Monday, April 16, 2012

JK Atua Sao Paulo Brazil

Rais Jakaya Mrisho kikwete na Mama Salma Kikwete  wakiwasili Jumapili Aprili 15, 2012 katika hoteli ya Tivoli jijini Sao Paulo, Brazil, tayari kwa ziara ya siku tano ya kikazi nchini humo. Kulia ni  Waziri wa kazi na Uwezeshaji Wanachi Kiuchumi na Ushirika wa Zanzibar Mh Haroun Ali Suleiman. Picha na habari: Ikulu.

 Rais Jakaya Mrisho kikwete amewasili  Brazil Jumapili Aprili 15, 2012  kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tano.

Katika ziara hiyo Rais Kikwete anatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Dilma Varna Rousseff wa Brazil  na Rais mstasafu wa nchi hiyo Mheshimiwa Inacio da Silva Lula na viongozi waandamizi wa nchi hiyo.

Katika ziara hiyo, Rais Kikwete atahudhuria mkutano wa mwaka wa wakuu wa nchi zinazoshiriki katika Mpango wa Ubia wa Uwazi Serikalini (Open Government Partnership-OGP) utakaofanyika mjini Brasilia chini ya Uenyekiti wa Rais Rousseff na kuhudhuriwa na wajumbe wapatao mia nne (400) kutoka serikalini, Asasi zisizo za kiserikali, Sekta binafsi pamoja na Mashirika ya Kimataifa.

 Ubia wa Uwazi Serikalini au kwa kifupi OGP,  ni mpango uliozinduliwa  Septemba 2011 mjini New York,  Marekani kwa lengo la kuwapa wananchi nafasi ya kushiriki  katika kuamua mambo yanayowahusu, kupitia vyama visivyo vya Kiserikali na vya Kijamii.

Ubia huu unashirikisha kwa usawa wawakilishi wa serikali kwa upande mmoja na wawakilishi wa Asasi zisizo za Kiserikali za Kijamii kwa upande mwingine. Nchi ya Brazil kwa kushirikiana na Marekani imekuwa mstari wa mbele katika kusukuma ubia huu.

Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia mkutano huo tarehe 17 Aprili, asubuhi mara tu baada ya hotuba ya  ufunguzi itakayotolewa na Mwenyekiti wa mkutano huo Rais Dilma Rousseff wa Brazil, ambapo ataelezea maendeleo iliyofikia katika kuandaa mpango kazi wa kutekeleza ahadi ya kuongeza uwazi kama ilivyokubaliwa katika kikao kilichofanyika Disemba 2011.
Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 20 Aprili, 2012.

JK Akiongea Na Balozi Mulamula

Rais Jakaya Mrisho kikwete akiongea na Msaidizi Mwandamizi wa Rais (Diplomasia) Balozi Liberata Mulamula baada ya mkutano wa maandalizi ya ziara yake ya siku tano nchini Brazil Jumapili Aprili 15, 2012 katika hoteli ya Tivoli jijini Sao Paulo. katikati  ni  Waziri wa kazi na Uwezeshaji Wanachi Kiuchumi na Ushirika wa Zanzibar Mh Haroun Ali Suleiman. 

Karibu Sana Mzee!"


JK akipeana mkono na baadhi ya waliofika uwanjani kumlaki. 

Shada La Maua Ya Brazil

Mke wa Rais Mama Salma kikwete akipokea shada la maua mara baada ya yeye na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwasili Jumapili Aprili 15, 2012 katika hoteli ya Tivoli jijini Sao Paulo, Brazil, tayari kwa ziara ya siku tano ya kikazi nchini humo. Kulia kwake ni Rais Kikwete na nyuma kulia ni  Waziri wa kazi na Uwezeshaji Wanachi Kiuchumi na Ushirika wa Zanzibar Mh Haroun Ali Suleiman na mwenye miwani ni Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Mh Francis Malambugi. Picha: Ikulu
 

No comments: