YAFUATIA YA NYERERE,MKAPA NA MWINYI, ZITTO ASEMA WAJISALIMISHE
RIPOTI ya utafiti wa utoroshaji wa fedha nchini kwenda kufichwa katika benki za nchi za nje ikiwamo Uswisi uliofanywa na na Shirika la Global Financial Integrity umeonyesha kuwa fedha nyingi kutoka Tanzania zilitoroshwa kati kipindi cha utawala wa awamu ya nne kati 2005 na 2009. Kwa mujibu wa ripoti hiyo kuhusu utoroshwaji wa fedha kwa njia haramu kutoka Afrika kwenda mataifa yaliyoendelea, ambayo gazeti hili limeipata, katika kipindi hicho fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola za Marekani 7,967.4 milioni (sawa Sh12.7 trilioni).
Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa katika kipindi cha utawala wa kwanza ulioishia 1985, fedha zilizofichwa nje zilikuwa Dola 3,493.3 milioni (Sh5.5 trilioni) na katika awamu ya tatu kati ya 1995 hadi 2005, zilikuwa Dola 2,108.8 milioni (Sh3.3 trilioni) wakati katika awamu ya pili zilitoroshwa Dola 529.1 milioni (Sh846 bilioni).Utafiti huo wa Shirika Global Financial Integrity unaonyesha pia nchi 20 za Afrika zinaongoza kwa kuficha fedha nje ya nchi, Nigeria ikiongoza.
Jumla ya Dola za Marekani 1.8 trilioni zimefichwa katika benki mbalimbali nje ya nchi kutoka katika nchi za Kiafrika katika kipindi cha mwaka 1970 hadi 2009.
Mpina
Akizungumzia ripoti hiyo jana, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina alishauri mambo mawili muhimu yafanyike ili kukabiliana na ufisadi wa kutorosha fedha na raslimali za nchi kwenda nje ya nchi.Alisema kuwa hatua ya kwanza ni kufanya marekebisho ya sheria za nchi na pili ni kujenga mfumo madhubuti wa kukabiliana na mafisadi nchini. Kuhusu marekebisho ya sheria, Mpina aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa baadhi ya viongozi wasio na uchungu na nchi wamekuwa wakitorosha kirahisi fedha na rasilimali za nchi kutokana na udhaifu wa sheria. “Ni lazima kwanza sheria zetu ziwe na nguvu ya kuweza kulinda fedha na rasilimali za nchi,” alisema mbunge huyo ambaye hivi karibuni alionyesha kukerwa na tabia hiyo aliyosema inazidi kuwadidimiza Watanzania kwenye wimbi la umaskini. Akizungumzia hatua za kuchukuliwa dhidi ya wahusika, Mpina alielezea kusikitishwa kwake na woga walionao baadhi ya viongozi kwa kuogopa kuwataja hadharani mafisadi. “Mfano suala la Rada… limekuwa ni tatizo na hakuna nia ya dhati ya kukabiliana na wahusika,” alilalamika.
Zitto: Tutawataja wahusika
Akizungumzia suala hilo jana, Zitto alisema kuwa walioficha fedha nje ya nchi wanapaswa kujisalimisha wenyewe kwa kuwa Serikali inaweza kupata orodha yao kutoka mamlaka ya Uswisi. Alisema kuwa amekuwa akishauriana na mmoja wa wabunge wa zamani wa Afrika Kusini ambaye ndiye aliyefanya naye utafiti kuhusu fedha hizo za kifisadi zilizofichwa Uswisi. “Tutawataja mmoja baada ya mwingine maana taarifa zetu ni za uhakika na hazina mashaka,” alisema Zitto. Alisema fedha hizo zimetokana na rushwa kwenye mikataba ya kutafuta mafuta, gesi na Kampuni ya Meremeta.
Kashfa ya kuwapo kwa vigogo walioficha fedha zao nchini Uswisi iliibuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini mwezi Juni mwaka huu na baadaye mwangwi wake kulitikisa Bunge katika mkutano wake wa nane uliomalizika Alhamisi ya Agosti 16 mjini Dodoma. Habari hizo zilikuwa zikinukuu taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Uswisi kuonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni, zilizotoroshwa na Watanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Jumatano wiki hii, tuhuma hizo ziliibuka tena bungeni pale Kambi ya Upinzani ilipodai kwamba inawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja ikiwa Serikali haitawataja.
Naibu Kiongozi wa Upinzani bungeni, Zitto alipokuwa akiwasilisha hotuba ya kambi yake kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha na Uchumi alisema kuwa miongoni mwa wanaomiliki fedha hizo ni kiongozi wa juu nchini, pamoja na aliyepata kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne ambapo anayefuatia anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine dola 20 milioni (Sh32 bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki dola milioni 10 (Sh16 bilioni).
Kwa kuangalia fedha hizo ni dhahiri kwamba vigogo watano tu kati ya kundi la Watanzania 27, wanamiliki dola milioni 126 (Sh201.6 bilioni) sawa na asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati wengine 22 waliobaki wanamiliki dola milioni 60 (Sh96 bilioni) sawa na asilimia 32.25. Kwa hesabu za kawaida, kiasi cha Sh300 bilioni, kinaweza kugharimia ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 33,300, ikiwa chumba kimoja kinagharimu kiasi cha Sh9 milioni. Katika orodha ya walioweka fedha nchini humo, pia wamo wafanyabiashara wanaomiliki kiasi cha dola kati ya milioni mbili na milioni saba.
Wamo wawili waliowahi kuwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere ambao akaunti zao zina kiasi kisichozidi dola 500,000 kwa kila mmoja.
CHANZO: Nhttp://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment