FOUR WAYS INTERNET & STATIONERY WANASHUGHULIKA NA USAMBAZAJI WA VIFAA VYA SHULE NA MAHITAJI MENGINE YA MAOFISINI IKIWA NI PAMOJA NA HUDUMA YA INTERNET MASAA 17 KWA SIKU INAFUNGULIWA SAA 7:00 HADI SAA 10:00 USIKU K A R I B U S A N A
Sunday, December 30, 2012
UTAJIRI WA GESI ASILIA: TUWASIKILIZE WATANZANIA WA MTWARA NA LINDI TUSIPUUZE
Mh zitto Kabwe
Maandamano ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki hii yameibua hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook, twitter na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji wapuuzi na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.
Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho yao na wanaona.
Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea kushindwa.
Mtwara na Lindi wanataka nini?.
Watu wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi nzima. Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike Mtwara tu la hasha.
Sio dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa maoni yao. Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini?
Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? Tumesahau ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza mapato mengi sana ya Fedha za kigeni? Waziri Muhongo anasema Mtwara warudishe Fedha za Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho? Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya Tumbaku.
Lakini tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge? Walifaidi fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau hata Reli iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali huru ya Tanzania?
Tujiulize zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu ya thamani ya dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa Mtwara wana Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye Gesi asilia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment