Sehemu ya Bandari ya Dar es
Salaam nchini Tanzania ambayo hutumiwa na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki
kupokelea bidhaa zao.
Uchumi katika
kanda ya Afrika Mashariki uliendelea kuimarika mwaka uliopita, 2012
licha ya changamoto lukuki iliyokabiliana nazo.Kanda nzima ilionyesha
uchumiwake kukua kwa nguvu na kusukuma juhudi za kuimarisha mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
EAC inajumuisha nchi tano
wananchama ikiwa ni pamoja na Kenya,Uganda, Tanzania, Rwanda na
Burundi, Mwandishi Isaac Mwangi wa Shirika Huru la Habari la Afrika
Mashariki (EANA) anaadika zaidi katika Makala haya:
Kwa mujibu wa taarifa rasmi
zinazotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kila baada ya miezi
mitatu, pato la mwaka katika robo ya kwanza ya mwaka uliopita
liliongezeka kwa asilimia 7 katika nchi za Rwanda na Tanzania na kiasi
kikubwa cha kuongezeka kwa pato pia liliripotiwa nchini Uganda.
Uganda iliripoti pato chanya la
kukua kwa uchumi wake katika robo ya kwanza ya mwaka 2012 kufuatia
kukua kwa hasi kwa uchumi wake katika robo ya mwisho ya mwaka 2011.
Uchumi wa Burundi kwa upande wake
uliendelea kuathirika vibaya kutokana na mambo mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kuongezeka kwa mfumuko wa bei,kushuka kwa makusanyo ya mapato
ya serikali na wabia wa maendeleo kujitoa kuunga mkono juhudi za
serikali.
Viashiria vya uchumi katika kanda hiyo ya Afrika Mashariki, vimeonyesha dalili kubwaya
kukua kwa uchumi wa kanda hiyo katika robo ya kwanza ya mwaka jana,
ikiwa ni pamoja na kwenye sekta za huduma nchini Rwanda na viwanda
nchini Uganda na Tanzania.
Hali ya kushuka mara kwa mara kwa
thamani ya fedha katika kanda hiyo pia ilipungua katika kipindi chote
cha robo ya pili ya mwaka 2012 ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa sera nzuri
za fedha zilizowekwa na mamlaka za udhibiti wa fedha katika kanda.
Viashiria vingine vya kupungua kwa
mfumuko wa bei ni pamoja na kupungua kwa bei ya mafuta na mavuno
mazuri ya vyakula yaliyotokana na hali nzuri ya hewa na kuimarisha
mikakati ya uzalishaji kama vile Mpango wa Kuimarisha Mazao nchini
Rwanda na Kilimo kwanza nchini Tanzania.
Pia viwango vya wastani vya
ubadilishanaji wa fedha za kigeni umepunguza makali ya kuleta mfumuko wa
bei miongoni mwa nchi wananchama.
Utafiti uliofanywa na jarida moja la African Business Magazine
umebaini kwamba ukuaji endelevu wa uchumi wa Tanzania unatokana na
uendeshaji mzuri wa makampuni kwa kufuata sheria na taratibu na hivyo
kuongeza idadi ya makampuni ya Kitanzania katika Kundi la Makampuni 25
ya Juu Afrika Mashariki kutoka matatu yaliyokuwepo hadi sita katika
kipindi cha mwaka mmoja tu.
Kampuni ya Azam ni moja ya vielelezo tosha vya Ukuaji wa Uchumi kwa
Kanda ya Afrika Mashariki hasa nchini Tanzania kutokana na jinsi kampuni hiyo
ya uzalishaji wa Bidhaa mbalimbali za Chakula inavyofanya kazi zake katika Nchi
za Afrika Mashariki
Kwa upande mwingine uchumi wa
Kenya haukukua kwa kasi kama nchi nyingine za Afrika Mashariki na
badala yake ilipata ongezeko la ziada la idadi ya watu. Uchumi wa
Uganda umeongezeka kutokana na matarajio ya kupata mafuta nchini humo.
Kenya imeripoti kukua kwa uchumi
wake kwa kiwango cha chini zaidi cha asilimia 3.5 katika kipindi cha
miaka minne iliyopita. Kiwango hicho kinashindana kihafifu na ukuaji
kwa nchi nyingine za kanda hiyo. Rwanda asilimia 7.9, Uganda asilimia
7.2 na Tanzania asilimia 6.7. Kenya pia amejikuta ikiwa na kiwango
kikubwa zaidi cha mabadiliko ya mfumuko wa bei kutoka asilimia 19.7
Novemba mwaka jana hadi kufikia asilimia 4.1 mwezi huu.
Ufanisi wa uchumi wa Kenya kwa
mwaka huu wa 2013 utapatikana kwa kiasi fulani kutegemeana na jinsi
gani nchi hiyo itakavyoendesha uchaguzi wake mkuu mwezi Machi.Kwa kuwa
ndiyo nchi yenye nguvu zaidi za kiuchumi katika kanda hiyo,ufanisi wake
pia utaathiri nchi nyingine wananchama wa EAC.
Nchini Burundi, mfumuko wake wa
bei umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka kutoka asilimia 25.2 mwezi Aprili
(ikiwa ni kiwango cha juu zaidi Afrika Mashariki) hadi asilimia 17.3
mwezi Juni kutokana na kushuka kwa bei za vyakula. Hatua ya kupungua
kwa mfumuko wa bei za vyakula inatokana na juhudi za serikali kuondoa
kodi za vyakula vya msingi vinavyoingizwa nchini humo kutoka nje.
Hatua hiyo ambayo ilianza
kutumika tangu Mei 15, iliishia Desemba 31, mwaka jana. Bidhaa za
vyakula zilizohusika kutotozwa kodi ni pamoja na unga wa muhogo,
mahindi na mtama na maharage, mchele, viazi,samaki na mafuta ya
alizeti. Mavuno mazuri ya mazao ya vyakula pia yamesaidia kupungua kwa
bei za vyakula.
Licha ya kuongezeka kwa hofu ya
vitendo vya ugaidi,sekta ya utalii ilifanya vizuri huku kukiwa na idadi
kubwa ya hoteli mpya na maeneo ya kupumzikia yaliyofunguliwa ili
kuendana na idadi kubwa ya watalii waliokuwa wanamiminika ndani ya
kanda hiyo ya EAC.
No comments:
Post a Comment