Scolastca Kevela akisaini fomu ya kukataa matokeo
ALIYEKUWA
mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT) wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe, Scolastica Kevela juzi alionja
machungu ya siasa za makundi baada ya kuzomewa kwa nguvu na baadhi ya
wajumbe wa mkutano huo.
Katika
uchaguzi huo ulioonekana kugubikwa na muelekeo wa siasa za Uchaguzi
Mkuu wa 2015, Rosemary Lwiva aliibuka mshindi kwa kujipatia kura 190,
huku Kevela akipata kura 164.
Lwiva
ambaye hata hivyo hakuweza kuthibitisha taarifa hii, anadaiwa kuwa
katika moja ya kundi la wabunge wanaotaka kujisafishia njia ya uteuzi
wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 huku Kevela akionekana kuwa
katika kundi linalotaka kupanua uwanja wa ushindani katika uchaguzi huo
kwa kuziunga mkono sura mpya.
Kuwepo
kwa muelekeo wa siasa za makundi katika uchaguzi huo kwa kiasi fulani
kulidhihirishwa na uwepo wa baadhi ya wabunge wa kiume (majina
yanahifadhiwa) ambao mkutano huo ulikuwa hauwahusu moja kwa moja.
Taarifa
zilizokuwa zimezagaa ndani na nje ya ukumbi wa UWT ulipofanyika mkutano
huo mjini hapa na ambazo zilikanushwa vikali zilidai kwamba mmoja wa
wabunge hao aliyekuwa akimfanyia kampeni mmoja wa wagombea hao
alikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kuambana na Rushwa (Takukuru).
“Hizi
taarifa sio za kweli hata kidogo, zinaenezwa na wapambe wa mmoja wa
wagombea anayejua atashindwa katika uchaguzi huu,” alisema mmoja wa
wapambe wa mbunge huyo.
Alisema
baada ya kusikia taarifa za mbunge huyo kukamatwa walilazimika kwenda
naye katika eneo la mkutano huo ili wale waliokuwa wakivumisha taarifa
hizo kwa lengo la kubadili mtazamo wa wajumbe juu ya uchaguzi huo
waishiwe hoja.
“Tumekuja
naye katika ukummbi wa mkutano huu kama unavyoona, hii ni kudhihirisha
kwamba taarifa zilizokuwa zinaenezwa dhidi yake zilikuwa propaganda,”
alisema.
Tukio hilo la Kevela kuzomewa lilitokea mara baada ya mgombea huyo kupewa nafasi ya kuwashukuru wajumbe baada ya matokeo kutangazwa, majira ya saa 1.30 usiku.
Kevela
aliyeanza kwa kuwaomba radhi wanawake wenzake alisema hakubaliani na
matokeo hayo kwasababu mgombea mwenzake aliyeshinda kiti hicho alitoa
rushwa.
“Sio
kwamba siwaheshimu, mmeona nimetumia muda kujaza fomu ya kukubali au
kukataa matokeo, ukweli ni kwamba huyu mwenzangu aligawa vitenge kwa
wajumbe wa Makete na Ludewa…” alisema na kabla hajamaliza wajummbe
walisimama na kuanza kumzomea.
Zomea
zomea hiyo iliyodumu kwa dakika tatu ilimlazimu Kevela aliyeonekana
kupandwa na hasira kumalizia kwa kusema asanteni na kwenda kukaa nyuma
ya meza kuu.
Alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa na Njombe anayemaliza muda wake, Deo Sanga aliyetuliza jazba za wajumbe na mgombea huyo.
“Ndugu
zanguni hili ndio jeshi litakalotuwezesha kushinda uchaguzi wa serikali
za mitaa wa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu wa 2015,” alisema.
Sanga
ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Kaskazini alisema baada ya uchaguzi huo
wanawake wanatakiwa kuwa kitu kimoja kwa kujenga mshikamano na
kuimarisha umoja wao.
“Vinginevyo
tutajiweka katika mazingira ya kushindwa vibaya katika chaguzi hizo
zijazo na kama manavyojua katika maeneo mengi ambayo wapinzani
wameshinda imetokea hivyo kwasababu ya mgawanyiko wetu,” alisema.
Pamoja
na kutoa rai hiyo, Kevela alisema pamoja na kukataa matokeo hayao ndani
ya siku 14 atakata rufaa kupinga matokeo hayo kwasababu yaligubikwa na
dosari nyingi.(Frank Leonard Blog)
No comments:
Post a Comment