Wednesday, December 12, 2012

Maoni Ya Katiba Yageuka Ngumi Za Bure!

Na Hassan Ali, Zanzibar
VURUGU kubwa za kurushiana ngumi zimetokea na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa katika zoezi la ukusanyaji maoni ya Katiba mpya katika majimbo ya Magomeni na Mpendae mjini Zanzibar.
Kwa mujibu wa Kamishina wa tume ya kukusanya maoni, Profesa Mwasiga Baregu, vurugu za kwanza zilitokea juzi katika viwanja vya Mzalendo Magomeni na zingine katika Uwanja wa Mpendae katika wilaya ya mjini Zanzibar.
Alisema chimbuko la vurugu hizo ni watu wanaokwenda kutoa maoni wakiwa wamepakiwa katika magari kushutumiwa kwamba ni mamluki kwani sio wakaazi halali wa maeneo hayo.
Alisema vurugu hizo zilitokea majira ya saa 8 mchana na kusababisha tume kusitisha kazi ya kukusanya maoni kwa sababu za kiusalama.
Alisema wananchi katika maeneo hayo, walianza kulalamika kuwa uwanja wa kutoa maoni umevamiwa na mamluki ambao sio wakaazi halali wa majimbo ya Magomeni na Mpendae mkoa wa mjini Magharibi, Unguja.
“Kazi ya kukusanya maoni imekwama mara mbili baada ya kujitokeza vurugu katika vituo vya kutolea maoni Zanzibar,”alisema Profesa Baregu.
Hata hivyo alisema Tume itaendelea na ratiba yake kama kawaida katika maeneo mengine na kuwataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yao.
Alisema tangu tume yake ianze kukusanya maoni katika wilaya ya Mjini, kumejitokeza ushindani mkubwa kati ya watu wanaotaka mfumo wa Serikali ya Muungano wa mkataba na wale wanaotaka mfumo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili kuendelea kutumika katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema ushindani huo umesababisha baadhi ya watu kujitokeza kutoa maoni zaidi ya mara moja kitendo ambacho ni kinyume na sheria ya tume ya mabadiliko ya Katiba ya Muungano ya mwaka 2012.
“Wananchi wamekuwa wakilalamika kuna makundi ya watu ambao sio wakaazi wanavamia mikutano na kutoa maoni zaidi ya mara moja kinyume na sheria,” alisema Profesa Baregu.
Hata hivyo alisema kwamba Tume yake ilikuwa na nafasi ya kuendelea kukusanya maoni baada ya kuimarisha ulinzi wa polisi, lakini hawakutaka kufanya hivyo kwa vile tume haitaki wananchi kutoa maoni wakiwa chini ya ulinzi wa askari wenye silaha, ndiyo maana wameamua kutumia askari kazu tangu kuanza kukusanya maoni yao Zanzibar.
Wakati huo huo Chama cha wananchi CUF kimelaani vurugu hizo na kutoa shutuma kali kwa Kamishina wa tume hiyo, Fatma Said Ali kuwa yeye na mwakilishi wa jimbo la Magomeni CCM, Salmin Awadhi ndiyo chanzo cha vurugu hizo.
Hata hivyo viongozi hao hawakuweza kupatikana kuelezea shutuma hizo jana lakini Mkurugenzi wa haki na Binadamu Habari na Uenezi wa CUF, Salum Bimani alisema viongozi hao waliwanyima wananchi haki ya kikatiba ya kutoa maoni na kusababisha vurugu.
Alisema wakati umefika kwa tume hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia sheria ya kuanzishwa kwa tume hiyo na viongozi kujiepusha na ushabiki wa kisiasa.
Bimani alisema wananchi wamekuwa wakijitokeza kutoa maoni yao lakini wamekuwa wakikumbana na vikwazo baada ya kufika katika vituo vya kutoa maoni kinyume na sheria ya time hiyo.
Kwa upande wake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeomba Tume hiyo kuwa macho na njama za baadhi ya vyama vya siasa za kuanda makundi ya vijana wasiokuwa wakaazi katika maeneo husika kwenda kutoa maoni na kusababisha vurugu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na katibu msaidizi wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Alli Mwinyi Msuko, alisema vurugu hizo zimesababishwa na wanasiasa kupandikiza watoa maoni mamluki.
Tangu tume hiyo ianze kukusanya maoni, wanachama na wafuasi wa CUF wamekuwa wakitetea Muungano wa serikali tatu ikiwemo ya Tanganyika, Zanzibar yenye mamlaka kamili na Muungano wa mkatba wakati wanachama wa CCM wakitetea Muungano wa Serikali mbili katika mabadiliko hayo.

http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=43438

No comments: