KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeeo( Chadema), Dk
Willbrod Slaa jana alizungumzia kukatishwa kwake tamaa na mahudhurio ya
wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho Jimbo la Kinondoni jijini Dar es
Salaam.Dk Slaa alisema hayo jana wakati wa Mkutano Mkuu wa jimbo hilo baada ya mahudhurio kuwa hafifu.
Alisema asilimia 50 ya mahudhurio ya wajumbe
katika jimbo hilo ni aibu na yanatia shaka iwapo wana nia ya dhati ya
kushika dola mwaka 2015.“Dalili hii inaonyesha kwamba kuna tatizo, hivyo
kupitia mkutano huu tutayamaliza na kurudisha ufanisi wa chama” alisema
Dk Slaa na kuongeza:
“Chadema ni chama ambacho kinajiandaa kushika dola
mwaka 2015, endapo hali hii itaendelea ya wajumbe kutafutana kwa njia
ya simu itakuwa hatari wakati wa kuunda baraza la mawaziri” alisema na
kuongeza:
“Haiwezekani Rais akawa anatafuta baraza la
mawaziri kwa njia ya simu, kwani bila kujipanga wakati huu itakuwa ngumu
huko mbele tunakokwenda,” alisema.Katika mazungumzo yake Dk Slaa alisema,
wanakusudia kutoa tamko la nini ifanyike kuhusu mauaji mbalimbali ya
wananchi yalifanywa na polisi baada ya Rais Jakaya Kikwete kushindwa
kuwachukulia hatua Waziri wa Mambo ya Ndani , Dk Emmanuel Nchimbi, Mkuu
wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema na Kamanda wa Mkoa wa Iringa
Michael Kamhanda.
“Hatuwezi kutulia huku tukiona vyombo ambavyo
vinatakiwa kulinda usalama wa raia ndio vinakuwa vya kwanza kuwaua raia
wasiokuwa na hatia huku kiongozi wa nchini (Rais Kikwete) akiwa kimya
bila kutoa tamko lolote,” alisema.
Katika mkutano huo, wajumbe walitakiwa kufika
mapema kwa ajili ya kuanza kwa mkutano saa 4 hadi saa 6 mchana, lakini
kutokana na ufinyu wa mahudhurio, mkutano huo ulianza saa 6.47 mchana.
Sifa zimwendee Mwenyekiti wa Chama hicho Jimbo la
Kinondoni, Deo Mushi ambaye alifanya kazi ya kuwatafuta wajumbe hao kwa
njia ya simu ili kutimiza idadi ya asilimia 50.
Mratibu wa Mkutano huo, Mkurungenzi wa Sera na
Utafiti wa Chama hicho, Chacha Mwita, alisema wajumbe waliokuwa wamefika
walikuwa hawana uwezo wa kuruhusu kufanyika kwa mkutano huo.
Mwita alisema idadi ambayo inatakiwa ya wajumbe wote ni zaidi ya 120, lakini waliokuwa wamefika walikuwa hawazidi 50.
Soma zaidi: http://www.mwananchi.co.tz
Soma zaidi: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment