Saturday, July 14, 2012

MADAKTARI KUANDAMANA JULAI 16 SAA NNE

CHAMA Cha Madaktari nchini (MAT), kimesema maandamano yao yako pale pale na tayafanyika Jumatatu ya Julai 16, saa nne, na si vinginevyo.
 
Aidha, MAT, kimelaani kutekwa na kupigwa kwa mwenzao Dk. Steven Ulimboka na kufutiwa leseni kwa wanafunzi wa vitendo (interns).
 
Uamuzi huo wa MAT, ulitolewa jijini Dar es Salaam, katika kikao cha dharula cha madaktari 500 walioketi katika ukumbi kituo cha Utamaduni wa Korea.
 
MAT, kupitia Katibu wake, Rodrick Kabangila alisema “Kwa pamoja tulilaani  vitendo vya unyanyaswaji wa serikali dhidi yetu, kwanza uamuzi wa  Baraza la Madaktari (MCT), wa kuwafutia leseni wanafunzi wa vitendo bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kutoa maelezo yao.
 
“MCT lilishindwa kuwaita na kupata maelezo yao badala yake walijichukulia hatua za haraka za kuwafukuza, wakati suala hilo lipo mahakamani”alisema
 
Kwa mujibu wa Kabangila, madaktari wanalaani hatua ya kunyimwa chakula na kufukuzwa na FFU kwenye vyumba vya kulala (hosteli), madaktari kabla ya taarifa ya maandishi kutoka Wizarani.
 
Pia, wanafunzi hao na wengine walinyimwa posho kabla ya barua ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
 
Hivyo, vitendo hivyo na vingine vinaonyesha udhalilishwaji mkubwa kwao, ikizingatiwa kuwa ni wanataaluma wanaohitajika ndani ya nchi.
 
Katika maelezo yake, taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa, na ikiwa unyanyasaji huo utaendelea, kutasababisha idadi kubwa ya madaktari kuondoka nje ya nchi.
 
Alionya kwamba endapo wataondoka taifa litakosa madaktari na kutafanya Wananchi zaidi ya milioni 12 kukosa huduma ya afya.
 
Mbali na hilo, Katibu huyo alisema, bado milango iko wazi kukutana na serikali ili kukaa mezani kwa lengo la kumaliza mgogoro wao ambao umedumu kwa muda mrefu sasa.
 
Kimsingi, Kabangila alisema kutokana na hatua hizo, wameandaa maandamano pindi watakapopata kibali kutoka vyombo vya usalama.
 
Hata hivyo, alisema maandamano ni haki yao na kibali ni kwa ajili ya ulinzi wao.
 
Alifafanua kwamba, maandamano yana lengo la kupinga dhuluma na uonevu dhidi ya taaluma muhimu ya udaktari na madaktari wenyewe.
 
Alisema, MAT inasikitishwa na dhuluma hiyo kwa kuzingatia uwiano duni wa madaktari hapa nchini ambapo daktari mmoja hutibu wagonjwa 30,000 kwa mwaka chini ya viwango vya kimataifa.
 
“Tutafanya maandamano ya amani, madaktari wote na wadau wa sekta hii wenye mapenzi mema tunawaomba washiriki… madaktari tutavaa makoti yetu meupe na watakaoshiriki nasi wavae vitambaa vyeupe.
 
Maandamano yataanzia nje ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, tutaishia kwenye geti la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, tukiwa na mabango ya kulaani kitendo cha kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande alichofanyiwa Dk. Steven Ulimboka,” alisema.
 
Dk. Kabangila alisema kuwa wataishinikiza serikali iunde tume huru kwa ajili ya kuchunguza suala la Dk. Ulimboka itakayofanya kazi haraka na wahusika wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

No comments: