Sweetbert Lukonge
KOCHA mpya Yanga, Thom Saintfiet amesema atatumia miaka miwili ya mkataba aliosaini jana kuiwezesha klabu hiyo ya Jangwani kuweka historia kwa kutwaa mataji matatu makubwa likiwemo Klabu bingwa Afrika.
Saintfiet, raia wa Ubelgiji alisema angependa kuona Yanga inakuwa timu ya kwanza Tanzania kutwaa ubingwa wa klabu Afrika.
"Nitaanza kutetea Kombe la Kagame, hii ndiyo kazi yangu kubwa ya kwanza, kisha nitaka kurejesha Jangwani ubingwa wa Ligi Kuu," alisema Saintfiet.
Michuano ya Kombe la Kagame inatarajia kuanza Jumamosi ijayo jijini Dar es Salaam, wakati patashika ya Ligi Kuu Bara itaanza baadaye Septemba mwaka huu.
Akiongea mara baada ya kusaini mkataba huo Makao Makuu ya Klabu, Jangwani jijini Dar es Salaam, Saintfiet alisema hakuna linaloshindikana kama atapata ushirikiano.
"Nimekuja Tanzania kufundisha Yanga, nataka ifikie mafanikio. Nataka kuwahahakikishia Yanga kwamba mimi ni chaguo sahihi," alisema Saintfiet.
"Yanga ni timu kubwa Afrika, naifahamu muda mrefu. Nimekuwa nikifuatilia soka la Afrika na hapa Tanzania, Yanga ndiyo iliyonivutia sana."
Kocha huyo mwenye uzoefu na soka la Afrika, alisema atatumia uzoefu wake kimataifa kuleta mageuzi makubwa katika soka la Tanzania kupitia uwapo wake Yanga.
Alisema atawekeza nguvu kwenye sera ya ushindi kwa kila mechi na atakuwa mwepesi wa kufanya mabadiliko timu yake itakapofanya vibaya.
Katika kuhakikisha anafikia mafanikio, atashirikiana vizuri na benchi la ufundi chini ya Kocha Msaidizi, Felix Minziro na Kocha wa Makipa, Juma Mfaume.
Akiongea baada ya pande zote mbili kutia saini, Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa alisema wamefurahishwa na ujio wa kocha huyo kwa vile wanaamini atasaidia kutimia kwa malengo ya klabu.
Mwesigwa alisema, mtazamo wa klabu kwa sasa ni kujikita zaidi kibiashara na kuwekeza kwenye soka la vijana, na wana imani uzoefu wake kimataifa utawasaidia kufikia malengo.
Aidha, Mwesigwa alisema klabu yao itakuwa tayari kumwongeze mkataba pindi huu wa sasa utakapomalizika, lakini hilo likiwezekana kutegemea iwapo malengo ya klabu yatatimia.
Kocha huyo jana alikabidhiwa ramsi timu na kuanza kuifundisha, ambapo kabla alipata fursa ya zaidi ya nusu saa kuongea na wachezaji.
Chanzo: http://mwananchi.co.tz/
No comments:
Post a Comment