HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WATANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 31 JANUARY, 2013
UTANGULIZI
Ndugu Wananchi;Kama ilivyo ada naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye Rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuzungumza kwa mara nyingine kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina ya Rais na wananchi wa Tanzania kila mwisho wa mwezi. Siku ya leo nitazungumzia safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia. Pia nitazungumzia ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Safari za Kikazi Nje ya Nchi
Ndugu Wananchi
Safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu. Nchini Ufaransa licha ya kuimarisha uhusiano wa kirafiki baina ya nchi zetu, tumepata wawekezaji wengi wakubwa wenye nia thabiti ya kuja kuwekeza hapa nchini. Pia tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa na mpango mwingine wa ushirikiano. Mpango wetu wa sasa ulioanza mwaka 2006 uliisha mwaka 2010. Mpango ule ulitusaidia sana kuboresha huduma za maji katika miji ya Utete mkoani Pwani na Mpwapwa mkoani Dodoma.
Katika mkutano wa Kongamano la Uchumi wa Dunia uliofanyika Davos, Uswizi, tumehakikishiwa ushirikiano katika kuendeleza juhudi zetu za kuleta mapinduzi ya kijani ili tujihakikishie usalama wa chakula na kupunguza umaskini vijijini na kukuza uchumi wa nchi yetu. Aidha, tulipata bahati ya kushirikishwa katika mjadala wa kuanzishwa kwa programu kubwa ya kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya upatikanaji wa umeme. Naamini programu hiyo ikitekelezwa na wakubwa kuheshimu kauli na ahadi zao itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ndugu Wananchi;
Nchini Ethiopia tulishiriki katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na katika kikao cha African Peer Review Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya tathmini ya utawala bora ya Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa. Kwa jumla hatuna mahali tuliponyooshewa kidole kuwa tunafanya vibaya.
Tumepongezwa katika mambo mengi na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona hatuna budi kuyaboresha. Nilipata nafasi ya kusema ambayo niliitumia kufafanua baadhi ya mambo yaliyokuwamo kwenye taarifa. Niliwashukuru na kuahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa. Tathmini ya nchi yetu ilipitishwa kwa kauli mojaVurugu za Kupinga Gesi Kusafirishwa Kutoka Mtwara
Ndugu wananchi;
Kama mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba, 2012 kule Kinyerezi, Wilaya ya Ilala hapa Dar es Salaam, niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam. Karibu na mwishoni mwa Desemba, 2012 kukafanyika maandamano mjini Mtwara kupinga ujenzi wa bomba hilo.
Katika maandamano yale na baadaye kwenye kauli za wanasiasa na wanaharakati yakatolewa madai kuwa gesi hiyo itumike kwa maendeleo ya Mtwara na kwamba yale yanayotakiwa kufanyika Dar es Salaam yafanyike Mtwara. Pia, zilitolewa shutuma nyingine dhidi ya Serikali eti kuwa kwa miaka mingi imewasahau na haiwajali wananchi wa Mikoa ya Kusini na ujenzi wa bomba hilo ni muendelezo wa hayo. Kauli mbalimbali za wanasiasa na wanaharakati ni kama vile ziliongeza mafuta kwenye kaa la moto na kuuchochea mpaka kukatokea matukio yaliyotusikitisha na kutshtua sote. Baadhi ya ndugu zetu wamepoteza maisha na mali za watu na Serikali kuharibiwa.
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya kuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013, tarehe 31 Desemba, 2012, nililisemea jambo hili. Leo mwezi mmoja baadae, napenda kusisitiza mambo mawili. Kwanza kwamba, si kweli kuwa Serikali inapuuza Mikoa ya Kusini. Na pili, kwamba kujenga bomba la kuipeleka gesi Dar es Salaam hakuinyimi Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa ya kunufaika na gesi iliyopo Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Serikali imefanya, inafanya na ina mipango ya kufanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya kuleta maendeleo katika Mikoa ya Mtwara na Lindi. Ipo mipango ya kuboresha miundombinu, huduma za kiuchumi na kijamii pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vikubwa na vidogo. Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika Mto Rufiji maarufu kama Daraja la Mkapa. Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya awali katika safari ya kutatua matatizo ya usafiri ya Mikoa ya Kusini. Serikali ninayoiongoza mie iliachiwa kazi ya kukamilisha ujenzi wa barabara za lami kufikia darajani na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Ruvuma. Kazi hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia kuimaliza. Tulikamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mnazi-Mmoja hadi Nangurukuru. Mwaka 2009 tukaanza ujenzi wa barabara ya kilomita 56 kutoka Somanga hadi Ndundu (darajani). Ujenzi wakilometa 36 za mwanzo ulienda vizuri. Bahati mbaya ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho umechelewa sana kwa sababu ya mmiliki wa kampuni iliyokabidhiwa kufanya kazi hiyo kufariki. Kwa sababu hiyo, kampuni ilipata mtikisiko kiasi na kusababisha kazi kutotekelezwa kwa kasi tuliyoitarajia. Sasa mambo yametengemaa na kazi inaendelea kwa kasi nzuri. Matumaini yetu ni kuwa ifikapo mwezi Desemba, 2013 kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Hali kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee Benjamin Mkapa alituachia jukumu la kumaliza ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma na ujenzi wa barabara ya lami kuanzia Mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Tumelikamilisha Daraja hilo na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi hadi Mangaka umekamilika. Mchakato wa kujenga barabara ya kwenda Songea na kwenda Darajani umefikia mahala pazuri. Tenda ya ujenzi wa barabara kutoka Tunduru hadi Mangaka mpaka Darajani imeshatangazwa. Kama mambo yataenda sawa miezi mitatu ijayo mjenzi atapatikana. Wakati huo huo ujenzi wa barabara kutoka Namtumbo hadi Songea – Mbinga na Namtumbo – Tunduru unaendelea. Hivyo basi, kwa barabara ya “MtwaraCorridor” kazi iliyobaki ni kutoka Mbinga kwenda Mbambabay ambayo tutaifanya wenyewe kama tulivyofanya kwa Mnazi Mmoja – Nangurukuru na Somanga – Ndudu na Daraja la Umoja.
Ndugu Wananchi;
Ipo pia mipango ya kuipanua na kuijenga upya bandari ya Mtwara ili iweze kuhudumia mahitaji ya utafutaji na uchimbaji wa gesi baharini, kuhudumia na kuvifanyia matengenezo vyombo vinavyotumika katika utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi. Pia iweze kuhudumia shughuli za kiuchumi zitakazotokana na uchumi wa gesi pamoja na zilizopo sasa. Nilipozungumza na makampuni ya utafutaji gesi pale Mtwara tarehe 25 Julai, 2011 waliomba nikubali bandari ya Mtwara iwe mahali pa kuhudumia vyombo vyote vinavyofanya shughuli ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta katika pwani ya Afrika ya Bahari Kuu ya Hindi. Pia waliomba kuwa sehemu hiyo ya bandari iwe bandari huru. Niliwakubalia bila ya kusita na tayari eneo la hekta 110 zimeshatengwa na kutangazwa rasmi kuwa bandari huru. Vile vile waliomba wapewe sehemu ya bandari ya sasa kuendeshea shughuli na eneo la kujenga kituo cha mitambo ya kuchakata gesi na kusafirisha nje.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kuzungumza na makampuni ya utafutaji gesi na mafuta na kuelezwa mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara inahitaji kupanuliwa na kujengwa upya. Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya Bandari walikuwepo na walinihakikishia kuwa watafanya hivyo.
Tayari eneo la bandari limeongezwa kutoka hekta 70.68 hadi 2,693.68. Eneo la bandari huru limeshatengwa hivyo hivyo na eneo la kampuni ya Dangote na makampuni ya gesi yaliyopo. Aidha, mchakato wa kupanua bandari iliyopo, kujenga gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo ya Msanga Mkuu ipo katika hatua mbalimbali za matayarisho na utekelezaji.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mkoa wa Lindi mipango ya kupanua na kuijenga upya bandari ya Lindi imefikia hatua nzuri. Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo tarehe 1 Desemba, 2012 nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Lindi ya tarehe 1 mpaka 5 Desemba, 2012. Hali kadhalika mipango ya kujenga bandari ya Kilwa iko mbioni. Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi moja ya makampuni yaliyogundua gesi baharini wameamua kujenga bandari na kituo cha kuchakata na kusarifisha gesi nje ya mkoa huo kama ilivyo kwa Mtwara. Naambiwa wametambua maeneo matatu, kilichobakia ni kuamua mojawapo ili ujenzi uanze.
Ndugu Wananchi;
Nilipotoka bandari ya Mtwara, siku ile nilitembelea Chuo cha VETA na kuzungumza na viongozi wa VETA taifa na wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa na mitaala ya kutoa mafunzo mahsusi yanayohitajika na sekta ya gesi na mafuta. Nilisisitiza kwamba tuwapatie vijana wetu mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni ya gesi na yale yatakayokuwa yanatoa huduma kwa makampuni hayo. Nilisema tusipofanya hivyo, makampuni hayo yataajiri watu kutoka nje na hatutakuwa na sababu ya kuwalaumu wala kulalamika.
Nafurahi kwamba agizo langu hilo limefanyiwa kazi ipasavyo. Hivi sasa katika chuo cha VETA Mtwara mafunzo hayo yanatolewa. Kampuni ya PetroBrass ya Brazil inaendesha mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana 25 kutoka mkoani Mtwara. Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana na Kampuni ya Gesi ya Uingereza (British Gas) na Volunteers Service Overseas ya Uingereza, kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo Enhancing Employerbility Through Vocational Training. Programu hii inalenga kutoa kozi zitakazowafanya wahitimu kuweza kuajiriwa katika sekta ya gesi. Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012.
Ndugu Wananchi;
Chini ya programu hii, walimu wa masomo yanayohusiana na gesi wanaongezewa ujuzi ili waweze kufikia viwango vya kimataifa. Vile vile, Wizara ya Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa kudhamini wanafunzi 50 kutoka mkoa wa Mtwara kusoma chuoni hapo ambao tayari wameshahitimu mafunzo ya msingi ya uunganishaji vyuma viwandani. Mchakato wa kuwapata wanafunzi 50kwa ajili ya mafunzo kama hayo kutoka mkoa wa Lindi unaendelea. Nimeambiwa mpaka wameshawapata vijana 25 bado 25.
Hali kadhalika, Wizara ya Nishati na Madini inadhamini wanafunzi 10 kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambako kozi za mafuta na gesi zinatolewa. Kipaumbele kwa udhamini huu unatolewa kwa wanafunzi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za kudahiliwa katika mafunzo haya. Wamepatikana watatu. Wataalamu hawa na wengine wa fani mbalimbali za gesi na mafuta watafundishwa kwa kiwango cha shahada ya kwanza na baadae uzamili na uzamivu ili nchi yetu ijitosheleze kwa wataalamu wa sekta hii.
Kupanga Mji wa Mtwara
Ndugu Wananchi;
Baada ya kutembelea bandari ya Mtwara na Chuo cha VETA, nilikaa na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Manispaa ya Mtwara. Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu wa kuwa na mpango kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango ambao utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji wa uchumi wa gesi. Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda, biashara, makazi, mahoteli, huduma za afya, elimu, mapumziko na burudani, viwanja vya michezo na kadhalika. Kazi ya kutayarisha Masterplan hiyo imeanza na Manispaa ya Mtwara inashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi.
Kwa upande wa uwekezaji nafahamu kuwa mpaka sasa makampuni 51yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda, hoteli, shughuli za uchukuzi na huduma hasa kwa sekta ya gesi. Wanachosubiri ni kutengewa maeneo ya kujenga, waanze. Hivyo kukamilika mapema kwa Masterplan ya mji wa Mtwara kutasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji huu kufanyika. Viwanda hivi vyote vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mtwara na Watanzania kwa jumla. Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi wa kiwanda cha saruji watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa.
Ndugu Wananchi;
Kabla hata ya ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na mipango ya kutumia gesi ya Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kuzalisha mbolea na kutumika katika kiwanda cha saruji. Kwa upande wa umeme kulikuwa na mpango wa kujenga mtambo wa kuzalisha Megawati 300 kwa kushirikiana na mwekezaji binafsi. Bahati mbaya wakati wa matatizo ya kifedha ya dunia mwaka 2009 mwekezaji huyo akashindwa kupata mkopo, hivyo mradi ukasimama kutekelezwa. Haukufa wala haukuhamishiwa Dar es Salaam au Bagamoyo kama ambavyo imekuwa inapotoshwa kwa makusudi. Mradi huo bado upo, tena mpango wa sasa ni kujenga Megawati 600 zitumike Mtwara na zingine kuziingiza kwenye gridi ya taifa kupitia Songea.
NduguWananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha mbolea, wawekezaji wengi wameshajitokeza tangu mwaka 2008 mpaka sasa. Mchakato umefanyika wa kuchambua wawekezaji wenye sifa na kutambuliwa. Mambo mawili yamechelewesha utekelezaji kuanza. Jambo la kwanza ni wawekezaji na kampuni ya Artumas iliyokuwa mbia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (T.P.D.C) wakati ule, kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya kuwauzia gesi. Wawekezaji walitaka bei ya gesi ipunguzwe, lakini kampuni ya Artumas na T.P.D.C. hawakuwa tayari kupunguza zaidi ya kiasi walichopunguza, ambacho wawekezaji bado waliona hailipi kwa kuzalisha mbolea.
Sababu ya pili ni matatizo ya kifedha yaliyoikumba kampuni ya Artumas katika kipindi hicho. Kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni ya Artumas iliathirika na kulazimika kuuza hisa zake kwa wawekezaji wengine. Katika kipindi hicho ilichopitia kampuni, mazungumzo na uwekezaji wa kiwanda cha mbolea hayakuweza kupewa kipaumbele. Mtazamo wa sasa wa wabia wapya na T.P.D.C. ni kuwa wao wenyewe sasa wawekeze katika ujenzi wa kiwanda cha mbolea. Serikali imekubali rai yao hiyo na wanaendelea na matayarisho.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni ya Dangote ucheleweshaji ulikuwa kwa sababu mbili. Kwanza, kampuni ya Dangote iliomba eneo zaidi ya ililokuwa imeomba na kupewa. Hoja yao ilikuwa kwamba eneo la ziada walilokuwa wanaliomba ndilo lenye malighafi nyingi na bora kwa utengenezaji wa saruji. Hivyo, waliamua kusubiri mpaka watakapopewa eneo hilo.
Bahati mbaya eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine na alikuwa na hati miliki nalo. Halmashauri ya Mtwara iliomba Serikali eneo hilo litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote. Serikali ilikubali. Hata hivyo, mchakato ulichukua muda na hata pale ulipokamilika mwenye eneo aliupinga uamuzi wa Serikali Mahakamani. Kesi ilichukua muda kusikilizwa na kumalizika. Bahati nzuri Serikali ikashinda na mara baada ya uamuzi wa Mahakama ndipo kampuni ya Dangote ikamilikishwa eneo hilo.
Kampuni nayo ilichukua muda kuanza. Hivi sasa, timu yake ipo kwenye eneo na mradi uko tayari kuanza kutekelezwa. Niliambiwa kuwa katika magari yaliyopigwa mawe katika fujo za Mtwara ni pamoja na lile la mradi huu. Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote. Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya kweli. Ni uzushi wa makusudi wa watu wenye nia mbaya na Serikali. Huwezi kudai kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara kwa hoja za uongo na kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu. Zilijengwa hisia kuwa gesi yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatayotokana na gesi hiyo. Na, wengine wakasema gesi inapalekwa Bagamoyo ili kuzidisha chumvi na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba Rais anapeleka gesi kwao. Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo. Pili, ukweli ni kwamba pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na kubaki. Gesi itakayoletwa Dar es Salaam ni asilimia 16 tu ya gesi yote iliyoko Mtwara kwa miaka ishirini ijayo. Hivyo asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini.
Kwa sababu hiyo, ndugu zetu wa Mtwara hawana sababu ya kuwa na wasiwasi. Ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya miaka mingi ijayo. Viwanda vinavyotumia gesi kama mali ghafi na vile vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya kutosha. Kwa upande wa uzalishaji umeme hali kadhalika ipo gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi. Hivi sasa tunacho kituo kinachozalisha umeme wa megawati 15 unaotumika Mtwara, Lindi, Tandahimba, Newala, Masasi, Nachingwea, Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo hautumiki wote hivi sasa.
Ndugu Wananchi;
Nayaeleza yote haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa tunawathamini sana na kuwajali. Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya Kusini. Aidha, sitakuwa tayari kuwaruhusu watu au mtu ye yote Serikalini kuwapuuza wananchi wa Mikoa ya Kusini au mkoa wo wote hapa nchini. Hiyo haitakuwa sawa. Nilishasema siku za nyuma na napenda kurudia tena leo kuwa kwangu mimi hakuna mkoa ulio bora kuliko mwingine. Ni kutokana na msimamo wangu huo ndiyo maana tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za Serikali katika mikoa iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa. Kazi ya ujenzi wa barabara za lami iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera inajieleza yenyewe. Mipango ya kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kufikia hadhi ya kimataifa na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na Kilwa ni ushahidi mwingine kati ya mambo mengi tunayoweza kuyataja.
Ndugu Wananchi;
Haya niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa na kuelezwa kwa kina na Mawaziri na Wakuu wa Idara husika za Serikali na Mashirika ya Umma pale Mtwara katika mkutano wa Waziri Mkuu na viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa na wazee wa Mkoa wa Mtwara tarehe 29 Januari, 2013.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kule Mtwara. Uvumilivu wake, usikivu wake na utulivu wake vimesaidia sana kulivusha taifa katika moja ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta nchi yetu tangu Uhuru. Nawapongeza Mawaziri na Wakuu wa Mashirika ya Umma na Idara za Serikali kwa mchango wao muhimu walioutoa, uliosaidia kufafanua masuala ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri. Kwa wao nawasisitiza na kuwakumbusha wajibu wao wa kuelimisha jamii kuhusu shughuli wazifanyazo. Wakifanya hivyo mara kwa mara migongano haitakuwepo na wapotoshaji hawatapata nafasi.
Ndugu Wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu ya dini, viongozi wa jamii, wazee, wana-Mtwara na makundi mbalimbali ya jamii, kwa muda waliotumia kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza wasaidizi wake wakifafanua masuala mbalimbali. Uvumilivu wao na uelewa wao ndivyo vilivyosaidia kurejesha hali kuwa ya kawaida. Nawaomba nao sasa, wote kwa pamoja washirikiane na Serikali kuelimisha umma kuhusu ukweli wa mambo. Pia watumie nafasi hiyo kutahadharisha jamii na kuwataka watu kuwa waangalifu na kupima maneno wanayoambiwa na watu. Wajiepushe na maneno au vitendo vinavyofarakanisha, kuchonganisha na kupandikiza chuki dhidi ya watu au Serikali. Waambieni kuwa ghasia hukimbiza wawekezaji kwani wakipata hofu kuwa hali ya amani na usalama ni ya mashaka, watatoka kwenda kuwekeza kwingine. Vyema iwe hapa hapa nchini, lakini wanaweza kwenda nchi nyingine na sisi kupoteza kabisa.
Ndugu Wananchi;
Nawapa pole wananchi wa Mtwara na Masasi kwa usumbufu walioupata kutokana na ghasia zilizofanywa. Nawapa pole waliofiwa na kujeruhiwa. Nawapa pole waliopoteza au kuharibiwa mali zao. Kwa kweli inasikitisha na kufadhaisha kuona watu wanafanya vitendo vya kuua, kuchoma moto nyumba za watu na majengo ya Serikali pamoja na , kuharibu na kuiba mali za watu. Huu ni uhalifu ambao hauna maelezo na haukubaliki. Tunaviachia vyombo husika vya dola na sheria kutimiza wajibu wao. Kwa waliohusika iwe fundisho kwao na kwa wengineo kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wengine siku zijazo. Sasa wameachwa pekee yao wakati wenzao wako huru na kufaidi maisha
Ndugu Wananchi;
Hili sakata la bomba la gesi limefika mahali pazuri. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni Sana kwa Kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment