Monday, July 30, 2012

WATAKA HATI MILIKI YA MMEA WA OLOISUKI AMBAO UNATENGENEZA CHAI

 
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Loiborsoit Integrated Rural
Development Organisation (Lirdo) la Kijiji cha Loiborsoit A,Kata ya
Emboreet Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara limeomba ubalozi wa Uswis kuwawezesha kupata hati miliki bunifu ya mmea wa Oloisuki ambao maganda yake yanatengeneza chai.

Akisoma risala mbele mwakilishi wa balozi wa Uswis hapa nchini,Katibu mkuu wa Lirdo Thaddeus Ole Orpiay alisema kupitia Lirdo wameandaa kitaalamu maganda ya tunda la mti wa Oloisuki (mjafari) Knob Tree (Kibaiolojia inaitwa Zanthoxylum ghalybeum) kwa kutengeneza chai au kuongeza ladha ya vinjwaji vya matunda.

Ole Orpiay alisema kupitia maganda ya matunda hayo ya mmea wa Oloisuki wameweza kubuni na kuandaa kitaalamu maganda ya mti huo na wanasafirisha hadi nchini Uswis kwenye soko la uhakika hivyo wapatiwe hati miliki bunifu.

Aliuomba ubalozi huo uwawezeshe kupatiwa hati hiyo ili kuhakikisha kuwa jamii ya kimasai inafaidika kutokana na rasilimali hiyo na siyo kufaidisha watu wengine wachache ambao hawahusiki.

Alisema mwaka 2006 waliingia ubia na asasi ya Enkaina e retoto
(helping hands) au mikono saidizi ili kuwatafutia masoko na
kushirikiana kutekeleza mradi huo pamoja na kuwafanyia utafiti.

"Mradi huu unawafaidisha wanawake 180 wa jamii ya kimasai waliotoka kwenye familia masikini na lengo letu ni kuwanufaisha wanawake 500 au zaidi ili kupambana na umasikini na kuongeza ajira," alisema Ole Orpiay.

Aliuomba ubalozi huo kuwasaidia fedha za uendeshaji wa mafunzo ya utunzaji mazingira kwenye vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Tarangire ambapo miti ya Oloisuki hustawi kwa wingi.

Akizungumza na wakazi wa Loiborsoit A,Mwakilishi wa balozi wa Uswis Geraldine Zeuner ambaye ni mkuu wa shirika la maendeleo na misaada la Uswis alilipongeza shirika la Lirdo kwa kuwanyanyua kiuchumi wanawake hao 180.

Zeuner alisema atahakikisha wanafanikisha maombi yote
yaliyowasilishwa kwao yaliyopo ndani ya uwezo wao kwani kwa muda wa siku tano alizokaa Loiborsoit A ameuona mti wa Oloisuki na kubaini changamoto zilizopo.

"Kupitia kinywaji cha Oloisuki tumeweza kutengeneza urafiki baina ya wakazi wa Loiborsoit na watanzania kwa ujumla na watu wa Uswis hivyo tumekuwa daraja la kutuunganisha sote," alisema Zeuner.

No comments: