Monday, August 27, 2012

SENSA YA WATU NA MAKAZI YAENDELEA VIZURI NCHI KOTE

Wengi wajitokeza Sensa ya Watu na Makazi  Send to a friend

Waandishi Wetu
SENSA ya Watu na Makazi imeanza jana nchi nzima, huku kukiripotiwa matukio kadhaa ambayo yamesababisha baadhi ya watu kushindwa kuhesabiwa ikiwamo ukosefu wa vifaa katika baadhi ya mikoa, makarani kukosa ushirikiano kutoka kwa mabalozi ambao wamegoma kwa madai ya kuwa hawakushirikishwa tangu awali.
Habari kutoka sehemu mbalimbali nchini zinaeleza kuwa baadhi ya wananchi waligoma kuhesabiwa na kutokana na matukio hayo, watu wanne wanashikiliwa na polisi Dar es Salaam kwa madai ya kusambaza vipeperushi kuzuia watu wagome kuhesabiwa.

Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadick alimweleza Rais Jakaya Kikwete jana kuwa waliwakamata watu wanne wakiwatuhumu kusambaza vipeperushi vya kuzuia watu wasihesabiwe. Alisema mmoja wao ni mwanafunzi wa chuo kikuu.
“Katika eneo la Mbagala, Mbande kulikuwa na msikiti mmoja ambao baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu walikuwa wamejifungia ili wasihesabiwe. Nimewaagiza polisi wawaache ili tuone mwisho wao, naamini nao watatoka tu na watahesabiwa. Hili zoezi ni la wiki nzima sasa kama wako tayari kukaa wiki basi ngoja tuone mwisho wao,” alisema.
Katika eneo la Buguruni makarani na wasimamizi wa Sensa waliopangwa eneo la hilo walijikuta katika wakati mgumu kutekeleza majukumu yao kutokana na baadhi ya familia kukataa kuhesabiwa.
Msimamizi wa Mtaa wa Madenge, Grace Chibaite alisema wakazi wa nyumba zaidi ya tatu katika mtaa huo wamekataa kutoa ushirikiano kwa waandikishaji, jambo ambalo limeripotiwa polisi kwa ajili ya hatua zaidi.
“Karani katoa taarifa ofisi ya serikali ya mtaa ambao wametoa ripoti polisi. Wao ndiyo watajua wanafanya nini,” alisema.

Baadhi ya watu waliolala usiku wa kuamkia jana katika nyumba za kulala wageni katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam hawakuhesabiwa kutokana na makarani wa Sensa kuchelewa kufika.
Baadhi ya wafanya kazi wa nyumba hizo, walidai kupewa majukumu na makarani wa Sensa kukusanya taarifa za watu waliolala katika nyumba zao, kazi ambayo walishindwa kuifanya.
Meneja wa Hoteli ya Rombo Green View ya Ubungo, Diana Kisamo alisema alipewa makaratasi ya Sensa na makarani ili awape wateja wajaze.
Alisema baadhi ya wateja walikubali na kujaza karatasi hizo, lakini wengine walikataa wakidai si sahihi yeye kuwapa karatasi hizo.

Pwani
Mratibu wa Sensa Mkoa wa Pwani, Philemon Mwenda alisema, kazi hiyo iliyoanza usiku wa kuamkia jana, ilikwenda vyema licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa ikiwamo baadhi ya makarani wa Rufiji kutishia kugomea kuhesabu watu siku ya kwanza kutokana na kuchelewa kupewa posho zao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu alisema kumekuwapo vitisho vya chinichini vya kutoshiriki, lakini hadi saa 7:00 mchana hakuna vurugu yoyote iliyoripotiwa.

Mbeya
Katika Mkoa wa Mbeya, baadhi ya makarani wamelalamikia ukosefu wa vitendea kazi hususan sare, vitambulisho na mabegi hali iliyosababisha wafanye kazi katika mazingira magumu.
Pia wamelalamika kwamba wananchi wengi walikuwa wamekosa mwamko, hivyo kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha kuhusu kuhesabiwa na umuhimu wake.
Hali hiyo imejitokeza katika baadhi ya maeneo hususan Kata ya Mbalizi Road, Mtaa wa Kabisa na kusababisha baadhi ya wananchi kuondoka katika makazi kwa madai kuwa wanakwepa usumbufu, kwani hawatambui umuhimu wa Sensa.
Karani wa Sensa Kata ya Mbalizi Road, Salome Faustine alisema mwamko mdogo wa jamii unachangiwa na kutotolewa kwa elimu ya Sensa, ambayo ingetolewa kupitia mikutano ya hadhara ingeweza kusaidia kurahisisha kazi hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Norman Sigalla alikiri kuwapo kwa ukosefu wa vitendea kazi na kwamba hilo ni tatizo la kitaifa na litafanyiwa marekebisho na kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kazi hiyo inafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amewataka wananchi kuendelea kuhesabiwa na wasisitishe shughuli zao kwani kazi hiyo ni ya siku saba na kwamba watahesabiwa na kuwataka makarani kuweka alama kwenye nyumba zilizohesabiwa.
“Wananchi endeleeni na shughuli zenu mtahesabiwa kwani makarani watapita kwa wakati mwingine na ndiyo maana Serikali imeona zoezi hilo litaendelea kwa muda wa siku saba,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani amesema kazi hiyo inaendelea vizuri na hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kwa uvunjifu wa amani na kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu ili wahesabiwe.

Mwanza
Mkoani Mwanza kumeripotiwa na kasoro kadhaa, baada ya Ofisi ya Takwimu ya Mkoa kupokea vifaa pungufu kutoka Makao Makuu ya Sensa.

Mratibu wa Sensa Mwanza, Deogratius Masanja alisema baadhi ya vifaa vilivyopungua ni vibao vya kuandikia na kwamba baadhi ya maboksi ya vifaa waliyokuwa wakiyafungua walikuta yakiwa na vifaa pungufu.

Singida
Kazi ya kuhesabu watu jana ilianza mkoani Singida kwa kusuasua, baada ya wananchi wachache waliogoma kuhesabiwa hadi walipopewa elimu ya umuhimu kuhesabiwa na kisha kutoa ushirikiano.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Queen Mlozi alisema, kazi inakwenda kama ilivyopangwa na kwamba vifaa vipo vya kutosha isipokuwa fulana, kofia na mavazi ya usiku.

Tanga
Mratibu wa Sensa Jiji la Tanga, Sabas Kasambala
Alisema, kulikuwa na tatizo la sare hasa fulana, ‘reflectors’ na kofia na kwamba zilitarajiwa kuwasili jana zikitokea Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa alisema jitihada zinafanyika kuhakikisha makarani wanapewa vifaa hivyo mara vitakapowasili.
“Hiyo ni dosari ambayo inafanyiwa kazi. Nimeshazungumza na mratibu wa mkoa, zitawasili wakati wowote kuanzia sasa,” alisema Gallawa.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Hafsa Mtasiwa amewaonya watakaojaribu kuvuruga Sensa akisema, watachukuliwa hatua.
Aliwataka wananchi kuwapuuza wale wanaotumia mwamvuli ya dini kuwapotosha ili wasishiriki Sensa.

Dodoma
Mkoani Dodoma kazi hiyo ilifanyika kwa utulivu mkubwa.
Mkuu wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi alisema hapakuwa na upungufu wowote wa vifaa na kazi hiyo ilifanyika bila matatizo.
Mratibu wa Sensa wa Mkoa wa Dodoma, Idd Miruke alisema katika maeneo waliyopita usiku wa kuamkia jana, kazi ilifanyika kwa utulivu na walipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wahusika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen alisema hadi jana hakuna tukio lolote lililokuwa limeripotiwa kutishia kazi hiyo.

Mara
Katika Wilaya ya Serengeti, Mara kulikuwa na ukosefu wa vitambulisho, kofia, fulana kwa makarani na malalamiko ya posho ndogo kwa wenyeviti wa vitongoji na vijiji.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Clement Rujaji alisema wanaendelea kurekebisha dosari hizo ambazo alisema zimechangiwa na makao makuu kutokusambaza vifaa kwa wakati.

Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo jana aliongoza kazi ya kuhesabu watu kwa kuzunguka mitaani kuanzia saa 6:01 usiku. Alizungumza na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuwahimiza kushiriki kuhesabiwa.
Akiwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Arusha, Magreth Martin aliwaambia watoto aliowakuta wamelala kwenye mitaa mbalimbali kuwa takwimu zao zitaiwezesha Serikali kuweka mipango ya kuwasaidia.

JK, Pinda wahesabiwa
Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana walihesabiwa na kutoa matamko kuhusu Sensa.
“Nimepata taarifa za kuwapo wenzetu wachache wanaosambaza ujumbe kuwazuia watu kushiriki zoezi hili na wengine kusambaza vipeperushi, nawasihi waache mara moja kwa kuwa zoezi linaendeshwa kwa mujibu wa sheria na si la hiari,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumza kwenye makazi yake, Ikulu jana Rais alisema:
“Napenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa zoezi hili ni muhimu sana kwa ajili kupanga maendeleo ya nchi yetu. Ili tupige hatua katika maendeleo, lazima tujulikane idadi yetu.”
Pinda akiwa kijijini kwake Kibaoni, Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi alisema posho kwa ajili ya wenyeviti wa vitongoji na vijiji ambao wataambatana na makarani wa Sensa zipo palepale na kwamba hawana haja ya kuhofu juu ya malipo yao.
Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sensa aliwasihi wenyeviti hao kuendelea na kazi yao bila wasiwasi wowote... “Ni kweli malipo yao yamechelewa. Ni suala la wikiendi tu kuingilia hapa kati, lakini napenda niwahakikishie kwamba stahili zao zipo, wao wachape kazi tu.”
Alisema mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi ilianza tangu mwaka 2004 na kwamba umeligharimu taifa fedha nyingi akisema mpaka sasa zaidi ya Sh140 bilioni zimeshatumika.

Kamishna wa Sensa
Kamishna wa Sensa, Hajjat Amina Mrisho alimweleza Rais Kikwete kuwa kazi ya kuhesabu watu ilianzia kwenye maeneo maalumu ambayo ni Vituo vya Mabasi vya Ubungo, Kariakoo maeneo yanavyotumiwa na watu wasio na makazi maalumu.
“Taarifa nilizo nazo ni kwamba zoezi linaendelea vizuri katika maeneo mbalimbali ya nchi, licha kuwa na watu wachache kuendelea kutuma ujumbe wa simu kutaka watu wasishiriki,” alisema.

Imeandikwa na Fidelis Felix, Joseph Zablon, Godfrey Nyang’oro na Aidan Mhando, Dar; Julieth Ngarabali, Pwani; Hawa Mathias, Mbeya; Gasper Andrew, Singida; John Semnkande, Pangani; Israel Mgussi na Habel Chidawali, Dodoma; Burhani Yakub, Tanga; Peter Saramba, Arusha

No comments: