Sunday, April 29, 2012

NCHUNGA AUNGURUMA JANGWANI, AWAPASHA WAZEE, AMTIMUA SEIF MAGARI

MWENYEKITI wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga amejibu mapigo ya Baraza la Wazee la klabu hiyo, waliotaka kuichukua timu kufuatia mgogoro unaoendelea klabuni.
Lakini Nchunga amekataa ombi au taarifa ya kujiuzulu kwa Mjumbe wa Kamati ya Usajili na Kamati ya Mashindano, Abdallah Ahmed Bin Kleb, wakati huo huo akimkubalia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Seif Ahmad Magari kuachia ngazi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari asubuhi ya leo, makao makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Wakili Nchunga alisema kwamba Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha jana imekubali kujiuzulu kwa Seif, lakini imekataa kwa Bin Kleb.
Aidha, kuhusu Wazee kuchukua timu, Nchunga alisema kweli alifanya nao kikao ana akawaambia atakuwa tayari kuwaachia timu waihudumie kwa mujibu wa Katiba, lakini kwanza lazima watoe vielelezo juu ya vyanzo vyao fedha ili ajue uhalali wake, wasije wakaiingiza klabu kwenye matatizo.
Alisema anahofia wasije wakawa wanapata fedha kutoka kwa watu wenye kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya- wakaiingiza Yanga kwenye matatizo.
Nchunga alisema iwapo watamuhakikishia vyanzo halali vya mapato, kwa mujibu wa Katiba atawaachia jukumu la kuihudumia timu na si kuhodhi madaraka ya uongozi.
Kwa kuwa Wazee walitaka kuanzia kazi kwenye mechi dhidi ya Simba Mei 5, mwaka huu, maana yake wao watahudumia timu, lakini mapato ya mechi watachukua akina Nchunga.
Baada ya kuifunga JKT Oljoro 4-1 wiki hii, wachezaji wa Yanga walipewa mapumziko na jana walikusanyika tayari kuanza mazoezi, ingawa walikwama kwa sababu ya mvua.
Mwenyekiti wa Yanga, Nchunga amesema timu sasa itaingia kambini kesho na kuanza mazoezi moja kwa moja chini ya makocha Fred Felix Minziro na Salvatory Edward, wakati huo akisikilizia Wazee kama watatekeleza masharti yake awakabidhi timu.

No comments: