WAKAZI wa Kata ya Kiluvya B Kisarawe Mkoani Pwani, wamemtuhumu Diwani wa Kata hiyo Azamen Massawe, kwa tuhuma za kujipa tenda ya ujenzi ofisi ya kata kinyume cha taratibu za tenda kinavyotakiwa.
Wakizungumza na na Fullshangweblog kwa nyakati tofauti jana wakazi hao walidai kuwa, wanashangazwa na hatua ya diwani huyo ya kujibebesha tenda kimya kimya bila kuitangaza kwa wazabuni wengine jambo ambalo halikubaliki.
Walisema kuwa ujenzi wa ofisi hiyo, mbali na kufanyika kimya kimya lakini wanautilia
shaka kutokana na utaratibu mbovu wa manunuzi ya vifaa vya ujenzi uliotumika kwani haukufuata sheria.
Walifafanua kuwa ujenzi huo uligharimu shil. milioni 24 ambapo wakazi hao wanapinga, kutokana na nguvu kubwa ya ujenzi huo imetokana na wananchi wenyewe.
Wakazi hao waliongeza kuwa licha ya ubadhilifu uliofanywa diwani huyo,bado vifaa vingi vilivyotumika katika ujenzi huo vimetoka katika duka lake la vifaa vya ujenzi.
“Awali alituuzia matofali ambapo kila moja liligharimu shil. 2500 huku akidai kuwa ofisi hiyo imetumia nondo 162 jambo ambalo si kweli, kwa sababu mosi ofisi hiyo tumeijenga sisi wenyewe kuanzia msingi” walisema kwa jazba wakazi hao.
Naye diwani wa kata hiyo Massawe, alipotakiwa kutoa ufafanuazi juu ya sakata hilo alisema hivi “ cha msingi mimi ni mfanyabiashara hivyo sikuona vibaya kuchukua tenda hiyo, na gari langu ndilo lililotumika kupeleka vifaa vya ujenzi katika ofisi hiyo bure bila malipo.
Vile vile alidai kuwa kamati ya ofisi iliyoratibu shughuli zote za ujenzi ndio inayoweza kuzungumzia suala hilo kwa kina kwa sababu ilihusika moja kwa moja katika mchakato mzima wa ununuzi wa vifaa.
No comments:
Post a Comment