Tuesday, December 11, 2012

Swahili Fashion Week Yahitimishwa


SWAHILI FASHION WEEK 2012 YAHITIMISHWA MWISHONI MWA WIKI HII
GABRIEL MOLLEL ANYAKUA TUZO MBILI
GABRIEL KUIWAKILI SWAHILI FASHION WEEK KATIKA MAONYESHO YA MITINDO MSUMBIJI 2012
Baada ya miezi mingi ya maandalizi, waandaji wa Swahili Fashion Week wamefanikia kuhitimisha onyesho kubwa la mitindo na mavazi katika nchi za Afrika mashariki na kati, tukio lilinaloendelea kuiweka tasnia ya mitindo katika ramani ya mitindo Afrika na Duniani kiujumla.
Ikiwa na viwango vipya na vyenye ubora, waandaji wamefanikiwa kuwa na tukio bora la mwaka na kuwaacha wahudhuriaji wakihitaji maelezo zaidi kuhusu onyesho la 2013. Kama ilivyo ada vitu vizuri lazima viwe na mwisho, Swahili Fashion Week 2012 ilimalizika kwa kutolewa tuzo siku ya Jumamosi ya tarehe 8, Desemba 2012.
Tuzo za Swahili Fashion Week 2012 zimelenga kutambua mchango wa wabunifu mbalimbali ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya tasnia ya mitindo Afrika Mashariki. Tuzo hizo zinaongeza chachu ya uvumbuzi na ubunifu katika tasnia ya mitindo. Hii inaendana na kuifanya mitindo ya Kiswahili kujulikana duniani. Alisema Mustafa Hassanali, Mmiliki na Muandaaji wa Swahili Fashion Week.  
Swahili Fashion Week 2012, imefanyika katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo jijini Dar es salaam, kuanzia tarehe 6-8 Desemba, ikiwa tukio kubwa la Mitindo ukanda wa Afrika Mashariki na Kati lililokutanisha wabunifu zaidi ya 50 kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Mshindi wa Tuzo mbili mwaka huu, Mbunifu Mvumbuzi wa mwaka na Mbunifu Bora wa Mwaka, Gabriel Mollel ataiwakilisha Swahili Fashion Week katika week ya mitindo Msumbiji inayoanza Desemba 7-15. Kwa mwaka wa tano sasa Swahili Fashion Week imefanikiwa kuendeleza uhusiano na Mozambique Fashion Week.
“Ni faraja kuiwakilisha Tanzana na Swahili Fashion Week katika maonyesho ya Msumbiji, kushinda tuzo mbili mwaka huu, kwangu ni matokeo ya kujituma na ubunifu mzuri, ninatumia muda mwingi kutengeneza kazi zangu. Hii tuzo inanipa nguvu kubwa lakini ni changamoto kwani kazi ngumu katika maisha ni kubaki katika hadhi ile ile ambayo watu walikuamini na kukupa katika shughuli unayoifanya” Alisema Gabriel
“Kama Swahili Fashion Week ni jambo la fahari na kujivunia kuwa sehemu ya Mozambique Fashion Week, Gabriel Mollel hataiwakilisha tu Swahili Fashion Week nchini Msumbiji, ila pia anaiwakilisha nchi yetu kwa kuonyesha ubunifu na mitindo iliyotengenezwa Tanzania” Alisema Mustafa Hassanali.
Huu ni mwaka wa Tano sasa tangu Swahili Fashion Week ianze kushirikiana na Mozambique Fashion Week ambapo Mustafa Hassanali alishiriki mwaka 2007 na 2008 huku Jamila Vera Swai akiwakilisha 2009, Manju Msita 2010, Robbi Morro na Ailinda Sawe wote walienda 2011.
“Swahili Fashion Week inalengo la kutangaza, kuinua na kutafuta masoko ya bidhaa za wabunifu wa Afrika Mashariki katika soko la Afrika na duniani kote. Tasnia ya Mitindo afrika inaitaji kutambiliwa na kuwekwa katika ramani ya dunia” Aliongeza Mustafa Hassanali.
Licha ya kutambua mchango wa wadau mbalimbali wa tasnia ya mitindo Afrika Mashariki, SFW pia ilitoa nafasi kwa wabunifu vijana wanaochipukia kuonyesha kazi zao na mitindo yao kwa mashabiki wa mitindo waliohudhuria katika Swahili Fashion Week mwaka huu ambapo wabunifu mbalimbali walionyesha ubunifu wao.
Wabunifu wa Swahili Fashion Week pia walipata nafasi ya kushiriki katika semina iliyoandaliwa na USAID COMPETE kwa kushirikiana na ORIGIN AFRIKA juu ya kutafuta masoko kwa bidhaa wanazozitengeza.
Swahili Fashion Week 2012 imedhaminiwa na Vodacom, USAID Compete, Origin Africa, EATV, East Africa Radio, Golden Tulip Hotel. Amarula, Precision Air, 2M Media, Global Outdoor Ltd, Vayle Springs Ltd, Eventlites, Ultimate Security, BASATA (Baraza La Sanaa Taifa),Strut It Afrika, Ndibstyles, PKF Tanzania, DARLING, PUSH Mobile, DarLife, Century Cinemax, Natol na 361 Degrees.
Kwa Picha zaidi za Swahili Fashion Week 2012: http://ramp.sdr.co.za/1212SFW/
KUHUSU SWAHILI FASHION WEEK
Swahili Fashion Week ni jukwaa kubwa la mitindo ya mavazi la kila mwaka katika ukanda wa Afrika mashariki na kati kwa sasa. Huu ni mwaka wa Tano sasa, ambapo Swahili Fashion Week imekuwa ni Jukwaa la wanamitindo na watengeneza vito vya urembo kutoka katika nchi zinazoongea Kiswahili na bara zima la Afrika kwa ujumla kuweza kuonesha vipaji, kutangaza ubunifu wao na kukuza mtandao wa mawasiliano ya kibiashara ndani na nje ya nchi kwa wadau wa mitindo. Hili limelenga kuhamasisha ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati kwamba ubunifu wa mavazi ni njia moja wapo ya kujipatia kipato na wakati huo huo kukuza bidhaa zinazotengenezwa Afrika ( Made in Africa concept)
Ikiwa imeanzisha uhai na jukwaa la matumaini kwa kilinge cha mitindo katika ukanda huu, Swahili Fashion Week Swahili Fashion week imelenga kuwa maonyesho ya ubunifu wa mavazi linaloonekana sana Afrika na hasa kwa ajili ya soko la kimataifa, lililoundwa, kutengenezwa na kujengwa mwaka 2008 na Mustafa Hassanali.
Ifikapo mwaka 2013, Swahili Fashion Week ina lengo la kuwa ni tukio litakalotokea mara mbili kwa mwaka, ambapo kwa kuanza tukio la kwanza litafanyika nchini Kenya kama sehemu ya kwanza kisha tukio lenyewe kabisa kufanyika baadae nchini Tanzania kama sehemu ya pili.
KUHUSU GABRIEL MOLLEL
Gabriel Mollel ni muasisi wa  Sairiamu Community Action Foundation, ambayo ndio nembo yake ya ubunifu, Sairiamu inamaana “Mtu anaetoa kwa mikono miwili” katika lugha ya kimasai. Gabriel amekua akifanya kazi zake kwa mikono yake mwenyewe kwa ajili ya jamii yake kwa da mrefu kabla hajawa na jina kubwa katika uwanda wa sanaa ya ubunifu hapa Tanzania, ameweza kushiriki katika maonyesho mbalimbali ikiwemo Harusi Trade Fair, Swahili Fashion Week na mengine mengi ambapo pia amekua mshindi wa Swahili Fashion Week katika kipengele cha Mbunifu Bora 2011.

No comments: