Wednesday, April 18, 2012

le Millya ang’oka CCM


James Ole Millya
Aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Ole Millya, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Arusha jana alipotangaza uamuzi wake wa kujitoa CCM na kujiunga na CHADEMA. Picha na Eliya Mbonea.
* Atua Chadema kwa mbwembwe
* Asema CCM si baba wala mama yake
* Atema nafasi zote za kitaifa alizokuwa nazo
* Beno Malisa amlilia, ataka vijana watulie

KUMEKUCHA Arusha, ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), James Ole Millya, kutangaza kuachia nafasi hiyo na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Millya alisema, amefikia uamuzi wa kuachia nafasi zote za ngazi ya taifa hadi mkoa alizokuwa akizishikilia ndani ya CCM, baada ya kujiridhisha kuwa chama hicho kimefilisika kisera.

Alisema mbali ya kufilisika kisera, aliifananisha CCM na mtu ambaye anaumwa ugonjwa wa Ukimwi, ambaye siku zote anaishi kwa matumaini tu.

Hadi kujiuzulu kwake, Millya alikuwa akishikilia nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa, Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa na Mjumbe Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha.

Alitaja sababu zilizomfanya aamue kuhama CCM na kujiunga na CHADEMA, kuwa ni pamoja na misukosuko mingi ndani ya CCM ambayo amekuwa akiipitia.

Alisema sababu nyingine, ni kuwekwa chini ya uangalizi wa Kamati ya Nidhamu.

Alisema siku zote, amejitahidi kukemea na kushauri mambo mbalimbali yasiyokijenga chama, lakini bado ameendelea kuonekana hana thamani.

“Siku zote nimekuwa nikikemea mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakihatarisha na kukibomoa chama kwa nia njema na upendo. Lakini nimeendelea kupuuzwa kutokana na CCM kuwa na kikundi cha watu wanaoonekana kukimiliki kama kampuni yao binafsi, alisema Millya.

Wakati akitangaza uwamuzi huo, Millya aliongozana na baadhi ya wafuasi wake, huku baadhi yao wakiwa wamevalia mavazi ya Kimasai.

Katika mazungumzo yake, Millya alinukuu maneno ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyowahi kuyatoa akiwa amestaafu uongozi ndani ya Serikali na chama.

Akinukuu alisema “Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, CCM si Baba wala Mama yangu, hivyo nami leo natangaza kuwa CCM si wazazi wangu kwa maneno hayo, natangaza rasmi kuondoka ndani ya chama hicho na kujiunga na Chadema.

“Nafanya hivi, bila kushawishiwa na yeyote nimefanya haya kutokana na uamuzi wangu binafsi, kwani siku zote nilikuwa natambua na kuona Chadema ndicho chama chenye kuwaletea matumaini mapya wananchi wa Watanzania,” alisema Millya.

Akitolea mfano wa baadhi ya mambo aliyowahi kuyakemea kama mwana CCM, Millya alikumbushia tamko lililowahi kutolewa na UVCCM Mkoa wa Pwani, waliowahi kusema ajaye mwaka 2015, hatatoka kanda ya kaskazini.

Millya alisema tamko hilo, si tu lilikiuka sheria za nchi kutokana na kuonyesha ubaguzi wa wazi kwa Watanzania, bali lilikwenda kinyume na miiko iliyowekwa na waasisi wa CCM, kwa kuonyesha sera za ubaguzi ndani ya chama, zinaonyesha kusimamiwa na kikundi cha watu waliojimilikisha.

“Kweli kama kiongozi, nilisikitishwa na taarifa hiyo na siku zote nilikuwa nikipinga hilo tamko kuwa halistahili ndani ya nchi hii. Lakini mpaka kesho, hakuna chombo chochote kiwe cha chama au Serikali, kilichokemea kauli hiyo ya kibaguzi ndani ya taifa.

“Ikulu yenyewe inayokimbilia kukanusha baadhi ya mambo ya kibaguzi yanayotolewa ama kwa kuihusisha, haijawahi kujitokeza kukemea kauli ya kibaguzi kama ile, kama Rais anatokea Pwani na waliotoa kauli hiyo ni UVCCM Pwani na ndani yao yumo mtoto wa Rais, hapo unategemea nini kama Ikulu haihusiki na tamo hilo,” alisema Millya.

Katika hatua nyingine, aliwarushia makombora baadhi ya vijana na watu wengine ndani ya CCM wanaoendelea kuishi kwa matumaini ya kusubiria kuteuliwa katika nafasi za ukuu wilaya na mkoa, kuwa kamwe kwa upande wake hakuwa ndani ya CCM kutegemea mambo kama hayo.

“Kamwe sikuwa nategemea kuishi kwa matumaini kama muathirika wa Ukimwi, nilipokuwa ndani ya CCM na ndio maana siku zote nilikuwa mstari wa mbele kufanya kile ninachokiamini.

“Kutokana na uamuzi wangu ambao bado naona ni sahihi na nitaendelea kuusimamia niliona, sina sababu ya kuendelea kupanda gari lenye pancha lukuki. Kuamua kwangu kuijiunga na Chadema, ni kuingia au kupanda gari lenye matumaini mapya kwa Watanzania.

Katika siku za hivi karibuni, Millya akiwa mmoja wa wana wa CCM alijitosa katika kura za maoni ndani ya chama hicho, akiomba jina lake liteuliwa kupigiwa kura katika nafasi za wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki.

Hata hivyo, kutokana na kile alichokiamini alidai hakuweza kupigiwa kura kutokana na makundi yasiyokuwa na faida jina lake halikurudi.

Kumbukumbu zinaonyesha, Millya alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM mwaka 2008, ameutumikia umoja huo kwa miaka takribani mitano sasa.

Kutokana na hali hiyo, aliwashukuru vijana wote aliofanya nao kazi na kuahidi kuendelea kushirikiana nao, huku akiwakaribisha Chadema.

“Nawaomba vijana wote ndani ya mkoa wetu wa Arusha na taifa kwa ujumla wenye mapenzi mema na taifa letu, tujiunge na Chadema, kwani ndicho chama chenye tumaini jipya na si CCM”.

No comments: