Tuesday, July 9, 2013

STARS NA UGANDA KIINGILIO BUKU TATU JUMAMOSI

KIINGILIO cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania, Taifa Stars na Uganda, The Cranes itakayochezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.

Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 kiingilio ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.


Taifa Stars

Viingilio vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika itachezeshwa na mwamuzi Thierry Nkurunziza kutoka Burundi. Mechi ya marudiano itachezwa jijini Kampala kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo (Ijumaa) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Barbershop iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi.
TFF inawakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
Wakati huo huo: Taasisi ya Wash United inayojishughulisha na usaji na utunzaji mazingira imeikabidhi fulana 200 na dola 1,000 za Marekani kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati yake na TFF yaliyosainiwa Novemba mwaka jana.
Fulana hizo kwa ajili ya kliniki za kila wikiendi (Jumamosi na Jumapili) zinazoendeshwa na TFF katika vituo 20 nchini kikiwemo cha Karume ikiwa ni sehemu ya mpango wa grassroots unaoshirikisha watoto wa umri kati ya 6 na 17 zimekabidhiwa na Mratibu wa Wash United, Femin Mabachi.
Hafla ya kukabidhi msaada huo imefanyika leo (Julai 9 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF ambapo kwa upande wake ulipokelewa na Ofisa Maendeleo wake Salum Madadi.
Wash United inafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika lake la maendeleo la GIZ, na hapa nchini moja ya eneo wanalotumia katika kampeni hiyo ili kupambana na magonjwa kama kuhara yanayosababishwa na uchafu ikiwemo kutonawa mikono vizuri, hivyo kusababisha vifo kwa Watanzania ni mpira wa miguu.

No comments: