Dodoma. Suala la kutimuliwa kwa madiwani wanane wa CCM katika Manispaa
ya Bukoba limeingia sura mpya baada ya Kamati Kuu kuwazuia Meya, Dk
Anatory Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki
kushiriki katika siasa mkoani humo hadi mwaka 2015.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa uamuzi
huo umefikiwa baada ya kubainika mgogoro wa viongozi hao, unakiumiza
chama katika jimbo hilo.
Taarifa zilidai chanzo cha ugomvi kati ya Balozi Kagasheki na Dk Amani,
ni kwa kila mmoja kutaka kugombea nafasi ya ubunge Jimbo la Bukoba mjini
katika uchaguzi ujao. Na kwa uamuzi huo, Kagasheki na Dk Amani
hawatashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hata hivyo, akitangaza uamuzi huo jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya
CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema viongozi hao watakutana na
Kamati Kuu leo na baada ya hapo utatangazwa uamuzi uliofikiwa.
Mbali na meya na mbunge huyo ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na
Utalii, wengine walioitwa katika kikao hicho cha leo ni Mwenyekiti wa
CCM mkoani humo, Costansia Buhinye, katibu wake, Averin Mushi pamoja na
mwenyekiti wa chama Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na katibu wake,
Janath Kayanda.
Kutokana na uamuzi huo, Kamati Kuu ambayo ilimaliza kikao chake saa 8:30
usiku wa kuamkia jana italazimika kukaa tena leo kuwaelezea uamuzi
uliofikia.
Kumekuwapo na mgogoro mkubwa katika Baraza la Madiwani wa Manispaa ya
Bukoba, ukimuhusisha Kagasheki na baadhi ya madiwani kwa upande mmoja;
na Dk Amani na kundi jingine la madiwani kwa upande mwingine.
Wakati wa mgogoro huo madiwani wamekuwa wakituhumiana ufisadi, na CCM
imekwishawatuma viongozi wake wa juu kuingilia kati mgogoro huo akiwamo
mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, lakini hakuna mafanikio
yaliyopatikana.
Kufikishwa kwenye Kamati Kuu kwa suala hilo kumekuja baada ya uongozi wa
CCM Mkoa wa Kagera kuamua kuwatimua uanachama madiwani hao, hatua
ambayo ilikuwa inahatarisha nafasi zao na hivyo kukiingiza chama hicho
kwenye uchaguzi mdogo.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo zinasema kuwa kuna uwezekano mkubwa
kwa viongozi hao kuwajibishwa kwa kukiuka kanuni, kwa kuwa upo uamuzi wa
chama unaokataza viongozi waliochaguliwa katika vyombo vya dola
kuwajibishwa kwa staili hiyo.
Madiwani waliovuliwa uanachama na kata zao katika mabano ni pamoja na
Richard Gaspar (Miembeni ), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander
Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe) na Yusuf Ngaiza ambaye pia
ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai).
Wengine ni Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe),
Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo)
Baada ya kutimuliwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema chama Mkoa wa Kagera hawana uwezo wa kuvua uanachama na kwamba
wenye uwezo huo ni ngazi ya taifa.
Nape alisema kwa mujibu wa taratibu za CCM, Mkoa wa Kagera walitakiwa
kuwasilisha tuhuma hizo ngazi za juu ili zijadiliwe na kuamuliwa na
Kamati Kuu (CC).
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu, viongozi wa kuchaguliwa na
wananchi kama wabunge na madiwani, hawawezi kuvuliwa uanachama na vikao
vya chini bali chombo chenye mamlaka hayo ni Kamati Kuu.
Hata hivyo, siku moja baada ya tamko hilo la Nape, CCM mkoani Kagera
kilisisitiza kuwa uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao ni halali, kwa kuwa
ulifanywa na kikao halali kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye, alisema kwa
mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho, hakuna kikao chochote ndani
ya chama kinachoweza kukinzana na kikao kingine kwa hivyo, bado madiwani
hao wamefutiwa dhamana ya uanachama kama mkoa ulivyoamua.
Buhiye alisema kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa ndicho kikao kikuu
chenye uamuzi wa kumwajibisha mwanachama yeyote, iwapo atabainika kwenda
kinyume cha taratibu na kanuni za chama, kwa mujibu wa katiba ya CCM.
Suala la Mansour
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imelipeleka suala la kutimuliwa
uanachama kwa Mwakilishi wa Kiembesamaki Zanzibar, Mansour Yusuf Himid
kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambako litajadiliwa leo na
kutolewa uamuzi.
Nape alisema mamlaka ya mwisho ya kumteua mwakilishi ni NEC, hivyo lisingeweza kujadiliwa na Kamati Kuu.
Source;Mwananchi
No comments:
Post a Comment