Gari lililopata ajali, la Mbunge wa Rombo (CHADEMA) Joseph Selasin
Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya gari la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), iliyotokea jana eneo la Boma Ng'ombe, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro jana jioni, imeongezeka na kufikia wanne.
Jana watu watatu walifariki papo hapo ajalini, huku watatu wakiwahishwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambapo mmoja wao, aliyekuwa mahututi amefariki leo.
Waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ni pamoja na Mama Mzazi wa Mbunge huyo, Catherine Joseph Selasini (80), Agatha Jerome Mahoo (85) mkazi wa Rombo ambaye ni mkulima pamoja na wanawake wawili ambao hawajatambulika majina yao mmoja akikadiriwa kuwa na umri wa miaka 70 - 75 na mwingine 35 - 40.
Majeruhi kwenye ajali hiyo ni pamoja na Mkewe Mbunge, Digna Kavishe (43)ambaye amepata majeraha sehemu za kichwa na hali yake siyo nzuri, pamoja na Mbunge mwenyewe, Joseph Selasini ambaye amepata majeraha kwenye bega pamoja na mkono wa kulia na hali yake inaelezwa kuwa inaendelea vizuri.
Chanzo cha ajali hiyo kimetajwa kuwa ni mwendokasi pamoja na kupasuka kwa gurudumu la mbele baada ya gari hilo kuingiliwa na pikipiki mbele na kukosa mwelekeo.
Miili ya Marehemu imehifadhiwa kwenye hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa ajili ya taratibu za mazishini.
No comments:
Post a Comment