Wednesday, August 1, 2012

WALIMU MKOANI RUVUMA WATAKIWA KUREJEA KAZINI.

Walimu wakuu wa shule za ,msingi,sekondari na waratibu elimu kata wakiwa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu aliyesihi kuwahamasisha walimu wote kuacha mgomo na kurejea kazini mara moja.Kikao hiki kimefanyika katika ukumbi wa chuo kikuu huria Manispaa ya    Songea(Picha na Revocatus Kassimba
                                                                                                                                          
Walimu katika mkoa wa Ruvuma wametakiwa kurejea kazini na kuachana na mgomo ambao unawaumiza wanafunzi kwa kuwanyima haki yao ya kupata elimu.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu wakati alipofanya kikao cha pamoja na walimu wakuu wa sekondari,shule za msingi na waratibu elimu kata wa wilaya ya Songea mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Chuo kikuu huria Manispaa ya Songea.
Mkutano huu aliuitisha ili kurejea kauli ya serikali kuwa mgomo unaoendelea mkoani Ruvuma na nchi kwa ujumla si halali kwani suala hilo lipo katika Mahakama Kuu  divisheni ya kazi.
“Nawasihi sana walimu wote rejeeni madarasani wakati huu suala hili likiendelea kushughulikiwa na mamlaka husika” alisema mkuu wa mkoa.
Mkuu wa Mkoa amewapongeza walimu wote ambao toka mgomo huu ulipoitishwa hawajasitisha kutoa Huduma ya kuwafundisha wanafunzi kwani kwa kufanya hivyo wameonyesha uzalendo na heshima kwa serikali ambayo ndiyo mwajili.
Mwambungu alikemea vikali tabia ya baadhi ya viongozi wa chama cha walimu mkoani Ruvuma kupita katika shule na kuhamasisha walimu kugoma na kueleza kitendo  hicho ni utovu wa nidhamu kwani shule zote ni mali ya serikali wala si za chama cha walimu (CWT).
“CWT si mwajili wa walimu bali ni chama cha kitaaluma hivyo kinapaswa kuheshimu maagizo ya mahakama na kusitisha mgomo kwa kuwatakia walimu wote warejee madarasani”
Mwambungu amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa CWT kuwahamasisha walimu kugoma kwa kupita mashuleni ambapo ameeleza kuwa serikali inawafuatilia na watakaobainika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa makosa ya uchochezi.
Aliongeza kusema kuwa uamuzi wa kugoma ni kuwadhurumu watanzania wengi wakiwemo watoto wa shule wasio na makosa hivyo akawasihi walimu wakuu wa shule za msingi , sekondari na vyuo kuwahamasisha walimu wao kurejea kazini kazi ambayo walimu wakuu wamekubali kuifanya ili kurejesha hali ya ufundishaji katika utaratibu wake.

Na Revocatus Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Ruvuma

No comments: