Sunday, March 25, 2012


Uchaguzi Arumeru Mashariki, Daftari la Wapigakura lafanyiwa marekebisho.

Na Eliud Russeta 
Dar es Salaam.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imelifanyia marekebisho madogo Daftari la Kudumu la Wapiga Kura  kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha.
Katika marekebisho hayo, NEC imewaingiza wapiga kura 26 kwenye daftari hilo na kufanya idadi yao kufikia 127, 455 kutoka 127,429 wa mwaka 2010
Taarifa za marekebisho hayo zimetolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Damian Lubuva ambaye amesema yamefanyika baada ya kubaini kuwepo kwa wapiga kura 54 waliojiandikisha zaidi ya mara moja na wengine vitambulisho vyao kuharibika, wakati 28 wamejitokeza zaidi ya mara moja kwenye daftari hilo lililotumika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Hata hivyo Jaji Lubuva amewatoa hofu wananchi kuwa marekebisho hayo ni halali na hakuna utata wowotekamainavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa.
Kutokana na marekebisho hayo, jumla ya watu 127, 455 wanatarajiwa kupiga kura kwenye uchaguzi huo Aprili Mosi mwaka huu katika vituo 427 vilivyopo ndani ya kata 17 za Arumeru Mashariki.
Katika hatua nyingine Jaji Lubuva amesisitiza kuwa Mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM kwenye uchaguzi huo Sioi Sumari ni mgombea halali kwa sababu ni raia waTanzania.
Amesema licha ya Sumari kuzaliwa nchiniKenyana wazazi wake kuwa Watanzania lakini hakuwa na uraia waKenyana hivyo ni mgombea halali.
Awali Machi 9 mwaka huu Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kilimwekea pingamizi mgombea huyo kwa madai kuwa siyo raia wa Tanzania bali ni raia wa nchini Kenya kabla ya tume ya taifa ya uchaguzi kulitolea ufafanuzi jambo hilo.


Kampeni za Arumeru Mashariki, Wagombea waendelea kunadi sera zao.


Arumeru.
Zikiwa zimebaki siku sita kabla ya  uchaguzi  mdogo wa ubunge  jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha kufanyika, vyama vya CCM na CHADEMA vinaonekana kuzidi kuchuana.
Wagombea wa vyama hivyo na wapiga kampeni wao wanazidi kusambaa maeneo mbalimbali ya jimbohilokuwashawishi wapigakura wawachague wagombea wao Aprili mosi mwaka huu.
Mgombea ubunge kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Sioi Sumari amepanda jukwaani kuomba ridhaa ya wapiga kura wamchague awe mbunge wao kwa kuwa ana uwezo wa  kutatua  kero  mbalimbali zinazowakabiliwa wananchi  wa jimbo  hilo.
Baadhi ya makada  wa  chama  hicho wamewaomba  wapigakura  kumchagua mgombea wa CCM  kwa kuwa ndiye anayeweza kusikilizwa kwa urahisi  na Serikali  anapopeleka matatizo yao.
Kwa  upande wake mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Joshua Nasari amesema kero zinazoyakabili makundi mbalimbali katika jimbohilo ndizo zilizomsukuma kuomba kuwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki.
Wapiga kampeni wa chama hicho wanaoambatana na mgombea huyo wamebeba jukumu la kuwaomba wapigakura kumchagua mgombea wa CHADEMA.
Vyama vinane ndivyo vinawania kiti cha ubunge kilichoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki Jeremia Sumari aliyefariki Januari 19 Mwaka huu.





 Wazo Langu

Wanasiasa Arumeru Mashariki msiwaingize polisi lawamani
Imeandikwa na Stella Nyemenohi; Tarehe: 20th March 2012 @ 14:59 Imesomwa na watu: 104; Jumla ya maoni: 0

 






“WANAACHA kunadi sera wanaingilia mambo ya ajabu, mara huyu ukoo wao hivi mara huru si raia. Haya mambo hayana manufaa kwa wananchi ambao lengo lao ni kutaka kusikia sera zitakazowaletea maendeleo”.

Hii si kauli yangu, bali ni ya Naibu Kamishna Msaidizi wa Polisi, Isaya Mngulu.

Huyu ndiye Mkuu wa Operesheni za Uchaguzi kwa Jeshi la Polisi katika Jimbo la Arumeru Mashariki, ambaye amekaririwa hivi karibuni akivionya vyama vya siasa kuepuka fujo na vurugu.

Japo kuchokonoana mambo binafsi si mambo mageni katika kampeni za uchaguzi si tu kwa Tanzania, kwa kauli hiyo ya Mngulu, inadhihirisha namna ambavyo Polisi imebaini kuwa mwelekeo wa kampeni unakwenda kusiko.

Taarifa zinaonesha, kwamba katika kampeni za uchaguzi Arumeru Mashariki, kuna lugha za matusi, uchanaji wa bendera za vyama na picha za wagombea.

Hivi karibuni imeelezwa kuwa msafara wa mgombea ubunge wa CCM, Sioi Sumari, ulishambuliwa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa Chadema.

CCM katika kuzungumzia tukio hilo, imetishia pia kuwaagiza vijana wake kuingia msituni iwapo vitendo vya vurugu dhidi yake vitaendelea.

Hii ni hatari. Ni vyema chama hiki kisitekeleze azma hii. Badala yake kizingatie usemi wa ‘akupigaye shavu la kulia mgeuzie na la kushoto’, ili kuepusha shari.

Ingawa katika siasa, falsafa ya ‘jino kwa jino’ ndiyo hupewa nafasi, lazima iangaliwe kwa umakini ili isije ikazaa hali tete inayoweza kuwagharimu si tu watu wa Arumeru Mashariki, bali pia Taifa zima.

Kwa mujibu wa Polisi, imeshapokea mashitaka matano ya vurugu na fujo katika mikutano ya kampeni.

Nayo ni ya uchanaji wa bendera za vyama vya siasa, picha za wagombea, lugha za matusi zinazodhalilisha wagombea na viongozi wa vyama hivyo.

Haya ndiyo yamelisukuma Jeshi hilo kupitia kwa Mngulu, kutoa onyo kwa wanasiasa. Polisi imeona fujo na vurugu zinaweza kusababisha hata damu kumwagika.

Polisi ina wajibu mkubwa wa kutoa onyo na kuimarisha usalama mapema ikizingatiwa kwamba mambo yakishaharibika, Jeshi hilo ndilo hulaumiwa.

Kama yalivyo majukumu yao, vurugu zikishatokea, polisi lazima wawajibike kuzituliza. Utulizaji wake huwa na matokeo hasi na chanya; kwa maana kwamba upo uwezekano mkubwa wa kusababisha ama majeruhi, vifo au udhalilishaji wa aina mbalimbali.

Inapotokea polisi katika harakati za kulinda amani wakajeruhi au kuua, vidole huelekezwa kwao, kuwa wamekiuka haki za binadamu.

Umma hukwepa kabisa kuangalia upande mwingine wa wanasiasa waliochochea vurugu husika.

Silengi kuwatetea polisi, kwamba siku zote katika udhibiti wa amani lazima wajeruhi au kuua. Natambua kwamba wakati mwingine upo uzembe na makusudi kwa baadhi yao.

Lakini haiondoi hoja kwamba wakati mwingine, wanasiasa wanawaweka polisi katika wakati mgumu kwenye mchakato mzima wa uchaguzi.

Kwa mantiki hiyo, viongozi wa vyama vya siasa waliopo kwenye kampeni Arumeru Mashariki, wanapaswa kubeba dhamana kuhakikisha amani inaendelea kuwapo si tu kwenye kampeni, bali pia siku ya uchaguzi na kutangaza matokeo.

Ikumbukwe, kwamba vitendo vyovyote vya wafuasi katika uchaguzi, msukumo wake unatokana na viongozi wakuu.

Viongozi wakuu ni kama baba katika familia. Mzazi makini hawezi kutetea uhalifu wa mtoto.
Wanapaswa kuwakaripia au kuwaonya wafuasi wao wanapowaona wanafanya vitendo
vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

Wafuasi kupopoa mawe misafara, kuchana bendera na picha za wagombea au kuvamia mikutano ya kampeni ya vyama vingine, wanapaswa kukaripiwa na viongozi wao kabla ya Polisi.

Hata hivyo, viongozi hukaa kimya hali inayodhihirisha kuwa wanawaunga mkono. Isitoshe
makaripio na maonyo, yameshageuka kuwa ya kawaida kutokana na vitendo husika kuendelea kujitokeza kila uchaguzi (hususan uchaguzi mdogo) unaotokea licha ya kanuni za maadili kuwapo.

Umefika wakati wanasiasa hususan viongozi wakuu wa vyama walioko Arumeru Mashariki wazingatie onyo hilo la Polisi.

Walirahisishie Jeshi hilo kazi kwa kukanya wafuasi wao. Wawadhibiti wasifanye vurugu na wasichukue sheria mkononi. Wanasiasa wasipende kuwaingiza polisi lawamani kwa kuchochea vurugu.

No comments: