Sunday, November 10, 2013

Prof Msola kuongoza Kamati Teule

peter_b1125.jpg
Spika wa Bunge, Anne Makinda (kulia) akizungumza na Mbunge wa Viti Maalumu, Clara Mwatuka na Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola katika Viwanja vya Bunge, mjini Dodoma jana.PICHA NA EDWIN MJWAHUZI
Spika wa Bunge, Anne Makinda ameunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza migogoro inayowahusisha wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Makinda alitangaza kamati hiyo ya wabunge watano jana, muda mfupi kabla ya Bunge kuahirishwa, hatua ambayo ni utekelezaji wa uamuzi wa Bunge uliofanywa Novemba Mosi, mwaka huu.
Kamati hiyo teule itaongozwwa a na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Profesa Peter Msola (Kilolo-CCM) na wajumbe Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii, Jenista Mhagama (Peramiho-CCM) na Magdalena Sakaya (Viti Maalumu-CUF).(P.T)
Wengine ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM). Makinda alisema uteuzi wake umezingatia uwakilishi wa vyama, uelewa wa tatizo na migogoro iliyopo nchini, uzoefu katika masuala ya kilimo na ufugaji na jinsia.
Kamati hiyo imepewa jukumu la kuchunguza kubaini kasoro zilizopo katika matumizi ya ardhi na hatimaye kupeleka mapendekezo bungeni, ambayo yatapunguza na kuondoa migogoro ya muda mrefu yanayoendelea kati ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Alizitaja hadidu za rejea kuwa ni, kuchambua sera mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi, ili kubainisha kasoro zilizopo na kuchunguza mikakati ya utekelezaji.
"Kufanya mapitio ya taarifa nyingine za kamati na tume zilizoundwa huko nyuma kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji, kuchambua mikakati yote ya Serikali kuhusu migogoro hiyo," alisema.
Nyingine ni kuchambua mikakati ya kulinda vyanzo vya maji, uharibifu wa mazingira, kutoa mapendekezo jinsi ya kuondoa migogoro na kudumisha uhusianao na utengamano kati ya wafugaji na wakulima. Nyingine ni kupendekeza hatua za uwajibikaji zinazopaswa kuchukuliwa ikiwa itabainia kuwapo kasoro za utekelezaji sera zinazotokana na udhaifu wa kiongozi.
"Kama mlivyooana hadidu za rejea na ukubwa wa tatizo lenyewe la migogoro ya ardhi kati ya wafugaji, wakulima, hifadhi, wawekezaji na watumiaji wengine wa ardhi;Ni dhahiri kazi itakuwa kubwa na inayohitaji umakini wa hali ya juu na muda wa kutosha katika kufikia mapendekezo yatakayowakilishwa bungeni," alisema.
Hata hivyo, alisema kamati hiyo inatakiwa kufanya kazi kwa weledi lakini kwa muda mfupi, ikizingatiwa kwamba ikiwa itachelewa kutoa taarifa yake, kunaweza kusababisha tatizo kuendelea kukua na kwamba inatarajiwa taarifa yake itawasilishwa katika Mkutano wa 14 wa Bunge, unaotarajiwa kuanza Desemba 3 mwaka huu.
Chimbuko la Kamati
Kuundwa kwa Kamati Teule ni utekelezaji wa Azimio la Bunge la Novemba 1, 2013, baada ya mjadala kuhusu mambo mawili; Operesheni Tokomeza Ujangili na Migoro baina ya wakulima na wafugaji.
Wachokozi wa hoja hizo walikuwa wabunge wa CCM; Kangi Lugola (Mwibara) na Saidi Nkumba (Sikonge), ambao walikuwa wametoa mapendekezo ya kujadiliwa kwa mambo hayo ambayo walidai kwamba ni ya dharura.
Kutokana na mjadala huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na mawaziri wake wawili; Khamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo David walijikuta katika shinikizo la kutakiwa kuachia ngazi.
Weabunge hao walisema viongozi hao wanatakiwa kufanya hivyo kama hatua ya kuwajibika kutokana na matukio ya vifo na baadhi ya watu kujeruhiwa katika matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na utekelezaji wa oparesheni tokomeza kwa upande mwingine.
Mjadala huo ulitanguliwa na maelezo ya Serikali kuhusu migogoro ya Wafugaji na Wakulima, Hifadhi za Wawekezaji yaliyotolewa na Dk Mathayo pamoja na yake yanayohusu Operesheni Tokomeza Ujangili, yaliyotolewa na Balozi Kagasheki.
Katika kuchangia mjadala huo, Profesa Msola ndiye aliyekuwa wa kwanza kuchangia husu akielekeza shutuma kwa Serikali na baadaye alihitimisha kwa kutoa hoja ya kutaka iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kadhia hiyo.

No comments: