga wetu walishiriki katika kuijenga nchi hii,
wametutarajia sisi tuendelee kuijenga na kuilinda heshima na hadhi ya
nchi yetu. Mengine yanayofanyika sasa sio tu yanaitia doa nchi yetu,
bali, yanaiaibisha nchi yetu.
Ndugu zangu,
Hatuna
haja ya kubaguana kwa misingi ya dini, ukabila na rangi. Sisi wote ni
Watanzania. Tuna historia ya kujivunia. Ni historia yetu wenyewe.
Kinyume na baadhi yetu wanavyofikiri au wanavyotutaka tufikiri, historia
yetu haikuanzia enzi za Mwarabu , Mjerumani au Mwingereza. Historia
yetu haikuanzia enzi za TANU wala Afro Shiraz.
Na dini
hizi za kimapokeo zinazotufanya sasa tufarakane zimekuja na kuzikuta
dini zetu za asili, na bado tunazo. Na hakika, Afrika hatugombanii
matambiko. Afrika kila ukoo una tambiko lake, hivyo basi, dini yake.
Kamwe hutasikia Waafrika wanagombania matambiko. Hutasikia Waafrika
wakigombana kwa tofauti za matambiko yao.
Na sisi
ni Waafrika. Hii leo mahala ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na hata
kufanikiwa kuwafanya wachinjane ni kwenye kwenye tofauti zao za imani
hizi za kimapokeo; Uislamu na Ukristo.
Naam; kamba hukatikia pabovu. Tusikubali dini iwe ndiyo penye ubovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania. Nahitimisha.
No comments:
Post a Comment