Wednesday, January 2, 2013

Juma Kilowoko ‘Sajuki’ Amefariki Dunia Leo Alfajiri




Simon Mwakifwamba (kushoto) na wadau wengine wakimsaidia Sajuki (katikati) kutoka jukwaani baada ya kudondoka katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha mwishoni mwa mwaka jana.
STAA wa filamu za Kibongo, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ amefariki dunia leo alfajiri katika hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa anapatiwa matibabu. Kwa mujibu wa Katibu wa chama cha waongoza Filamu Wilaya ya Ilala, Rajabu Amiri ni kwamba hivi karibuni Sajuki alikuwa anasumbuliwa na tatizo la upungufu wa damu. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amen!
CHANZO CHA KIFO CHAKE
sajuki
Inna lilahi Wainna Illaihi Raajuni Zanzibardaima imepokea taarifa ya kifo cha Msanii maarufu wa filamu nchini Tanzania anaejuulikana kwa jina Juma Kilowoka maarufu kama (Sajuki )msanii huyo amefariki duni alfajiri ya kuamkia leo katika hospitali ya Taifa muhimbili jijini Daresalam.
Ineleweka  kwamba  msanii huyo alikuwa anauguwa na maradhi yaliosababisha uvimbe ndani ya Tumbo lake lakini kwa msaada wawasamaria wema waliweza kumchangia na kumfanya apate matibabu nchini India ambapo hali yake iliendelea kuimarika na kuwa nzuri kwa afya yake badae na baadae kurudi Nchini Tanzania.
Baada ya kurudi nchini Tanzania msanii huyo aliona ni busara kwenda kuwashukuru baadhi ya watu waliosabaisha kufika kwake India kwa matibabu na baadhi ya mashabiki wake ndipo alipoamua kuenda Mkoani Arusha takribani wiki moja iliopita kwa lengo la kutoa shukrani kwa wakaazi wa jiji hilo kutokana na ushirikiano wao waliouwonesha kwake  wakati akiugua,Jijini Arusha alipokelewa na Umma mkubwa wawatu uliofika hapo kwa ajili ya kumuona msanii huyo lakini kutoka na watu kuwa wengi sana waliofika kumuona kukampelekea Sajuki  kupata mshituko wa Moyo ghafla na kuanguka chini na badala yake kukimbizwa hosptil kwa ajili ya matibabu zaidi lakini kwa kudra ya Mwenyezimungu ameweza kumchukua kiumbe wake alfajiri ya kuamkia leo.
 SOMA ZAIDI JUU YA KIFO CHA SAJUKI

Asubuhi ya leo nimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha msanii wa filamu marehemu Sajuki, vyovyote iwavyo, maanake tusubiri magazeti  PENDWA kuanza kukufuru kwa kusema kuwa freemason wanahusika na kifo cha kila msanii anayekufa, hata Sajuki watasema katolewa kafara na freemason. Mimi nimetafakari nikaona ni vema niweke mambo sawa kwa upeo wangu kabla ya hao waandishi wanaomkufuru mungu hawajaanza kuuza nakala zao chafu. Hebu tujifunze kwa manabii na watu wema pindi wakipatwa na misiba walikuwa wanafanya nini huenda tutapata mazingatio kutoka kwao.
“…Ndipo Daud akainuka pale chini, akaoga, akajipaka mafuta, akabadili mavazi yake, akaingia nyumbani mwa BWANA akasali…mtoto alipokuwa hai, nalifunga, nikalia, kwa maana nalisema, ni nani ajuaye kuwa BWANA atanihurumia mtoto apate kuishi? Je, naweza kumrudisha? Mimi nitakwenda kwake lakini yeye hatanirudia mimi” 2 samweli 12:16-23
Hayo ni maneno ya mfalme Daud[a.s] aliyatamka mara baada ya kufiwa namtoto wake aliyezaa naye na mwanamke wa Uria, huyo mtoto alikuwa kaka yake na Suleiman, hakuaa sana mara baada ya kuzaliwa, aliugua sana na hatimaye akafa. Hivyo ndivyo Mfalme alivyopokea kifo cha mtoto wake, na sisi tuvipokee hivyo vifo vya wapendwa wetu. Huwa sishangai nikiona walokole wakipiga miziki ya kumsifu mungu kwenye misiba yao, hivyo ndivyo inavyotakiwa, tumsifu mungu kwaajili ya vifo vya wapendwa wetu badala ya kumkufuru. Wengine wakifiwa wanaenda kwa waganga kupiga bao ili kujua ndugu yao kafa kafaje.
Ni muda mrefu Sajuki amekuwa akipigania uhai wake, na muda wote huo alikuwa anapata mateso makubwa kwa maradhi yaliyokuwa yanamsibu, ama kwa hakika imeniwia vigumu kuficha simanzi niliyonayo sasa. Pamoja na hayo kifo ni kiumbe, naam, kimeumbwa na BWANA kwa makusudi yake. Amini niwaambiayo kuwa, kifo kimeumbwa kwaajili ya siku ya kufa, hivyo hayana budi kuwa midhali tungali tu juu ya mgongo wa ardhi, eeh!!! kila mtu lazima afe haijalishi ni tajiri, maskini, mwenyehekima, mpumbavu, nk. rejea mithali 16:4 na muhubiri 2:14-17.
“macho yake mwenye hekima yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani; ila hata hivyo nikatambua ya kwamba ni tukio moja la mwisho liwapatalo wote sawasawa. Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili. Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu! Basi, nikauchukia uhai; kwa sababu kazi inayotendeka chini ya jua ilikuwa mbaya kwangu; yaani, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo.” Mhubiri 2:14-17
“Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.” Mithali 16:4
Mhubiri 2:14-17 ni aya ambazo zimemnukuu mfalme Suleiman, akifafanua ulazima wa kifo sanjari na upuuzi wa kuwekeza duniani na kusaahu ahera yetu. Kila tendo tulifanyalo liwe sehemu ya ibada, kuanzia kula, kuvaa, kutafuta riziki, kuoa na kuolewa, kuzika, na mambo yote ayafanyayo mwanadamu kwa masaa 24 lazima yawe chini ya sheria ya mungu na hiyo ndio ibada.
Mithali 16:4 pia ni maneno ya mfalme Suleiman, ambayo yanatuambia kila kitu kimeumbwa kwa kusudi lake, wenzangu hata kifo kimeumbwa na kusudi lake, kinyume chake kisingeumbwa. Hivyo si vema kupambana na kifo kwa kumeza ng’aramo, tuache mapenzi ya mungu yatimizwe.
Hakuna jambo kubwa ambalo shetani analitumia kumpoteza mja isipokuwa ni “kifo”. Shetani ametufanya tuogope kifo badala kumuogopa muumba wa kifo. Miongoni mwetu tumekuwa tukimuasi Mola wetu ili mradi tupate kukiepuka kifo, tena twafanya haya ili hali tukijua kuwa haitowezekana kamwe kukiepuka kifo!
Nikisema haya haimaanishi kuwa nazipinga jitihada za kujitibu zenye lengo la kutupunguzia si kama kutuondolea maradhi yasababishayo adha na maumivu kwa miili yetu, hapana, sizipingi na ninazikubali, kwani zimethibiti katika misahafu ya dini zote. Ninachopinga mimi ni jitihada zenye lengo la kutuepusha na kifo.
Mtume Muhamad[s.a.w] alinukuliwa akisema “kila maradhi yana dawa yake, isipokuwa kifo na uzee”. Kwa mujibu wa nukuu hii kifo kimefananishwa na maradhi, maradhi ambayo yasokuwa na dawa. Hii ina maanisha nini? Hii ina maanisha kuwa, kwa mujibu wa uislamu ni haramu kutafuta hila au mbinu ya kujiepusha na kifo.
Ifike mahala tutamani kufa zaidi kuliko hata kuishi, kwani tunapata mmea wa ngano wenye mashuke mengi kwa kuzika mbegu bora ya ngano.Mja mwenye kufanya mema mwili wake ni kama mbegu bora ya ngano. Mwili wa mtu mwema ndio huleta mwili wa milele uso shikwa na hukumu ya kifo wala ya kuharibika.
“Amin, amin, nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali hiyo hiyo peke yake; bali ikifa hutoa mazao mengi” mathayo 12:24
“Ndugu zangu , nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu haziwezi kurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika…maana sharti huu uharibikao uvae kutoharibika, na huu wa kufa uvae kutokufa…mauti imemezwa kwa kushinda” 1 wakorintho 15:50-54
“Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu.” Qur-an 29:57
“Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa” qur-an 21:35
Misaafu yote ya kiislamu na kikristo imekubalina pasina kukhitalifiana juu ya ulazima kifo kwa kiumbe, kifo ambacho kitapelekea roho kuvaa mwili usioharibika tayari kwa kupokea kheri au shari. Kwakuwa kifo ni hatua ambayo kamwe hatuwezi kuiruka katika maisha yetu, hakuna umuhimu wowote wa kulia na kuhuzunika kupita kiasi hata tukufuru kwaajili ya wapendwa wetu, badala yake ni bora tuwaombee maghufira kwa M/mungu ili wapate kusamehewa dhambi zao na kuzidishiwa malipo kwa mema waliyoyafanya kabla ya vifo vyao kuwakuta.
“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu” qur-an 14:41
Tuutamani mwili uso kuwa na udhaifu wala kuharibika kwa kuukinai mwili wenye udhaifu na kuharibika, kinyume chake tujiandae kucheza kidugu na mashetani katika jahnam. Kiduguku ambacho kitatufanya tulie kilio kikuu na cha kusaga meno. Eeeh! M/mungu tuepushe na adhabu ya moto sisi na wapendwa wetu waliotangulia mbele yako na turuzuku pepo zenye daraja kubwa inshallah!
Petu pazuri lakini kwenda shughuli, huko petu hakuna maradhi, umaskini, vita, wala njaa. Kuna kila namna ya raha na starehe. Kwa sisi wanaume kuna mahurain; wanawake warembo wasikuwa na siku mbaya hata moja katika mwezi, watakuwa ni makonde yetu na tutayaingilia tupendavyo. Kwa wanawake watakutana na majamali; wanaume ambao hawajui kuchoka wala kukinai, wapo kwaajili ya kuongeza nakshi kwenye Firdausi hata paitwe ni sehemu ya raha na mustarehe.
Huko hakuna uchungu wa kuzaa wala uchungu wa limbuko la mapenzi kwa wanawake, huko kila kitu kitamu, yaani kila kitu kizuri. Kama ndivyo kwanini tusitamani kifo? Machozi yetu na yawe dhahabu na ya tiririke kwenda juu kwa umbo la ngazi au njia, yakikauka na yawe njia kwetu na ngazi ya kutufikisha kwa mpendwa wetu Sajuki na wengineo ambao wametangulia mbele ya haki huko mbinguni.
Niko na imani Sajuki ametangulia kwenda kutuandalia makazi. Tumuache Sajuki ajiandae kutupokea nyumbani, naam, kutupokea katika mji wenye rangi nzuri na adhimu, mji wenye rangi ya manjano. M/mungu amlipe badala ndugu yetu mpendwa kwa kila jambo la kheri alilolitenda hapa duniani, na wala asimuhesabie kosa, si kama tutakavyo sisi, bali atakavyo YEYE MWENYEWE, MAPENZI YAKE YATUKUZWE NA JINA LAKE LIHIMIDIWE.

No comments: